Ndege iliyombeba mzee Albano sostenes
mwakatala ilipunguza kasi taratibu na hatimaye ikasimama.Tayari gari la
wagonjwa lilikwisha fika na wauguzi na madaktari walikuwepo tayari kuhakikisha
mzee Albano anapatiwa kila huduma inayohitajika wakati akishushwa toka ndegeni
na kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi
.Kiongozi wa msafara ule wa madaktari na wauguzi toka hospitali kuu ya Patrick memorial hospital Dr.Henry Mgumbwa alikuwa pembeni akibadilishana hili na lile na madaktari wenzake.
.Kiongozi wa msafara ule wa madaktari na wauguzi toka hospitali kuu ya Patrick memorial hospital Dr.Henry Mgumbwa alikuwa pembeni akibadilishana hili na lile na madaktari wenzake.
Kutoka serikalini alikuwepo mheshimiwa
waziri wa afya akiiwakilisha serikali ,pamoja na viongozi mbali mbali,vile vile
walikuwepo viongozi wa dini toka madhehebu mbali mbali, na viongozi wa kisiasa
pia walikuwepo.Ilimradi kila nyanja ambayo iliguswa na taarifa za kurejeshwa
nchini mzee Albano ilituma mwakilishi wake.
Familia ya mzee Albano ilishuka ndegeni
ikiongozwa na mke wake na binti zake wawili Serena na Isabella wakiambatana na
mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini mzee Bryson Kamutere ambaye ni mshirika
mkubwa wa kibiashara wa Albano Mwakatala aliyeambatana nao India ,wakasalimiana
na kufarijiwa na ndugu na viongozi kadhaa wa serikali waliokuwa pale uwanjani
pamoja na viongozi wa dini.Ilikuwa ni hali ya simanzi kubwa.Huko nje ya uwanja
kulikuwa na umati mkubwa wa watu na
magari ambao wote walionyesha jinsi gani mzee Albano alivyokuwa mtu wao wa
muhimu.
Taratibu zote zikakamilika hapo
uwanjani kisha mzee Albano huku akiwa hana
fahamu ,akapakiwa katika gari la
wagonjwa na safari ya kuelekea hospitali ikaanza.
Taarifa za kurejeshwa nchini Mzee
Albano Mwakatala zilisambaa karibu kila kona ya nchi.Magazeti yaliandika kwa
kirefu juu ya kushindikana kupona huko nchini India na kisha madaktari bingwa
kushauri arejeshwe nyumbani ,kwa sababu hakukuwa tena na tumaini la kupona,kilichosubiriwa ni siku ya kufariki
kwake.Madaktari katika hospitali kubwa nchini India walijitahidi kwa muda wa
zaidi ya mwezi mmoja katika kujaribu kuutibu ugonjwa wa mzee Albano bila
mafanikio.
Mzee Albano alikuwa ni mmoja kati ya
watu wenye heshima kubwa sana nchini Tanzania.Alikuwa mmoja kati ya wawekezaji
wakubwa wazawa,aliyewekeza katika viwanda vya kusindika mazao ya kilimo karibu
kila mkoa na siku zote alikuwa akijitahidi na kuipigia kelele sana serikali juu
ya kuongeza ajira kwa wazawa.Hii ilimfanya ajulikane na kupendwa .Pamoja na
kuwa mmoja kati wa wawekezaji wakubwa nchini,ambaye alichangia kupatikana kwa
ajira lukuki kupitia kampuni zake,alikuwa pia ni kimbilio kubwa kwa wale watu
masikini wenye matatizo mbali mbali.Karibu kila mwezi alikuwa akilipia gharama
za operesheni kubwa kubwa za watu mbali mbali wasiokuwa na uwezo,ndani na nje
ya nchi achilia mbali kulipia gharama za elimu kwa watoto ambao wazazi wao
hawakuwa na uwezo wa kuwasomesha,vile vile aliweza kuvisaidia vikundi vingi vya
akina mama na vijana katika kujikwamua kimaisha.Ni mzee aliyekuwa na heshima ya
pekee katika jamii ya watanzania.
