Tuesday, April 1, 2014

TEN CHAPTERS SEHEMU YA 1



            "Jamani majirani naomba mnisaidie ananinua hukuuuuu !!!!!!! Sauti ya mwanamke akilia akiomba msaada ikamstua Genes aliyekuwa mezani akinyoosha nguo kwa ajili ya kuwahi ibada ya pili inayoanza saa nne za asubuhi.
Akaizima pasi na kutulia kwa  sekunde kadhaa ili asikie ni wapi ilikokuwa ikitoka sauti ile.Kwa mbali akasikia kama sauti za watu wakizozana.Akapunguza sauti ya redio ili aweze kusikia vizuri sauti zile zilitokea wapi.Aliamini sauti zile za kuzozana zilitoka katika moja ya chumba cha wapangaji wenzake lakini hakuwa na uhakika ni chumba kipi.Sauti ya mwanamke akilia ikasikika tena na safari hii akaamua kuzima kabisa redio yake ili asikie vizuri.
            "Jamani nisaidieni ananiuaaa..!!!!!! sauti ile ya mwanamke ikarudia tena kuomba msaada .Genes akaitambua sauti ile ,ilikuwa ni ya msichana jirani yake aitwaye Naomi anayefanya kazi katika hoteli ya kitalii ya Mbuni lodge..
            "Nini kimetokea leo? Naomi na mumewe wanapigana ? Mbona siku zote wamekuwa wakiishi kwa amani ? akawaza Genes na kufungua mlango wa chumba chake akatazama kama kuna mtu yeyote pale uani ambaye alikuwa akiufuatilia ugomvi ule lakini hakukuwa na mtu yeyote yule ambaye alionyesha kujali watu wale waliokuwa wakipigana.Milango yote ya vyumba vya wapangaji wengine ilikuwa imefungwa na ilionyesha walikuwa wametoka .
            Naomi na mumewe Sheddy walikuwa wakiishi chumba cha jirani na Genes.Wakati akijishauri afanye nini mara akasikia kishindo  kikubwa katika ukuta uliounganisha chumba cha Naomi na chumba chake.
            "Watauana hawa.Ngoja nikawaamue" akawaza Genes ,na taratibu akatoka chumbani kwake na kuelekea katika chumba cha Naomi.Akajaribu kugonga mlango kwa nguvu na kisha akaisikia sauti ya Naomi toka ndani.
            "Ingieni mlango haujafungwa"
 Genes akakinyonga kitasa na kuingia ndani.Ghafla akajikuta amefunga breki za ghafla kwa kitu alichokishuhudia. Naomi na mumewe Sheddy walikuwa wakipigana wakiwa wamevaa nguo za ndani pekee.Naomi alikuwa amevaa chupi ndogo nyeupe na  sidiria nyeupe iliyoyafunika matiti yake madogo na kuyafanya yasimame na kutamanisha.Kwa sekunde kadhaa Genes alibaki amesimama amepigwa na bumbuwazi na macho yake yalikuwa yameelekea katika mwili ule mwororo,mweupe wa Naomi. Kwa jinsi alivyokuwa akiheshimiana na Naomi Genes akaingiwa na woga  na kutaka kurudi nje
            "Genes nisaidie anataka kuniua huyu" Naomi akaomba msaada.Genes akasitisha kitendo alichotaka kukifanya cha kurudi nje.Badala ya kuwaamua akabaki amemkodolea macho Naomi .
            "Genes nakuheshimu sana nakuomba tafadhali utoke ndani mwangu haraka .Usijaribu kuingilia mambo yasiyokuhusu." Sheddy mume wa Naomi akasema kwa ukali na kumstua Genes ambaye alikuwa ameyaelekeza macho yake kwa Naomi akiusaili mwili ule wenye kutamanisha..
            "Genes usimsikilize huyu shetani...nisaidie ananiumiza !!! Naomi akapiga ukelele.
            "Sheddy tafadhal..............." Genes akajaribu kutamka kitu lakini Sheddy akamzuia
            "Genes nakwambia toka humu ndani mwangu haraka sana.Nani kakupa ruhusa ya kuingia humu ndani? Ugomvi wangu mimi na mke wangu unakuhusu nini? tafadhali ondoka haraka sana kabla sijakufanyia kitu kibaya " Sheddy akasema kwa ukali huku ameikamata mikono ya Naomi kwa nguvu
            "Genes nisaidie ananiumizaa!!!!! .....Naomi akalia huku akijitahidi kujitoa katika mikono ya Sheddy.Genes akamuonea huruma Naomi alivyokuwa akilia akashikwa na hasira
            " Sheddy nakuomba tafadhali usiendelee kumpiga mkeo.Nakuomba ndugu yangu niko chini ya miguu yako muache mkeo.Unamuumiza " Genes akasema taratibu akijaribu kumsihi Sheddy amuachie mkewe.
