MASIMULIZI
Monday, April 7, 2014
" BEFORE I DIE " SEHEMU YA 6
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Uncle wewe ni Padri au mchungaji ? “
“kwanini umeuliza hivyo? Inno akauliza huku akicheka kichini chini
Unaonekana tu. Hauonekani kama ni mtu aliyezoea kuchukua wanawake wanaojiuza.Unavyoonekana una wasi wasi sana.Ni mara yako ya kwanza kuchukua kahaba?”
Innocent akatabasamu na kucheka kidogo halafu akasema
“mimi si padre wala mchungaji kama unavyofikiri ,ila ni kweli kwamba sina mazoea ya kutoka na wanawake wanaofanya biashara ya kujiuza.Kusema ukweli ni mara yangu ya kwanza na imekuwa ni kama muujiza Fulani kwa sababu sijielewi mpaka sasa hivi
nimewezaje kufanya kitendo kama hiki.” Innocent akasema na kujishika kichwa
.
“Sasa uncle kama ulikuwa huna mpango na mimi umenileta huku kufanya nini? Si ungeniacha basi pale kijiweni manake leo nilikuwa na mteja wangu wa kiarabu alikuwa aje kunichukua saa sita usiku halafu yeye analipa kwa dola.Kama huna mpango na mimi tufanye basi fasta fasta halafu nijikatae nikacheki mpango mwingine. “ Marina akasema huku akikivua kinguo chake cha juu na kubaki kifua wazi.Innocent anapatwa na mstuko wa ghafla
kwa kuziona chuchu zile zilizosimama.
ENDELEA…………………………….
“Marina vaa nguo yako
halafu tuongee.” Innocent akasema kwa msisitizo huku mapigo ya moyo yakienda kwa kasi.
“Uncle mbona unaniwekea usiku? Au wewe si mzima? Kama vipi niambie niende zangu” marina akalalama.
“Si hivyo marina .naomba vaa kwanza nguo yako halafu tutaongea.” Innocent akasema huku akiinuka na kuiendea simu.Akapiga simu mapokezi na kuomba waletewe mvinyo .
“mambo si hayo bwana.Muda wote nimekwambia uniagizie kinywaji unajivuuuuuuta kama nini” marina akasema huku akivaa ile nguo yake.
Innocent akarudi na kuketi karibu na marina akamwangalia kwa sekunde kadhaa.
“Unaogopa nini? Kama kondom ninazo.Ukitaka bila ya kondom itabidi tubadili bei ” Marina akasema
“ Hapana Marina sina maana hiyo na wala siogopi.” Innocent akasema
“ Sasa kama huogopi mbona unaniangalia kama vile ninataka kukutoa roho? Mimi ni wako nitumie utakavyo kwa usiku wa leo.”Marina akasema
“Marina naomba unisikilize vizuri”
“Ndiyo nakusikiliza” Marina akasema huku akikaa sawa
‘nimekuleta hapa si kwa ajili ya kukutumia na kukulipa.Mimi si mtu wa namna hiyo.Nilikuona katika lango la kuingilia pale klabuni ,nikajikuta nikistuka ghafla
na kuguswa sana Nilijiuliza maswali mengi ni kwa nini uko pale na genge lile la akina dada wanaouza miili yao,nikakosa jibu .Nilitamani nishuke nikuondoe toka katika kundi lile lakini nikaamua niwatoroke wenzangu na kukuchukua kuja nawe hapa ili nipate walau fursa ya kuongea nawe.Kwa hiyo naomba ufahamu kwamba sina lengo la kuutumia mwili wako halafu nikulipe.Hata kama nikikulipa kiasi gani cha fedha ,hakitaweza kurudisha thamani ya utu wako.Kwa maana hiyo Marina naomba uwe huru na wazi kwangu,nomba tuongee kama marafiki.Lengo langu ni kukusaidia na pengine kukutoa kabisa katika biashara hii unayoifanya.”
Innocent alisema taratibu na kumfanya marina ainue uso wake na kumtazama usoni.Mara mlango ukagongwa,Inno akainuka na kwenda kufungua,alikuwa ni mtumishi wa hoteli aliyekuwa ameleta mvinyo.Inno akamimina katika glasi na kumpatia Marina ambaye aliupamba uso wake kwa tabasamu pana sana linalomfanya Innocent naye atabasamu
“Mtoto anaonekana anapenda sana ulevi huyu.” Innocent akawaza.
Marina akapiga mafunda kadhaa ya mvinyo ule halafu akakohoa kidogo na kusema
“Du ! huu mvinyo si mchezo.Kwani uncle ulikuwa unataka kunisaidia kivipi? Marina akauliza
“Ningependa kwanza kufahamu historia yako kwa ufupi tu,umetokea wapi,unaishi wapi,wazazi wako wako wapi, na mwisho ningependa kufahamu ni kwa nini uliingiia katika biashara hii ya ukahaba.”