Albano Sostenes mwakatala ,ambaye baba
yake alikuwa na asili ya Ureno alizaliwa mkoani Mbeya wakati huo baba yake akiwa
mwekezaji mkubwa katika kilimo cha mpunga mkoani humo.Baba yake alioa mwanamke
mweusi kutoka mkoani mbeya na wakafanikiwa kupata mtoto mmoja tu ambaye ndiye
yeye mzee Albano.Alikulia mkoani Mbeya hadi alipomaliza elimu ya sekondari na
kujiunga na chuo kikuu cha Kilimo ambako alihitimu shahada ya kilimo.Akaenda
tena kuendelea na masomo nchini Japan katika kilimo cha Mpunga kwani alitaka
kuendeleza kazi aliyokuwa akiifanya baba yake.Ni wakati huo ndipo alipopatwa na
pigo kubwa la kuondokewa na wazazi wake wote wawili waliofariki kwa ajali ya
gari.Alirudi nchini baada ya kumaliza masomo yake nchini Japan ,akaendeleza
miradi ya kilimo aliyoiacha baba yake kwa ufanisi mkubwa. Ndani ya miaka miwili
alikuwa amepiga hatua kubwa na kuongeza mtaji mara dufu ya ule wa baba yake.Hii
ikamfanya ajikite tena zaidi katika uwekezaji mwingine.Akafungua viwanda karibu
kila mkoa ili kuyaongezea thamani mazao ya wakulima.Akawa tegemeo kubwa la
mazao ya wakulima nchini.Biashara yake ikawa kubwa sana na sasa akawa mmoja
kati ya wawekezaji wakubwa na hapo ndipo alipoamua kuhamia mkoani Dar es salaam
kwa sababu za kibiashara.
Alioa mke wake aliyekuwa mzaliwa wa Mbeya ambaye walikutana masomoni
nchini Japan.wakafanikiwa kupata watoto wawili wa kike wenye uzuri usioelezeka Serena
na Isabella.
Siku moja akiwa katika safari zake za
kibiashara alivamiwa na kundi la watu watu wenye silaha wanaosadikiwa kuwa ni
majambazi ambao walimshambulia wakiwa na lengo la kumuua lakini kwa msaada
mkubwa wa walinzi wake majambazi wale hawakufanikiwa kumuua badala yake
walifanikiwa kumpiga na na kitu kizito kichwani na kumuacha akiwa hana fahamu.Tukio
lile lilipelekea umoja wa wafanyabiashara kucuhukua maamuzi ya kumpeleka mzee
Albano nje ya nchi kwa matibabu ya
haraka.Akiwa nchini India alikopelekwa kwa matibabu alifanyiwa uchunguzi na jopo la madaktari
bingwa wakijaribu kutafuta namna ambayo
wangeweza kufanya upasuaji .Hatimaye waliita familia yake na kuieleza ukweli
kuwa operesheni hiyo ilikuwa ni haitawezekana kwa mzee Albano kufanyiwa
upasuaji wa kichwa kwa sababu hakukuwa na tumaini la kupona hata kama
angefanyiwa upasuaji huo.Taarifa hii ilikuwa ya mstuko mkubwa sana kwa familia
yam zee Albano.Suala la kufariki baba yao lilikuwa ni msamiati mgumu kwa
familia hii,hivyo wakataka kumuhamishia nchini Marekani katika hospitali kubwa
zaidi,lakini mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini mzee Bryson kamutere
ambaye ni rafiki mkubwa wa Albano aliyeambatana na familia ya Albano nchini
India akawashauri kwamba wazingatie ushauri wa madaktari wale bingwa na kurejea
nyumbani kwani hata wangekwenda wapi hakukuwa tena na tumaini la mzee Albano
kupona.Hatimaye baada ya majadilino marefu mke wa mzee Albano alikubali
kumrejesha mumewe nchini kama alivyoshauriwa na madaktari.
Kwa muda wa
wiki nzima vyombo vya habari viliandika kwa
wingi taarifa za mzee Albano.SIKU ZA
ALBANO ZINAHESABIKA,KABURI LA ALBANO LAANDALIWA,TAIFA LAJIANDAA KUOMBOLEZA,hivi
ni baadhi tu ya vichwa vya habari vilivyokuwa vikipamba magazeti ya kila
siku,hali iliyoamsha wasi wasi mkubwa miongoni mwa wale waliomfahamu na
kumpenda mzee Albano.
