MASIMULIZI
Thursday, April 3, 2014
TEN CHAPTERS SEHEMU YA 3
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
"Sijui kwa nini nimempa kuku wangu mzima na mimi kukosa kitu cha kula kwa usiku huu.I'm so stupid kwa sababu nimempa mwanamke kuku mzima ambaye atamla na mwanaume mwenzangu.Du ! sijawahi kufanya ujinga wa namna hii..I'm so stupid" akasema Genes huku akijipiga kichwa kwa mikono yake halafu akainuka na kuelekea jikoni kuangalia ni kitu gani ambacho angeweza kula kwa usiku huo.Hakuona kitu chochote cha kula hivyo ikamlazimu kuvaa viatu na kutoka kwenda kutafuta kitu cha kula .Alikuwa amechukia sana.
Genes alikwenda sehemu wanakouza chakula akaagiza chips na kuendelea kula lakni mawazo yake yote yakiwa kwa Naomi.Kabla hajamaliza kula ikangai meseji katika simu yake Akaichukua na kuisoma.Ilitoka kwa Naomi.Akasonya na kisha akaifungua na kuanza kuisoma
"Genes umetoka? Nimekuja kugonga mlangoni kwako ili tupate chakula wote lakini sijajibiwa.Kama uko ndani njoo huku kwangu nimepika chakula tule wote" Genes akairudia tena kuisoma meseji ile akatafakari kisha akaamua kutokuijibu.
Alipomaliza kula akaanza safari ya kurejea nyumbani kwake.Mlango wa chumba cha Naomi ulikuwa wazi lakini hakuwa na hamu hata ya kutaka kuchungulia ndani .Moja kwa moja akaenda chumbani kwake na kuufunga mlango akapanda kitandani kulala kwani tayari siku yake ilikwsha haribika
ENDELEA……………………………………………………….
Dakika kama kumi hivi toka Genes arejee chumbani kwake ukaingia ujumbe mfupi katika simu yake.Akaichukua na kuutazama ujumbe ule ulitoka wapi.Ulitoka kwa Naomi.Ujumbe ulisomeka hivi
" Genes mbona hujanijibu? bado nakusubiri ili tule chakula.Nimepika chakula cha watu wawili.Naomba unijibu tafadhali" Genes akatafakari na kuamua kumjibu Naomi
" Mimi nimetoka kula mgahawani.Nilitaka tule wote lakini niliogopa baada ya kumkuta mumeo mpya.Sikutaka kukuletea matatizo.Nashukuru Naomi naomba uendelee kula mimi sintakuja"
akausoma tena ujumbe ule akaridhika kisha akautuma
Baada ya dakika moja ukaingia tena ujumbe toka kwa Naomi
" Genes uliogopa bure ,yule si bwana wangu.Yule ni kaka yangu wa kuzaliwa tumbo moja na alikuja kunitazama baada ya kumtaarifu kwamba nimeachana na yule bwana wangu.Kaka yangu yule anafanya kazi mamlaka ya mapato na alikuja kuniona kama nina tatizo lolote anisaidie kwa sababu katika famila yetu tuko watoto wawili tu." Genes akatabasamu baada ya kuusoma ujumbe ule mfupi kisha naye akaandika ujumbe wa kumjibu Naomi
" Samahani sikujua kama yule ni kaka yako.Nilifikiri labda ni mume mpya.Nisamehe kwa kukufikiria vibaya Naomi" akautuma ujumbe ule na baada ya muda ujumbe ukaingia tena toka kwa naomi
" Genes mimi ni mwanamke ninayejiheshimu sana tofauti na unavyonifikiria.Nashukuru hata hivyo kwa kuniona ni mtu mwenye tabia za kubadilisha wanaume.Sikutegemea kama ungeweza kunifikiria hivyo"
Genes akajilaumu sana kwa
kumuwaza Naomi kwa ubaya namna ile.Alitambua kwamba Naomi alikwisha chukia kwa hiyo akaanza juhudi za kumpooza.Akaamua kumpigia simu ambayo ikaita bila kupokelewa.akapiga tena lakini simu ikaita na haikupokelewa.Genes akainuka na kukaa kitandani
" Nimeshharibu kila kitu.Naomi amechukia na hataki hata kuipokea simu yangu.Kwa nini lakini niliamua kumweleza vile? Sikupaswa kumwambia vile.Wivu wangu wa kijinga sasa umeniharibia kila kitu.Sijui nitamwambiaje ili aweze kunielewa na
kupunguza hasira zake.Akawaza sana na kisha akaamua kuandika ujumbe mfupi wa maandishi.