Marina akainama chini akafikiri kwa sekunde kadhaa halafu akainua kichwa ,akamimina mvinyo katika glasi ,akagugumia yote,akaongeza tena nusu yake akainywa yote.Akaiweka glasi chini halafu akainama.baada ya kama dakika moja hivi akainuka,akafungua pochi yake na kutoa kitambaa kidogo.uso wake ulikuwa umejaa machozi.Innocent akastuka.
“marina kulikoni mbona hivyo? Mbona unalia? Nimefanya vibaya kukuuliza?
Huku akilia kichini chini Marina akasema
“Innocent kwa takribani miaka saba sasa sijawahi kukutana na mtu yeyote ambaye amewahi kuniuliza swali kama hili.Hakuna hata mtu mmoja ambaye amewahi kuhoji ni kwa nini ninauza mwili wangu,hakuna hata mtu mmoja ambaye amewahi kunionea huruma.Wewe ni mtu wa kwanza ambaye umeniuliza maswali ya namna hii.Wewe ni mtu wa kwanza ambaye umenirudishia tena historia mbaya ya maisha yangu ambayo tayari nilikwisha kuifuta kichwa mwangu.” Marina akasema huku akilia.
“Nyamaza kulia marina “ Innocent akamkaribia zaidi na kumbembeleza.
“Innocent ,ni mara ya kwanza leo nimekutana na mtu ambaye ameona thamani yangu na kukataa kuudhalilisha utu wangu kwa kuutumia mwili wangu na kunilipa fedha.Nimekuwa nikilala na wanaume wa kila aina,wengine ni viongozi serikalini lakini hakuna hata mtu mmoja ambaye amewahi kunionea huruma hata kwa umri wangu huu mdogo badala yake wengine wamekuwa wakinibaka,wengine wananitumia kwa nguvu bila kunilipa chochote ,nimekutana na
kila aina ya udhalilishaji wa dunia hii katika umri huu mdogo.Sijawahi thaminiwa hata siku moja.Ninaichukia dunia Innocent.Nimekwisha kata tamaa kabisa na maisha haya kiasi kwamba hata mimi mwenyewe sioni thamani ya utu wangu.”
Marina akanyamaza na kuendelea kulia.Innocent akambembeleza hadi akanyamaza.Akamimina mvinyo katika glasi akapiga funda kubwa akaweka glasi chini akaufungua mkoba wake na kutoa sigara.akaiwasha na kupiga mikupuo kadhaa .Huku sigara yake ikiwa mkononi akamgeukia Innocent na kusema
“Innocent siku ya leo nahisi ni kama nimekutana na Malaika kwa sababu kwanza umenileta katika hoteli hii kubwa ya hadhi,umeninunulia chakula kizuri,mvinyo safi na zaidi ya yote umenionyesha thamani yangu mimi kama mwanamke na kama binadamu.” Marina akasema huku akipiga mkupuo mwingine wa sigara na kupuliza moshi mwingi
“Marina siku zote mimi nimekuwa nikiheshimu sana utu wa mtu na ndio maana niliguswa sana nilipokuona pale klabuni umekaa katika genge la wanawake wanaojiuza.Ninauthamini utu wako ndiyo sababu niko hapa na wewe sasa hivi ili kutaka kukufahamu vizuri na kuona ni jinsi gani ninaweza kukusaidia”
Marina akamtazama Innocent usoni,akapiga tena mkupuo mwingine wa sigara,akageukia pembeni na kuupuliza moshi .
“Innocent mimi kwa sasa kunisaidia itakuwa vigumu sana kwa sababu tayari nimekwisha haribika.Sasa hivi kazi hii imekwisha niingia kwenye damu na siwezi kuiacha tena.Tayari nimekwisha ingia katika matumizi mabaya ya pombe na madawa ya kulevya kama bangi.Wakati mwingine tunachanganya na unga wa kulevya.maisha yangu tayari yamekwisha haribika.Kwa umri huu mdogo nilionao nimeshapitia mambo mengi sana.Nimepitia maisha magumu ambayo nikikuhadithia unaweza ukatoa machozi.Innocent nimekwisha kata tamaa na maisha yangu haya.Hapa nilipo sielewi kama nimekwisha athirika na ukimwi au la kwa sababu kuna wanaume wengine hawataki kutumia kondomu kwa hiyo inanilazimu kufanya nao mapenzi bila kutumia kinga.”