H atimaye siku ya kurudishwa
nyumbani mzee Albano ikawadia.Siku
iliyokuwa na majonzi tele.Watu waliokuwa hapo uwanjani ni kama vile walikuwa
msibani.Maongezi yalikuwa ni ya chini chini kila mmoja akionyesha huzuni
aliyonayo.Pamoja na kuwa ni siku ya kazi lakini huwezi amini umati wa watu
uliokusanyika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.
Patrick Charles memorial hospital ni
moja kati ya hospitali kubwa kuwahi kujengwa nchini Tanzania.Ilikuwa ni
hospitali ya aina yake kwa kuwa ilikuwa na uwezo wa kutibu karibu kila
ugonjwa.Hospitali hii ilijengwa mahususi kwa ajili ya kumbukumbu ya Dr Patrick Charles
mmoja kati ya madaktari waliojitolea maisha yao katika kuwasaidia watu masikini.Katika
kuuenzi mchango wa baba yake ,Patrick Jr akaamua kujenga hospitali hii kubwa na
ya aina yake ili kutoa matibabu kwa watu wote na hasa yale magonjwa makubwa
yaliyoshindikana katika hospitali nyingine zote hivyo kupunguza gharama za
kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya upasuaji na matibabu.Hospitali hii
iliyosheheni mabingwa wa kila fani ilihudumia si tu Tanzania bali hata nchi
zote zinazoizunguka.
Eneo lote la kuegesha magari katika hospitali hii kubwa lilijaa
magari kwa mara ya kwanza toka hospitali hii imefunguliwa.Watu wote hawa
walikuwa wamekuja kuonyesha mshikamano wao kwa mzee Albano na kumtakia afya
njema.Gari la wagonjwa lililombeba Mzee Albano likaingia hospitalini
hapo,likaingizwa mpaka ndani kabisa na mzee albano akiwa bado hajitambui
akapokelewa na kupelekwa katika chumba maalumu kwa ajili ya kupatiwa uangalizi
.
Kila kitu kilifanyika kwa haraka na kwa
umakini wa aina yake.Dr Henry alikuwa bega kwa bega na madaktari wake
kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.Baada ya kuhakikisha
kila kitu kiko safi na tayari Mzee Albano anaendelea kupatiwa matibabu
akaelekea ofisini kwake.Akabonyeza namba kadhaa katika simu yake ya mezani
“Hallow Dr Henry hapa toka Patrick Charles
memorial hospital,Naomba kuongea na Dr Jason tafadhali” Akasema Dr Henry
“ Dr jason hawezi kuongea nawe muda
huu yuko katika upasuaji.Baada ya kama dakika kumi hivi atakuwa amemaliza”
“Ok akimaliza upasuaji tafadhali naomba anipigie
ni muhimu mno”
Dr Henry akakata
simu kisha akapiga simu mapokezi na kuomba mke wa Mzee Albano na wanae waweze
kupandisha ofisini kwake.