"Naomi nafahamu umechukia sana kwa maneno niliyokuambia.Nakuomba usikasirike tafadhali.Nisamehe kama nilikuudhi halikuwa lengo langu kufanya hivyo.Nilipomuona yule kaka yako ni kweli nilifikri labda ni mtu wako na nikajisikia vibaya kwa sababu baada ya kuachana na yule bwana wako nilitegemea kwamba ungekaa mwenyewe na kujijenga kwanza.Nakujali na sipendi mwanaume
yeyote akulaghai kama yule uliyeacha naye.Nadhani umenielewa.Ulale salama" akausoma ujumbe ule na kuhakikisha kwamba uko safi kisha akautuma halafu akajifunika shuka na kutafuta usingizi.
Naomi alipoupata ujumbe ule wa Genes alitabasamu.
" Sasa nimeamini kwamba Genes ananijali na kuna kila dalili kwamba ananipenda kwa sababu kama asingekuwa na hisia za kimapenzi juu yangu asingekuwa na wivu kwa kaka yangu."
" Hizi ni dalili njema sana kwangu.Ninampenda Genes na sasa nimeamini hata yeye ananipenda.Kitakachofuata sasa ni kuanza kumfahamu kiundani.Nataka kuzifahamu tabia zake zote za ndani na nje.Nitaweza kuzifahamu tabia zake iwapo nitakuwa na mazoea naye ya karibu." akawaza Naomi huku akitabasamu na kuufunga mlango wake akapanda kitandani kulala.
**************************************************
Ni siku ya Jumanne asubuhi na mapema Genes alikwisha amka na kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini.Kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi sana kutokana na Naomi kukasirika jana yake wakati wakijibizana kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi.Kichwa kilimuuma sana ni namna gani anageweza kumpooza Naomi ambaye hakutaka hata kupokea simu yake.Alifikiria jinsi ya kuendelea kuudumisha urafiki wao ulioanza kukua kwa kasi.Wakati akiwaza huku akijiandaa kwenda kazini mara mlango wake ukagongwa.Ilikuwa ni asubuhi sana na hakujua ni nani ambaye alikuwa akimgongea mlango.Akaufungua mlango na kukutana na sura yenye tabasamu ya Naomi.Genes akajikuta akitabasamu
" Ouh Naomi..habari yako" akasema Genes
" Umeamkaje Genes" akasema Naomi ambaye mkononi alikuwa ameshika mfuko
" Nimeamka salama" akasema Genes huku akitabasamu
" Genes huu mzigo wako.Ni shea yako niliyokuwa nimekuandalia jana.Kula kabla hujakwenda kazini" akasema Naomi huku akitabasamu na kumfanya Genes acheke kidogo huku akiupokea mfuko ule halafu Naomi akaondoka zake.Ndani ya mfuko ule kulikuwa na chakula kilichopikwa usiku na Genes akagoma kwenda kula.Genes akatabasamu na kukiweka chakula kile jikoni.
kisha akaondoka na kuwahi kazini kwake.
Siku hii alishinda mwenye furaha kuzidi siku iliyotangulia.Kitendo cha Naomi kumletea chakula asubuhi kilimdhihirishia kwamba hakuwa amekasirika tena.Wakati wa mapumziko ya mchana Genes akamuandikia Naomi ujumbe mfupi
wa maandishi
" Naomi nashukuru kwa chakula ambacho kimenipa nguvu na sihitaji kula tena mchana.Samahani kwa kutokuja kula jana ila naomba uniruhusu niilipe siku ya jana kwa kukualika kwa chakula cha usiku siku ya jumammosi kama utakuwa na nafasi" Genes akautuma ujumbe ule na baada ya muda mfupi ujumbe toka kwa Naomi ukarejea.