            "Genes naona hujanifahamu vizuri mimi ni nani.Nimekwambia ugomvi wangu mimi na mke wangu unakuhusu kitu gani? Tafadhali ondoka humu ndani mwangu haraka." Sheddy akafoka.
            "Mshenzi wewe humu ni kwako? Una kitu chochote unachoweza kusema ni chako humu ? " Naomi akamwambia Sheddy kwa ukali.Kwa hasira Sheddy akamnasa kibao kizito.
            "Malaya mkubwa wewe..nimekwisha kuonya siku nyingi juu ya matusi yako unayonitukana.Umepata kiburi baada ya mwanaume wako kuja kukusaidia? Ngoja sasa niwaonyeshe adabu wewe na malaya mwenzako" Sheddy akasema kwa ukali.Kauli ile na kitendo cha kumnasa Naomi kibao vikamkasirisha sana Genes.Kwa nguvu akamvaa Sheddy na kumsukuma akaangukia kitandani.Naomi akaitumia nafasi hiyo kuchukua kitenge na kujifunga kisha akatoka nje huku akilia
            "Inuka sasa upigane na mimi wewe si kidume?Nakwambia inuka upigane na mwanaume mwenzako" Genes akasema akiwa amefura kwa hasira.
            "Genes nimekwambia toka ndani mwangu haraka sana.Nitakuitia mwizi sasa hivi!!! akasema Sheddy kwa ukali akiwa amekaa kitandani
            "Nimekwambia inuka unipige mimi badala ya mkeo...." akasema tena Genes kwa kujiamini
            "Genes nimekwambia toka ndani mwangu.Unaingilia mambo yasiyokuhusu kwa nini? Ugomvi kati yangu mimi na mke wangu unakuhusu nini?Halafu huna hata adabu unaingia ndani mwangu bila hodi na kutukuta tukiwa watupu" akafoka Sheddy
            "Hata kama ni mkeo,hupaswi kumpiga kama mnyama.Nimekufahamu muda mrefu sana lakini sikutegemea kama unaweza ukafanya kitendo cha aibu kama hiki cha kumpiga mkeo bila huruma.Umenishangaza sana Sheddy.Kwa taarifa yako ni kwamba siku  hizi wanawake hawapigwi kama unavyofanya.Wanawake wameamka na wanadai haki zao.Akikupeleka katika vyombo vinavyohusika na haki za wanawake unaweza ukachukuliwa hatua kali sana." Genes akasema na kuanza kuipunguza jazba aliyokuwa nayo.
            "Genes wewe huna mke na huelewi matatizo tunayokumbana nayo sisi watu tunaoishi na wanawake ndani.Siku ukioa ndiyo utafahamu haya ninayokwambia.Huyu Naomi unayemtetea amebadilika sana siku hizi.Amekuwa na kiburi cha ajabu .Sijui ni kwa nini amebadlika namna hii.Ninahisi kuna mwanume amempata ambaye anampa kiburi.Naomi hakuwa hivi.Naomi hakuwa mtu anayesimama na kujibizana na mimi" Sheddy akasema
            "hata kama amekukosea Sheddy hukupaswa kumpiga.Kama mwanaume ulitakiwa uwe na busara ukae chini na mkeo na muongee kama mke na mume na kisha muyamalize matatizo yenu na maisha yaendelee.Ninamfahamu Naomi vizuri na sidhani kama ana tabia kama hizo unazohisi anazo.Mbona mkeo ni mtu anayejiheshimu sana tofauti na wanawake wengine hapa mtaani.Jaribu kukaa na mkeo muongee na muyarekebishe yale yote yaliyotokea.Mnapopigana mnajiabisha ninyi wenyewe.Mnawafaidisha majirani ambao wanabaki wanawacheka kila mpitapo.Tafadhali ndugu yangu nakuomba kama mwanaume mwenzangu kaa na mkeo na mjaribu kutafuta suluhu ya matatizo yenu." Genes akasema na mara mlango ukafunguliwa Naomi akaingia akiwa ameongozana na balozi wa mtaa mzee Msuya pamoja na wazee wengine wawili.