“Karibuni sana .” Akasema Dr Henry
baada ya mke wa mzee Albano na wanae kuwasili ofisini
“Kwanza napenda kuwapa pole nyingi sana kwa
kazi kubwa mliyoifanya ya kumuuguza mzee wetu mpaka katika hatua hii aliyofikia
.Mama na wanao mnastahili pongezi kwa ujasiri mkubwa mliouonyesha.Papo hapo
bado tunazidi kuwaomba mzidi kuwa wavumilivu kwa sababu hali ya mzee wetu bado
si nzuri sana kama wenyewe mnavyoona na kwa mujibu wa taarifa za kidaktari.Sisi
hapa tunaahidi kufanya kila tunaloweza ili kumpa tiba inayostahili mzee wetu
mpaka hapo baadae kwani tumepokea taarifa toka kwa mheshimiwa rais kwamba
tufanye kila linalowezekana kumsaidia mzee Albano. Tunaye Daktari wetu bingwa wa
mambo ya mishipa ya fahamu ya ubongo na uti wa mgongo,kwa sasa yuko Dodoma
kikazi ,nimempigia simu sasa hivi lakini bado yuko katika upasuaji hivyo muda wowote
atapiga simu atakapomaliza .Nataka naye arudi mara moja leo hii hii ili aongoze
jopo la madaktari katika kumpa tiba mzee wetu.Ninamuamini Dr Jason ni daktari
wa ian yake hapa nchini na nina hakika baada ya kumuona na kumfanyia uchunguzi
mzee wetu basi anaweza akatupa uhakika kama atapona au hatapoa.Kwa sasa msiwe
na wasi wasi sana kwani hata kama huko Nje ya nchi wameshindwa sisi hatuwezi
kukata tamaa kirahisi kwani si mara moja kuna watu wameshindikana kupona huko
nje ya nchi lakini wamekuja kupona hapa.…….”kabla hajaendelea simu ikaita
akaipokea
“Hallow,Dr Henry hapa”
“Dr Henry Ni mimi Jason.Nimepata
ujumbe wako.”
“Ndiyo Dr Jason nimekupigia nikakuta
uko katika upasuaji .Dr Jason nakuomba uache shughuli zote hapo Dodoma na
urejee mara moja hapa Dar es salaam. Leo Mzee Albano amerudishwa kutoka India
hivyo Serikali ikatukabidhi sisi jukumu la kuhakikisha tunampatia huduma zote
muhimu za kitabibu.Hapa tunapoongea niko na familia yake.Ninachoomba ni kwamba
itatumwa ndege yetu leo saa kumi na mbili jioni ije ikuchukue ili uongoze jopo
la madaktari katika matibabu ya mzee Albano”
“Ok ! Dr Henry hakuna tatizo.Nitakuwa
tayari muda huo ndege itakapofika” akasema Dr Jason
“ Ok ! Dr Jason.See you then.Bye”
Akakata simu na kuendelea na maongezi na familia ya mzee Albano.
********************************
Saa kumi na mbili za jioni ndege
ndogo inayomilikiwa na hospitali ya
Patrick Charles memorial ilitua katika uwanja mdogo wa hospitali hiyo
uliopo pembezoni mwa majengo ya hospitali.Ni ndege iliyomleta Dr Jason bingwa
wa neva za fahamu za ubongo na uti wa mgongo.Ni mmoja kati ya madaktari bingwa
wachache sana wenye uwezo wa kipekee kabisa katika fani hii kwa ukanda huu wa
Afrika.
Dr Jason akapokelewa na Daktari mkuu Dr
Henry kisha kwa mwendo wa kasi wakaanza kuelekea hospitalini.
“Mgonjwa anaendeleaje? Akauliza Dr
Jason
“mgonjwa hali yake bado si nzuri.Mpaka
sasa hivi bado hajarejewa na fahamu” Akasema Dr Henry
Moja kwa moja wakaelekea katika
chumba cha wagonjwa mahututi alimolazwa Mzee Albano. Alipoingia Dr Jason mle
ndani ya chumba cha mgonjwa kila mmoja aliyekuwemo alionyesha tabasamu la
matumaini usoni.Hii ilionyesha ni jinsi gani walivyokuwa na imani na Dr
Jason.Kwa haraka akapewa taarifa ya maendeleo ya mgonjwa,akaomba apewe na faili
la mzee Albano,kisha akaelekea ofisini kwake.
Ni saa tatu za usiku sasa,masaa matatu yameshapita
tangu Dr Jason alipoanza kulipitia faili la Mzee Albano.Alilipitia kwa umakini
mkubwa sana na alilirudia mara ya pili
na ya tatu.aliporidhika akainua simu na kumpigia Dr Henry ambaye hakupoteza
muda akafika ofisini kwa Dr Jason.
“Dr Henry nimelipitia kwa makini faili
la mgonjwa, kuna hivi vipimo nimeviorodhesha hapa ninataka vichukuliwe mara
moja.Ni vipimo muhimu sana ambavyo vitatusaidia kuona jinsi ya kuanza kumsadia
mgonjwa”
Dr Henry akaichukua karatasi ile yenye
vipimo alivyoviorodhesha Dr Jason akaiangalia kisha akasema.