" Nashukuru Genes lakini sintakuweo kwa siku kadhaa.Nimepata safari ya kikazi nitarudi jumamosi.Kama hutajali naomba tufanye jumapili"
Genes akatabasamu halafu akaandika ujumbe wa majibu
" Nashukuru kwa kukubali mwaliko wangu.hakuna shaka tutapata chakula cha usiku siku hiyo ya jumapili.Safari njema " akautuma ujumbe ule na baada ya dakika moja ukarejea ujumbe
toka kwa Naomi ukisomeka
" Ahsante"
Genes akatabasamu na kujawa na furaha kubwa moyoni.
**************************************************
Ilikuwa ni wiki ndefu sana kwa Genes.Siku hizi chache ili kufika jumapili aliona ni zaidi ya miezi.Aliisubiri kwa hamu kubwa siku ya jumapili ambayo angepata chakula cha usiku na msichana mrembo Naomi.Maandalizi yote yalikamilika kabla ya siku ya jumapili ikiwa ni pamoja na kuweka oda maalum ya chakula cha watu wawili katika moja ya hoteli kubwa na nzuri yenye hadhi ambayo aliamini ingewafaa yeye na Naomi.Ni siku ambayo Genes alikuwa ameipanga kuanza rasmi mbio za kumpata mrembo huyu aliyeupeleka mbio moyo wake.
" Nataka niutumie usiku wa kesho kuanza rasmi kinyang'anyiro cha kumpata Nami.Nasema ni kinyang'anyiro kwa sababu najua si mimi pekee ambaye nina ndoto za kuwa na mrembo yule baada ya kuachana na mpenzi wake.Nafahamu wako watu wengi ambao wangependa kuitumia nafasi hii kumpata mrembo yule.Nitajitahidi kila niwezavyo kujaribu bahati yangu na kama ni mapenzi ya Mungu mimi niwe naye basi nitakuwa naye.Nataka nimfanyie vitu vya tofauti kabisa na alivyokuwa akifanyiwa na yule mpenzi wake.Nataka afahamu kwamba katika hii dunia bado wako wanaume wengi wenye kujua kupenda na kujali, wenye kuweza kumpa raha za dunia hii." akawaza Genes akiwa kitandani amejipumzisha.Ilikuwa ni siku ya jumammosi siku ya mapumziko. Siku hii aliitumia kufanya maandalizi kwa ajili ya siku ya kesho.Mpaka saa mbili za usiku bado Naomi hakuwa amerejea nyumbani toka safari.Hali hii ikaanza kumpa Genes wasi wasi mwingi
" Itakuwaje kama hatarudi leo? ..Nina hakika lazima atarudi leo kwa sababu Naomi hawezi kunidanganya.Hata kama ni usiku wa manane lazima atarejea tu." akawaza Genes
" Lakini kwa nini nisimpigie simu ili nifahamu kama atarejea leo au vipi?
akawaza Genes halafu akaichukua simu yake na kutafuta namba za Naomi akapiga lakini alijibiwa kwamba simu anayopiga haikuwa ikipatikana .Akajaribu tena kwa mara ya pili na ya tatu lakini jibu likawa ni lile lile.Akavuta pumzi ndefu na kuamua kujilaza kitandani.
***********************************
Hatimaye ikawadia siku ya jumapili.Siku ambayo Genes alikuwa akiisubiri kwa hamu kubwa.Asubuhi na mapema Genes akaamka na kuanza maandalizi ya kuhudhuria ibada huku akiwa na mawazo mengi kama Naomi alirejea usiku .Alitoka nje na kujaribu kuchungulia mlangoni kwa Naomi lakini hakukuwa na dalili zozote za kuwepo Naomi hapo nyumbani,akazidi kupatwa na wasi wasi mwingi.