            "Kijana nini kimetokea? Mbona mwenzio amekuja ameniletea malalamiko kwamba umekuwa ukimpiga ? Balozi mzee Msuya akamuuliza Sheddy ambaye akamtazama na kisha kwa dharau akauliza
            "wewe unaongea kama nani? Mambo yangu mimi na mke wangu yanakuhusu nini?
 Mzee Msuya akaangaliana na wale wazee wenzake kisha akamgeukia Sheddy na kusema
            "Sikiliza kijana.Mimi ni balozi wa mtaa huu .Ninamfahamu Naomi toka alipohamia hapa mtaani.Ni mwanamke anayejiheshimu sana na sikutegema kama siku moja ungeweza kumfanyia kitendo kama hiki cha kumpiga.Nimekuja hapa kusikiliza sababu iliyopelekea wewe kumpiga mkeo na kumuumiza mkono namna hii kabla sijamruhusu aende mbele zaidi kwa hatua stahiki dhidi yako."
            "Balozi mimi nakushangaa sana mtu mzima kama wewe kuanza kuingilia ugomzi wa vijana .Naomba jamani muondoke humu ndani na mniache mimi na mke wangu tuyamalize mambo yetu sisi wenyewe.Naomba mkaendelee na kazi zenu" Akasema Sheddy.
            “Kijana naomba uwe na adabu kwa wazee wako.Usiongee kama vile unaongea na wahuni wenzako huko mitaani.Nina uwezo wa kukuchukulia hatua sasa hivi" akafoka mzee Msuya
            "Unichukulie hatua kwa kosa lipi wewe mzee? Ugomvi haukuhusu wewe unaingilia Mimi nimekwaruzana na mke wangu wewe yanakuhusu nini?..." Akasema Sheddy kwa ukali .
            "Kijana nakuomba uwe na adabu tafadhali.Msikilize balozi wako anataka kusema nini" akasema mzee mmoja kati ya wale wawili waliokuwa wameongozana na balozi Msuya
            "Balozi mimi sitaki malumbano zaidi na huyu mtu.Ninachokisema ni kwamba nimechoka naye na simuhitaji tena hapa kwangu.Ninachotaka yeye achukue begi lake na aondoke zake sitaki tena kumuona hapa ndani kwangu." Naomi akasema kwa ukali akiwa amesimama nyuma ya balozi.
            " Kijana umesikia mwenzako anavyosema ? Amekuchoka na hataki tena kukuona ndani kwake." Akasema balozi Msuya
            "Hapa si kwake.Hapa ni kwangu mimi na hana nguvu yoyote ya kunitoa humu.Kama  ni kuondoka aondoke yeye" akasema Sheddy .Mzee Msuya aamwangalia kwa makini na kusema
            "Kwanza mimi sikufahamu kabisa katika orodha ya watu wangu wa mtaa huu. Ninayemfahamu ni Naomi pekee.Wewe si mtu wa mtaa huu.Nakuomba kijana usiendelee kufanya fujo hapa.Nitaita askari sasa hivi waje wakuchukue na kukuweka ndani." akasema balozi Msuya.
            'Niwekwe ndani kwa kosa lipi? Kugombana na mke wangu nikawekwe ndani? akauliza Sheddy kwa ukali
            "Huyu kijana anaonekana hanifahamu vizuri" Mzee Msuya akasema na kuchukua simu yake akazitafuta namba fulani na kupiga.
            "Halo Afande Sadiki.Habari yako ndugu yangu" akasema mzee Msuya
            "Afande ninaomba msaada wako wa haraka.Kuna kijana mmoja amevamia chumba cha msichana mmoja hapa mtaani kwangu na analeta fujo,amempiga na hataki kutoka .Naomba unitumie vijana wawili ili waweze kutusaidia kumtoa kijana huyu" akasema mzee Msuya akatulia kusikiliza upande wa pili wa simu na kisha akasema
            "Nashukuru sana afande.Waelekeze wafike pale nyumbani kwangu "  akamaliza kuongea na simu na kuikata kisha akamgeukia Sheddy
            " Nilikuwa naongea na mkuu wa kituo .Anawatuma askari wawili sasa hivi ili wakuchukue wakakuweke ndani " akasema mzee Msuya.