“Ok ! Dokta nafikiri timu nzima ya
vipimo ipo tayari,ngoja watuletee vipimo hivyo”akatoka na kumwacha Dr Jason
bado akiendelea kulipitia faili lile.
Saa moja baadae Dr Henry alirudi akiwa
na faili lenye vipimo vyote alivyovihitaji Dr Jason.
“Kila kitu kiko humu Dr Jason.Kama
kuna kitu kingine unahitaji niko ofisini”
Jason
akaliweka faili alilokuwa akilipitia pembeni kisha akaanza kulipitia lile faili
lenye vipimo alivyokuwa akivihitaji.Dakika zaidi ya arobaini alizitumia
kuyapitia majibu yale ya vipimo alivyovitaka.Akasimama na kuzunguka humo
chumbani huku akiangalia juu.Ni wazi kuna kitu kikubwa alichokuwa
akikifikiria.Mwishowe akaamua kumwita Dr Henry.
“Dr Henry nimepitia kwa umakini faili
la mgonjwa na baadae majibu ya vipimo tulivyovifanya ”
“yes Dr.” Akajibu Dr Henry kwa shauku
ya kutaka kujua nini alichoitiwa
“Dr Henry kuna kitu nimekigundua katika uchunguzi wangu
ambacho hawa wenzetu kule India walishindwa kukigundua.Pamoja na kwamba
mabingwa wenzangu huko India walisema haiwezekani kwa mgonjwa kufanyiwa
upasuaji lakini bado sijakubaliana nao kutokana na majibu ya vipimo
nilivyovitaka.Nina kila sababu ya kukwambia kuwa tunaweza kumfanyia mgonjwa
upasuaji na kuokoa maisha ya mgonjwa.”
Dr Henry alibaki mdomo wazi akiwa hana
la kuongea.Alimuamini Dr Jason kupita kiasi kwani ni mmoja kati ya madaktari
wenye uwezo na akili ya ajabu sana.Lakini kwa hili alionyesha mstuko wa
dhahiri.
“Najua umestuka sana Dr Henry baada ya
kusikia kwamba ninaweza kumfanyia mgonjwa upasuaji ambao huko India
wameshindwa.Siwewe tu ambaye anaweza kustushwa na jambo hili bali kila mtu
anaweza akastuka akisikia kauli yangu,lakini ukweli ni kwamba mgonjwa bado
anayo nafasi ya kuishi iwapo nitamfanyia upasuaji wa haraka.Nashindwa kuelewa
kwa nini hawa madaktari wa India walishindwa kuligundua hili na kusema kuwa
mzee huyu hawezi pona.Jambo hili linanipa wasi wasi mkubwa sana kama walifanya
uchunguzi wa kutosha” akasema Dr Jason
Saa nzima
ilitumika kwa Dr Jason kumwelezea na kumfafanulia Dr Henry juu ya kile
alichokigundua katika majibu ya vipimo na sababu ya kutaka upasuaji ule
ufanyike.Dr Henry bado hakuwa na uamuzi hivyo akaamuru kuitishwa kikao cha
dharura usiku huo cha madaktari pamoja na uongozi wa hospitali ili kuona kama
kuna ulazima wowote wa kufanya operesheni hiyo.
Haraka haraka ujumbe ukasambazwa kwa
timu yote ya madaktari na kwa muda wa dakika ishirini wote wakawa wamekusanyika katika chumba cha
mikutano.Mkutano huu ulichukua zaidi ya masaa manne ndipo wote waliporidhika
kuwa kweli kuna ulazima wa mzee Albano kufanyiwa upasuaji katika ubongo wake
baada ya kuhakikishiwa na Dr Jason kwamba iwapo angefanyiwa upasuaji kulikuwa
na uwezekano mkubwa wa kuyaokoa maisha yake..
Ilipata saa tisa za usiku wakati Dr
Henry alipompigia simu mke wa mzee Albano na kumtaka yeye na familia yake
wafike hospitali hapo asubuhi na mapema kuna jambo la muhimu wanataka kuelezwa.