" Ina maana Naomi hajarejea? ... Alijiuliza swali hili bila kupata majibu.Furaha yote aliyokuwa nayo ikaanza kutoweka.Akaoga na kujiweka tayari kuondoka kuwahi kanisani kwa ajili ya ibada.Wakati akijiandaa kuwahi ibadani ujumbe mfupi wa maandishi ukaingia katika simu yake.Akaichukua simu yake na kuusoma ujumbe ule.Ulikuwa umetoka kwa Naomi
" Habari yako Genes..Nimeona nikujulishe kwamba tayari nimesharudi ili usiwe na wasi wasi." Genes akatabasamu baada ya kuusoma ujumbe ule akaketi sofani na kuandika ujumbe wa majibu.
".Pole kwa safari Naomi.Nashukuru umerudi salama.Bado unakumbuka ahadi yangu ya siku ya leo?
Genes akautuma ujumbe ule na baada ya muda mfupi Naomi akajibu.
" Ninakumbuka .saa ngapi umepanga tutoke?"
Genes akatabasamu na kujibu
" Saa moja kamili za jioni"
baada ya muda mfupi Naomi akajibu.
" Sawa.Nitakuwa tayari muda huo"
Uso wa Genes ukapambwa na tabasamu zito.Akasimama ndani ya chumba chake kwa dakika kadhaa akiwaza huku akitabasamu na kisha akatoka na kuwahi katika ibada ya asubuhi.
" Saa tatu za asubuhi ibada ikamalizika lakini kwa Genes hakuwa ametoka na kitu chochote katika ibada ile kwa sababu katika muda wote wa ibada mawazo yake yote yalikuwa kwa Naomi.Alikuwa akiwaza usiku utakavyokuwa.Moja kwa moja baada ya kutoka ibadani Genes akaelekea nyumbani kwake kujiandaa na jioni.
Saa nne za asubuhi Naomi akaamka .Alihisi uchovu mwingi sana.
" Kama si Genes kuniomba kutoka na mimi nikamuahidi
siku ya leo wala nisingerudi.Namheshmu sana Genes na siwezi kumuangusha.Iwapo nisingerudi leo sidhani kama angenielewa." akawaza Naomi akawasha redio yake na kuweka muziki laini akarudi tena kitandani.
" Sijui ni kwa nini Genes ameanza kuniingia akilini namna hii.Kila siku siachi kumuwaza.Ni kijana mzuri kusema ukweli na hana sifa yoyote mbaya.Ana heshimika na kila mtu ni kijana mtaratibu,mcheshi mtanashati na mwenye tabia njema.Sijui ni kwa nini ninazidi kuvutika kuwa karibu naye toka siku ile aliyoamua ugomvi wangu na Sheddy." akawaza Naomi huku akiendelea kujigeuza pale kitandani.
" Inaonekana hata yeye pia amevutika nami ..au ni kwa sababu siku ile alinikuta nikiwa na nguo ya ndani pekee?" Naomi akawaza halafu akaona aibu kidogo baada ya picha ya tukio lile la Genes kumkuta akigombana na Sheddy huku wakiwa na nguo za ndani pekee kumjia kichwani.
" Nasikia aibu sana kila nikikumbuka kuhusu tukio lile.Lakini pamoja na hayo siwezi kuzizuia hisia hizi za kutaka kuwa karibu na Genes.Ninahisi ninahitaji sana kampani yake.Nikiwa naye ninajisikia furaha sana.Usiku wa leo utakuwa ni kipimo halisi cha hisia zangu kama ni za kweli ama la.Nitautumia usiku huu kumfahamu vizuri Genes ni kijana wa namna gani hasa." akawaza Naomi akainuka na kuanza kutafuta nguo nzuri itakayompendeza kwa ajili ya usiku wake na Genes.
TUKUTANE TENA SEHEMU IJAYO
KWA SIMULIZI ZAIDI TEMBELEA HAPA MASIMULIZI
0 comments:
Post a Comment
Followers
MAHABA
SERENA
BEFORE I DIE
I DIED TO SAVE PRESIDENT
FAIDIKA NA MASIMULIZI
DEATH MESSENGER
CHOMBEZO ZA MASIMULIZI
MISS TANZANIA PART 2
Blog Archieves
April 2014
(57)
About Me
pettysean.blogspot.com
View my complete profile
Total Pageviews
BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU
Powered By
masimulizi
0 comments:
Post a Comment