            "Lakini huu ni uonevu jamani.Kwa nini lakini mnafanya namna hii? Kwa nini mnavunja ndoa yangu? akalalamika Sheddy.Naomi aaonyesha kukerwa na kauli ile ya Sheddy
            "Ndoa ! Umemuoa nani hapa? Nimesema chukua begi lako na uondoke sitaki kukuona tena  ndani kwangu." Akasema Naomi huku akilichukua begi dogo la kijani na kuanza kupakia nguo za Sheddy.Sheddy ambaye alikuwa amekaa kitandani akiwa amevaa nguo ya ndani pekee akainuka na kuvaa suruali yake na shati  halafu akavaa viatu vyake vya kuchomeka.
            "Begi lako hili hapa.Naomba uondoke na sitaki tena kukuona hapa kwangu" Naomi akasema akiliweka begi mezani.
            "Kweli Naomi unadiriki kunifukuza? Sheddy akamuuliza Naomi huku akimuangalia kwa jicho kali.
            "Sheddy jaribu kuwa mwelewa.Mwenzako amekwisha kuambia kwamba ondoka nyumbani kwake na ndiyo sababu ya kuita uongozi wa mtaa kama  mashahidi.Unapoendela kumghasi ghasi kwa maswali unafikiri atabadili mawazo yake? Chukua mizgo yako na uondoke umuache mwenzio aishi mwenyewe kwa amani" Genes akasema
            " Tulia wewe mtoto  wa kiume mwenye kimbele mbele kama mwnamke.Mambo hayakuhusu unayaingilia kama nini sijui" akafoka Sheddy.Kauli ile ikamkasirisha sana Genes akaliinua begi dogo la Sheddy akalirusha nje na kisha akaanza kumsukuma Sheddy kutoka mle ndani.
            "Wewe mwanaume gani unayeishi kama ndege? Huna makao maalum.Kumbe kiburi chote hiki hata shuka la kujifunika huna? Ondoka  ndani mwa watu muache mtoto wa watu apumzike.Amechoka kukulea baba mzima kama wewe" Akasema kwa kejeli Genes.Sheddy akarusha ngumi kwa dhumuni la kutaka kumpiga Genes usoni lakini Genes akawahi kuidaka.
            "Sitaki kupigana na wewe Sheddy.Sitaki kuharibu siku yangu bure.Nakuomba uondoke kwa amani kabla polisi hawajafika hapa" akasema Genes
            " Nakwambia hivi ,tutaonana mtaani..Lazima nikutafute nkuonyeshe kwamba sisi ndio wenye mji huu.Nitakufanyia kitu kibaya sana.na wewe Naomi ninakuambia utanitambua mimi ni nani.lazima nikuonyeshe kazi malaya mkubwa wewe." akatamba Sheddy
            "Kijana tafadhali usiendelee kutukana watu hapa.Umekwisha pewa mizigo yako ondoka kwa amani.Naomi hakuna kitu kingine amekisahau huyu kijana ili kesho asirudi tena hapa? akauliza mzee Msuya
            "Hapana mzee Msuya.Kila kitu chake nimemuwekea humo katika begi lake."akajibu Naomi
            " haya kijana safari njema" Mzee Msuya akasema.Sheddy akageuka na kumtazama kwa macho makali
            "na wewe mzee lazima nikushikishe adabu.We si ndiyo kinara wa kuvunja nyumba za watu basi nitakuonyesha kwamba mimi ndo mtoto wa mjni haswaa....subiri mziki wangu unakuja" akasema Sheddy huku akiliinua begi lake na kulivaa mgongoni akaanza kupiga hatua kuondoka huku akitukana.
            "Haya mama sasa uko salama .Jitahidi huyu kijana asije akarudi tena hapa.Hafai kabisa .Kijana ana dharau sana”
akasema mzee Msuya
            "Samahani sana mzee Msuya kwa dharau alizozionyesha kwako.Yule ndivyo alivyo ana dharau nyingi sana." Akasema Naomi kwa adabu.
            "Usijali Naomi .Ila ninakuonya kama mwanangu tulia na utapata mwanaume mwenye tabia njema,mwanaume anayekujali na mwenye heshima kwako,kwa kila mtu na anayejiheshimu yeye mwenyewe,si kama huyu kijana sijui ulimtoa wapi."