*******************************
Ni
milio ya ndege wa aina mbali mbali walioruka katika miti na bustani nzuri za
maua zilizopo ndani ya jumba hili la kifahari ndizo zilizokuwa
zimetawala.Ukimya mkuu ulikuwemo ndani ya jumba hili.Katika ghorofa ya juu
kabisa kikao kizito kilikuwa kikiendelea . Mzee Bryson kamutere,mzee mwenye
utajiri wa kutisha nchini Tanzania
alikuwa ndiye mwenyekiti wa kikao hiki.Pembeni yake alikuwepo binti yake
,mbunge mwenye umri mdogo kuliko wote katika bunge la jamhuri ya muungano wa
Tanzania Stella kamutere,halafu wakawepo na watu wengine tisa wenye nyadhifa
mbali mbali serikalini na mashirika binafsi.Alikuwepo Kumzaya ( Wakili wa
kujitegemea na mfanyabiashara) , Ambakisye mwalukosa ( waziri wa kilimo ) ,Benard
kukoa (mfanyakazi benki kuu ) , Nestory kazima ( mfanyakazi wizara ya fedha ) ,
Ernest kobwa ( Naibu waziri wa fedha ) , Sospeter Aloswa ( waziri wa maliasili
) , Azim Patel ( mfanyabiashara ) , Godwin Masawe ( mfanyabiashara) , Jacob
simala ( mfanyakazi hazina) , Emmanuel Vincent ( afisa uwanja wa ndege) , Sixmund
kamita (kamishna wa madini)
“Ndugu
wajumbe wa kikao hiki,nawashukuruni sana kwa kuitikia wito huu wa dharura japo si wote mliohudhuria lakini mliopo
mnatosha sana kuendesha kikao hiki.”
Alifungua kikao Mr Kamutere.
“Jambo
tunaloenda kulizungumza ndugu zangu ni jambo zito.nafikiri wote mnazo taarifa
za kurejeshwa nchini Mzee Albano.Mpango wetu ulikwenda vizuri sana kule
India,madaktari katika hospitali ile aliyokuwa anatibiwa walifanya kama vile tulivyowataka wafanye .Nilikuapo
kule na niliongea nao wakanielewa na kukataa kumfanyia upasuaji mzee Albano na
kuifanya familia yake kuamini kwamba mzee wao hawezi kupona hata kama
akifanyiwa upasiaji.Haikuwa kazi ndogo kuwashawishi wale madaktari japokuwa
imetugharimu fedha nyingi sana.Kwa sasa dunia nzima inaelewa kuwa mzee Albano
hawezi kupona na hana siku nyingi za kuishi.Kwa muda wa wiki moja toka sasa
mzee Albano atakuwa amekwisha fariki na
hilo ndilo hasa lengo letu.
“ kwa nini
hukuacha afanyiwe upasuaji na afariki wakati akifanyiwa upasuaji huko
India? Hakuna ambaye angehisi chochote
kwani wagonjwa wengi tu hufariki wakati wakifanyiwa upasuaji” akauliza Sixmund kamita
“Hatukutaka afe kifo chenye
mashaka.Tunataka kila mtu afahamu kwamba Albano alifariki kwa ugonjwa.Kurudi
kwa Albano kusubiri kifo chake ni ushindi mkubwa kwani alikuwa mtu hatari sana kwetu .Hatakiwi
kabisa kuendelea kuvuta hewa hii safi.Pamoja na juhudi hizo za kuhakikisha
kwamba mzee Albano haponi limeibuka tatizo dogo.Kwa mujibu wa vyanzo vyetu
vya uhakika toka hospitali ya Patrick Charles
Memorial ambako Albano amelazwa baada ya kurudishwa toka India ni kwamba hivi
tunavyoongea ,madaktari na familia ya Mzee Albano wako katika kikao.Kuna
uwezekano mkubwa mzee Albano akaendelea kuwa hai kwa sababu kuna huyu daktari
bingwa wa neva za fahamu za ubongo na uti wa mgongo anaitwa Jason Charles ambaye
anataka kumfanyia upasuaji mzee Albano
na kuna uwezekano mkubwa kuwa
iwapo atafanyiwa upasuaji huu kuna uwezekano mkubwa sana Albano akapona.Daktari
huyu inasemekana ni mmoja kati ya madaktari wachache wa kutumainiwa katika masuala ya ubongo na uti
wa mgongo si hapa Tanzania tu bali ukanda wote wa afrika mashariki na
kati.Tunachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kuhakikisha hilo halitokei kwa gharama
zozote zile.Lazima tuhakikishe kwamba huyo daktari hafanikiwi kumfanyia
upasuaji Albano.Tukikubali upasuaji huo ukafanyika na Albano akapona,siwafichi
ndugu zangu lazima Albano atulipue kwani suala hili alikwisha liweka wazi ”Mzee
Bryson akatulia akavuta pumzi na kuwaangalia wajumbe ambao pamoja na kuwa
chumba walichokuwamo kuwa na kiyoyozi lakini bado nyuso zao zilionyesha kuvuja
jasho.