Marina akainama chini na kuzama katika mawazo mengi.Innocent akamtazama kwa makini akamuonea huruma binti yule .Taratibu akainuka akaichukua simu yake na kumpigia dereva wake wa kazini na kumwambia achukue gari la kampuni na kuwafuata dada yake na rafiki zake klabuni alikowaacha kwani yeye hatarudi tena kule.Baada ya kuongea na Juma akampigia dada yake sarah
“Innocent uko wapi? Mbona umesema unarudi sasa hivi lakini muda unazidi kwenda huonekani? Au umemkimbia Lulu? “ Saraha akasema
“hapana
si hivyo Saraha.Kuna mahala tumekwenda na rafiki zangu akina Abuu na nina wasi wasi tutachelewa kurudi.Kwa hiyo nimempigia simu Juma yule dereva wa kampuni aje awachukue na gari hapo klabuni.” Innocent akadanganya
“Haya Inno sisi tunaendelea tumeongezeka sasa tuko kama watu kumi na tano hivi.Leo ni mpaka asubuhi” Sarah akasema na kukata simu.Innocent akarejea pale sofani ambako bado marina alikuwa amejiinamia.
“Marina unaweza ukanieleza historia ya maisha yako? Innocent akauliza kwa sauti ya upole.
“Innocent historia ya maisha yangu hautapenda kamwe kuisikia.Haifurahishi na siku zote huwa sipendi kuongelea masuala yoyote yanaohusiana na historia ya maisha yangu kwa sababu huwa inaniumiza mno.”Marina akasema
“Jikaze Marina naomba unieleze japo kwa ufupi” Innocent akasisitiza
Marina akakaa kimya kidogo halafu akanywa mvinyo kidogo na kusema
“Innocent naona silewi kabisa.Unaweza ukaniruhusu nipulize jani kidogo?
“Jani gani? Innocent akauliza
“ah ! Innocent usijifanye hulifahamu jani bwana.Bangi” Marina akasema.Innocent akastuka,akafikiri kidogo halafu akasema
“Kuwa huru,we puliza tu” Innocent akajibu .Marina akatoa pakiti lililokuwa na bangi akaiweka mezani ,akachambua ,halafu akafunga katika karatasi moja nyeupe ,akainuka na kusogea pembeni,akaiwasha na kuvuta yote.alipomaliza akarudi sofani.
“sasa hapa najisikia kidogo afadhali” Marina akasema.Innocent akaendelea kumwangalia kwa mshangao.
“Innocent usishangae.Haya ndiyo maisha yangu.Bila kupata hii kitu maisha yangu hayaendi.Jani ndilo kila kitu kwangu,ndilo linanifanya niwe jasiri katika kukabiliana na maisha haya Hili ndilo linanifanya niwe kamanda.”Marina akasema.
“Marina hebu naomba unieleze historia ya maisha yako .”
Marina akamtazama Innocent ,macho yake yakiwa makavu halafu akasema
“kwa kuwa umeonyesha ni jinsi gani ulivyomstaarabu na mwenye utu ,nitakueleza bila kukuficha historia yangu yote hadi hapa nilipo japokuwa inaniumiza sana.” Marina akasema halafu akachukua glasi na kuumalizia mvinyo uliokuwa umebakia akatoa sigara na kuiwasha.
“Samahani kama ninakukera Innocent lakini siku zote nikiwa na mawazo mengi ni lazima nivute sigara “
“Usijali Marina jisikie huru” Innocent akajibu.
Marina aliivuta sigara ile kwa hisia kubwa akapuliza moshi mwingi juu huku Innocent akiendelea kumshangaa.Ilikuwa ni mara ya kwanza kushuhudia binti mdogo aliyekuwa amekubuhu katika ulevi namna ile.
“Historia yangu imeanza hivi” Akasema Marina huku akiishikilia sigara yake kwa mkono wa kulia.
“ Katika maisha yangu sikuwahi kumjua baba yangu mzazi.Kwa mujibu wa maelezo ya mama ni kwamba hata yeye hakumfahamu baba yangu ni nani. “ Marina akasema halafu akavuta tena sigara yake na kupuliza moshi juu ,akamtazama Innocent halafu akaendelea.
“kwa mujibu wa maelezo aliyonipa mama yangu,yeye alitokea mkoani Morogoro.Anadai kwamba huko alikotoka alikuwa yatima kwa hiyo baada ya taabu nyingi alizokuwa akipata kijijini kwao ,ikamlazimu kuja jijini dar es salaam kutafuta maisha.Alipofika hapa hakuwa na ndugu wala mtu yeyote aliyemfahamu.Alitafuta kazi sana bila mafanikio.baadae akapata kazi ya kuosha vyombo katika mgahawa wa mama mmoja maeneo ya Yombo.Kazi hiyo haikuwa na mshahara wa kutosha hivyo ikamlazimu kuacha kazi hiyo na kutafuta kazi nyingine.Alifanya kazi mali mbali kama kufua nguo za watu,kazi za ndani lakini bado hali ya maisha yake haikubadilika.Kwa kuwa alikuwa bado msichana mdogo na umbo lake lilikuwa la kupendeza akaamua kujiingiza katika biashara ya kuuza mwili baada ya kushawishiwa na rafiki zake
.