            "Nashukuru sana mzee Msuya kwa kunisaidia kumuondoa huyu kijana hapa kwangu endapo ningekuwa mimi peke nisingeweza kumtoa hapa kwa sababu alikwisha kataa kutoka kabisa.Kwa mambo niliyoyapata wakati nikiwa na kijana huyu sintafanya makosa tena ya kurukia rukia wanaume wasiokuwa na mbele wala nyuma.Nimejifunza mengi na safari hii nitakuwa makini sana na hawa vijana wasiokuwa na mwelekeo " akasema Naomi
            "Mimi nakushauri pia uende polisi ukatoe maelezo ili wawe na kumbu kumbu kwa sababu wote tumesikia akikutishia maisha yako.Iwapo utapatwa na jambo lolote lile basi tutajua ni yeye ndiye anayehusika." Genes akasema
            " Hilo ni wazo zuri sana umelitoa.Yule kijana anaweza kweli akamdhuru mwenzake.Si mwema kabisa yule kijana.Usipuuze alichokisema nenda polisi ukatoe maelezo na watakuwa na kumbu kumbu ili kama kuna jambo lolote baya litakutokea basi tujue ni yeye ndiye mhusika mkuu." Akashauri mzee Msuya
            "Nashukuru sana Genes kwa kunisaidia.Samahani sana kwa kukupotezea wakati wako" akasema Naomi
            "Usijali Naomi ,iwapo akirudi tena na kuanza kukuletea fujo usisite kuniambia ili nimpeleke mimi mwenyewe polisi.Mjinga yule amesababaisha hadi nimechelewa ibada" akasema Genes
            "ouh samahani sana Genes." akasema Naomi
            "Usijali Naomi.Nitasali hata ibada ya kwenye Televisheni" akasema Genes na kuwafanya watu wote waangue kicheko.
            "Msicheke.Ni kweli nitasali ibada ile itakayo onyeshwa katika luninga." Genes akasema  huku akielekea ndani mwake.Akajitupa kitandani na kuanza kukumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea.Picha ya Naomi akiwa amevaa nguo ya ndani ndogo nyeupe pamoja na sidiria nyeupe iliyoyafanya matiti yake madogo kusimama ilimjia usoji na kumfanya akishike kichwa chake kwa mikono yake miwili.
            "Sikutegema kama siku moja ningekuja kumuona Naomi akiwa katika hali ile.Naomi ni mwanamke mrembo na anayejiheshimu sana .Toka amehamia katika nyumba hii nimekuwa nikitafuta nafasi ya kujaribu kuwa naye karibu lakini nimeshindwa.Leo kama bahati nafanikiwa kumuona akiwa mtupu namna ile.Nilipomuona mwiloi mzima ukanisisimka .Lazima nikiri kwamba Naomi ni msichana mzuri.Namsifu mwenyezi Mungu kwa uumbaji wake uliotukuka kwani pale alitulia na akatuumbia pambo la dunia.Sijui kwa nini mtoto kama yule hajashiriki mashindano ya urembo.Nina imani angeweza kushika nafasi za juu sana kama angeshiriki kwa sababu ana vigezo vyote vya kumuwezesha kuwa mrembo maarufu..Sjui yule muhuni alimpa nini Naomi hadi akashawishika kuishi naye.Kweli mapenzi ni sawa na upofu kwa sababu Naomi hakuwa saizi ya yule mlevi Sheddy.Naomi anatakiwa awe na mwanaume mwenye kujua nini thamani ya mwanamke.Mwanaume mwenye kujua kupenda." akawaza Genes kisha akainuka pale kitandani na kukumbuka kwamba alikuwa amezima redio wakati akienda kuamua ugomvi.akaiwasha redio yake akaketi sofani na  kuendelea kuwaza.
            "Sura ya Naomi bado inanijia akilini kila sekunde.Siwezi kuacha kumuwaza mtoto mzuri kama Naomi.Nadhani hii ni nafasi ambayo natakiwa kuitumia ili kuwa karibu na Naomi.Lazima niitumie nafasi hii kikamilifu ili niweze kumpata msichana yule mwenye uzuri wa kipekee kabisa.Nitaanza kwanza kwa kujenga mazoea naye ya ukaribu na hasa katika kipindi hiki ambacho ameachana na jamaa yake anahitaji kuwa na mtu wa kuweza kumliwaza na kumfanya asahau yale yote yaliyopita.Hii ni nafasi yangu .Sitakiwi kufanya makosa .Lazima nifanye kila aina ya jitihada ili niweze kumpata  Naomi.Siku nyingi nimekuwa nikimuwaza lakini nilimuheshimu kwa kuwa alikuwa akiishi na bwana wake.Kwa sasa yuko huru na sitaki tena kuipoteza nafasi hii adimu." akawaza  Genes.Akawasha pasi na kuendelea kunyoosha nguo zake.Kazi ya kunyoosha nguo ilikuwa ngumu sana kwani kila mara sura ya Naomi ikawa inamjia kichwani na kumfanya aache kunyoosha na kukaa akiwaza.