“Baba umesema Dr Jason Patrick Charles
ndiye anayetaka kufanya huu upasuaji?” Stella akauliza kwa msisitizo huku
akimtolea baba yake macho ya shauku
“Yes my dear.Ni huyu huyu mchumba wako
Dr Jason”
"
Unbeliavable !! akasema Stella.Hakuamini alichokisikia toka kwa baba yake.
" Jason ndiye anayemfanyia
upasuaji mzee Albano ! Ouh Mungu wangu lazima nimtaarifu aachane mara moja na
mpango huo..they are going to kill him.Siwezi kukubali katu jambo hilo litokee.I
love him so much " akawaza Stella.Hali yake ilibadilika ghafla baada ya
kulisikia jina la mchumba wake likitajwa katika kikao kile.Hakuwa na amani tena
**********************************
Dr jason
aliwasili hospitali asubuhi na moja kwa moja akaelekea katika chumba maalum
alicholazwa mzee Albano.Hali yake haikuwa na mabadiliko yoyote.Akatoka na
kuelekea ofisini kwake kabla ya kukutana
na familia ya mzee albano ili kuielezea kwa ufasaha juu ya uamuzi wake wa
kumfanyia operesheni baba yao.
Siku hii alionekana mwingi wa mawazo na
hakutaka kujishugulisha na kazi nyingine
yeyote licha ya kuwa mafaili kadhaa ya
wagonjwa hapo mezani kwake.Akili yake aliielekeza katika kitu kimoja tu,ugonjwa
wa mzee Albano.Akiwa bado katika mawazo mengi mara simu yake ikaita alikuwa ni Daktari mkuu Dr Henry.
“Dr Henry habari za asubuhi.’
“Nzuri Dr Jason.habari za toka jana?”
“Nzuri tu .Mimi tayari nimeshafika
ofisini ,nimetoka kumuangalia mgonjwa hali yake haina mabadiliko yoyote.”
“ Dr Jason nadhani ni wakati sasa wa kukutana
sasa na familia ya Mzee Albano pale katika chumba kidogo cha mikutano ili
tuongelee suala hili la mzee wao, nilipata taarifa kuwa walikwisha fika muda
mrefu sana na nikaelekeza wapelekwe kule ili tukaongee nao.”
“Ok ! Dr Henry nakuja sasa hivi”
Akajibu Dr Jason na kukata simu kisha akatoka na kuelekea katika chumba kidogo
cha mikutano.
Muda mchache baadae tayari alikwisha fika,akakinyonga kitasa
na kuingia ndani.Chumba kilikuwa na madaktari pamoja na familia yam zee
Albano.Ghafla Dr Jason akasimama.Alikiona kitu ambacho hakutegemea kukiona.
“Serenaa…!!!!!!. Akasema Dr Jason kwa mstuko mkubwa.
Kila mtu mle chumbani
akastuka na kubaki akishangaa.Serena ambaye alikuwa ameongozana na mama yake na
Isabella naye akabaki ameduwaa akishangaa.
“ Jason
..!!!!! ..akasema Serena kwa sauti
ndogo.Isabella mdogo wake aliyekuwa amekaa pembeni yake akageuka na kumtazama
dada yake kwa mshangao.
0 comments:
Post a Comment