 
                                                           
*           *           *           *

            Sauti ya mlango kugongwa ndiyo iliyomstua Genes toka usingizini.Alikuwa amelala toka saa kumi za jioni.Taratibu akainuka na kwenda kuufungua mlango.Mlangoni alikuwa amesimama msichana mwenye uzuri wa shani Naomi akiwa na tabasamu lenye aibu  kwa mbali.Genes akapatwa na mstuko kidogo kwa jinsi Naomi alivyokuwa amependeza.Alikuwa akiushangaa uzuri wa Naomi jioni hii .Kwa namna alivyokuwa akimuangalia ni kana kwamba ilikuwa ni mara ya kwanza kumuona.Naomi pia aligundua kwamba Genes alikuwa akimuangalia akaona aibu na kutazama chini.
            "Naomi karibu sana" akasema Genes baada ya Naomi kuanza kuangalia chini alipogundua kwamba Genes alikuwa akimuangalia
            "Genes samahani kwa kukusumbua.Sikujua kama ulikuwa umelala" akasema Naomi.
            "Usijali Naomi.Nilikuwa nimejipumzisha si unajua tena inatubidi kujiandaa kwa ajili ya kesho kazini" akasema Genes huku akitabasamu
            " Karibu ndani Naomi" akasema Genes na kuufungua mlango zaidi ili Naomi apite.Jioni hii Naomi alikuwa amependeza vilivyo ndani ya mavazi meupe.Huku akiona aibu Naomi akaingia chumbani kwa Genes.Mkononi alikuwa ameshika mfuko mweusi wa nailoni.
            "Karibu kiti Naomi" Genes akamkaribisha Naomi kiti.
            "Ahsante sana Genes" akajibu Naomi na kuketi sofani.Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Naomi kuingia chumbani kwa Genes.
            "Naomi unatumia kinywaji gani? akauliza genes akiwa ameushika mlango wa friji.
            "Nashukuru sana Genes ,naomba usisumbuke kwani nimetoka kunywa soda muda si mrefu" akajibu Naomi
            "Ni mara ya kwanza kuingia kwangu nakuomba uniachie walau baraka kidogo kwa kunywa walau glasi moja ya soda." Genes akasisitiza.Naomi kwa aibu akakubali
            " Habari za Jumapili? Genes akaanzisha maongezi baada ya kumpatia Naomi kinywaji
            "Habari nzuri Genes.Sijui wewe umeshindaje?
            "Mimi nimeshinda salama.Kutwa nzima ya leo nilikuwa nimepumzika ndani" akasema Genes kisha akapiga funda moja la kinywaji kilichokuwa katika glasi yake.
            "Genes nimekuja kukushukuru kwa msaada wako ulionisaidia wa kuweza kumtoa yule jamaa ndani kwangu.Nilikwisha jaribu kutaka kumuondoa lakini nikashindwa kwa sababu kila nilipojaribu kumwambia simuhitaji tena alinitishia kuniua ikanibidi kukaa kimya.Vile vile samahani sana kwa matusi yote aliyokuwa amekutukana." Naomi akasema huku akiangalia chini .Uso wa Genes ukajenga tabasamu pana sana.
            "Usijali Naomi.Ni mambo ya kawaida kutokea na wala wewe si wa kwanza kukorofishana na mumeo." Akasema Genes na kumfanya Naomi atabasamu akainua kichwa na kusema
            "Yule hakuwa mume .Ni mtu niliamua kuishi naye lakini hatukuwa na mipango yoyote ya mbeleni kwamba tuoane na kuwa mke na mume" Naomi akasema
            " Sikufurahishwa na kitendo alichokifanya cha kukupiga ndiyo maana nilipandwa na hasira nikataka kupigana naye." Genes akasema huku akicheka kichini chini
            "Du ! pole sana Genes.Ulifanya kazi kubwa sana ya kumuondoa yule jamaa kwangu.Bila ya wewe sijui ingekuwaje leo.Nahisi pengine angeniulia ndani" Naomi akasema
            "Kwa sasa jitahidi kutokuwa na mawasiliano naye ya namna yoyote ile .Jitahidi kuishi mwenyewe na kuyatengeneza maisha yako.NI wakati wako wa kujijenga" akasema Genes
            "Kweli kabisa Genes.Natakiwa niitumia nafasi hii kujitenegenezea msingi mzuri wa maisha" akasema Naomi na kuimalizia soda iliyokuwamo katika glasi lake
            "Genes mimi si mkaaji sana .Nina kazi za kufanya usiku huu ambazo kesho natakiwa niziwahishe kazini.Kuna mzigo huu kidogo nimekuletea." Akasema Naomi huku akiinuka pale sofani.
            "Nashukuru sana Naomi.Siku yoyote muda wowote ukihitaji msaada wa namna yoyote usisite kuniambia.Au kama akirudi yule jamaa na kuanza kukuletea fujo usiogope kunitaarifu.Nitamkamata na kumpeleka polisi mimi mwenyewe.Si katika shida tu,hata siku ukijisikia mpweke na unahitaji mtu wa kuongea naye na kubadilishana mawazo mimi niko hapa,usisite kunigongea mlango au hata kunipigia simu.Naomba unipatie namba yako ya simu kwani sikuwa na namba yako katika simu yangu.Si vibaya mara moja " Genes akasema na kisha wakabadilishana namba na  Naomi akaondoka.
            Baada ya Naomi kuondoka Genes akaufunga mlango na kusimama kwa sekunde kadhaa akiwa amekishika kiuno chake na uso wake umejengeka kwa tabasamu pana sana.Akaiendea soda aliyokuwa amebakiza Naomi katika chupa akaibusu na kuinywa.
            "Nahisi ni kama vile niko ndotoni.Naomi leo ameingia chumbani kwangu !! .Hii ni dalili njema sana.Huu ni mwanzo mzuri sana" akawaza Genes.
            "Humu kwenye huu mfuko kuna nini? akasema taratibu Genes huku akiufungua mfuko ule na kukuta kuna nyama ya kuku ya kukaanga.
            "Wow ! ...Naomi... I love you so much.Nakupenda sana Naomi..Laiti ungejua ni namna gani moyo wangu unakuhitaji ungenionea huruma" Genes akasema taratibu akakibusu kigaja cha mkono wake na kukipuliza kuelekea chumba cha Naomi.

ENDELEA KUFUATILIA MFULULIZO WA SIMULIZI HII KILA SIKU HAPA MASIMULIZI

1 comment:

  1. Huu ni lazima ushuhudia usomaji na kila mtu, nipo hapa kuruhusu ulimwengu wote kujua kuhusu mtu aliyeokoa uhusiano wangu na mtu huyu mkuu anaitwa Dr IZOYA. Hakika alifanya kazi nzuri kwangu kwa kumrudisha mpenzi wangu wa zamani ambaye aliniacha na kuahidi kamwe kurudi kwangu tena. Kwa hili, nimekuja kutambua kuwa kutoa maelezo ya Dk IZOYA kwa ulimwengu utafanya mengi mazuri kwa wale walio na nyumba zilizovunja au uhusiano kwa ajili yake ili kukusaidia kurekebisha uhusiano huo uliovunjika au ndoa yako. Unaweza kumfikia kupitia anwani yake ya barua pepe: drizayaomosolution@gmail.com au kumwita moja kwa moja kwenye [+12098373537]. Kuwasiliana naye na kuona jinsi tatizo lako litatatuliwa ndani ya 24hours. Pia mtaalamu katika mambo yafuatayo ...
    (1) Unataka kurudi nyuma yako.
    (2) Unataka kukuzwa katika ofisi yako.
    (3) Unataka wanaume / wanawake kukufuate.
    (4) Unataka mtoto.
    (5) Wewe ni mjasiriamali na unataka kushinda mikataba
    (6) Unataka mume wako awe wako milele
    (7) Unahitaji msaada wa kiroho.
    (8) Umeshambuliwa na unataka kupona fedha zilizopotea.
    (9) Weka talaka
    (10) Kualika kwa mila ya fedha
    (11) Chagua uchaguzi

    ReplyDelete

Followers

 

BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU

Powered By masimulizi