Alianza kuifanya biashara hiyo akiwa na umri wa miaka 18.Baada ya muda mfupi aliiona biashara hii kama ndiye mkombozi kwake kwa sababu iliweza kumsaidia kukidhi maisha yake na kumsaidia kimaisha.”
Marina akatulia tena akawasha sigara nyingine na kuvuta mikupuo kadhaa halafu,akaendelea na simulizi yake.
“Kwa mujibu wa maelezo yake ni kwamba kutokana na kuwa na wanaume wengi ambao hawakutaka kufanya mapenzi salama ,alikuwa akipata mimba nyingi na kutoa kwani hakuwa tayari kulea mtoto.Baada ya kuitoa mimba karibu saba akapata mimba nyingine na akajishauri sana katika kuitoa mimba ile na akaamua asiitoe ,akailea mimba ile na hatimaye akafanikiwa kuzaa mtoto ambaye ni mimi.Hata baada ya kunizaa mimi bado mama aliendelea na biashara ya ukahaba.Nikiwa darasa la tano mama akaanza kuumwa.hali yake ikazidi kuwa mbaya kadiri siku zilivyokuwa zikisonga.Maisha yetu yalibadilika kuanzia hapo kwa sababu maisha yetu kwa ujumla yalitegemaa biashara ile ya ukahaba aliyokuwa akiifanya mama.Mama akawa hawezi kutoka ndani na kwenda kufanya tena biashara ile na ndipo ilipobainika kwamba alikuwa ameathirika na virusi vya ukimwi.Hali ilikuwa mbaya ikanibidi kujiingiza katika biashara aliyokuwa akiifanya mama ya kuuza mwili kipindi hicho nikiwa mtoto mdogo wa miaka kumi na moja tu.Nilifanya biashara ile na kupata fedha za kumtibu mama na kuendesha maisha yetu.Wale waliokuwa wateja
wa mama wakageuka na kuwa wateja wangu.Niliendelea na biashara ile na mwishowe ikanilazimu kuacha shule ili niweze kupata muda mzuri wa kufanya kazi ile.Nikakubuhu ukahaba katika umri mdogo.”
Marina akavuta tena sigara,akakaa kimya kidogo halafu akachukua chupa ile ya mvinyo akamimina mvinyo katika glasi akapiga funda kubwa halafu akaendelea.
“Siwezi kusahau uchungu nilioupata baada ya mama yangu kufariki dunia.Yeye ndiye aliyekuwa ndugu yangu pekee ninayemfahamu.Yeye ndiye alikuwa kila kitu kwangu.baada ya mama kufariki sikuwa na namna nyingine ya kufanya kwa sababu hakukuwa na mtu au ndugu wa kuweza kunisaidia katika maisha hali iliyonilazimu kuendeleza kazi hii ya ukahaba mpaka hivi leo.” Marina akasema halafu akainama na kuivuta sigara yake,akatazama juu na kupuliza moshi hewani.
“Haya ndiyo maisha yangu Innocent.” Marina akasema.Innocent akamtazama usoni akamuonea huruma sana.
“Pole sana Marina.”
“Ahsante Innocent “ Marina akasema na kuizima sigara yake iliyokuwa imemalizika.
“Hebu niambie ukweli Marina.Kazi hii inakuingizia kipato cha kutosha kuweza kukidhi mahitaji yako ya kila siku? Innocent akauliza
“Inategemea na siku.Kuna baadhi ya siku tunaingiza pesa ya kutosha na baadhi ya siku unamaliza hata usiku mzima huna mteja yeyote.Kiujumla maisha ni magumu na tunakumbana na matatizo mengi kama vile wateja wakorofi ambao wanakutumia na kugoma kukulipa fedha.” Marina akasema na kutazama juu.Innocent akamtazama usoni kwa huruma halafu akasema
“Marina historia ya maisha yako imenigusa sana .najua uliamua kuifanya kazi hii si
kwa kuipenda bali ni kwa sababu hukuwa na njia nyingine ya kuweza kuishi.Toka moyoni mwangu nimeamua na niko tayari kukusaidia ili uweze kuondokana na maisha haya unayoyaishi.”
“Innocent katika maisha yangu yote sijawahi kutana na mtu yeyote ambaye ameonyesha kuguswa na matatizo yangu na kuamua kunisaidia.Nashukuru sana kwa hilo Innocent lakini sioni kama kuna haja ya kunisaidia na wala sioni sababu ya kunisaidia.maisha yangu yamekwishaharibika Maisha haya nimekwisha yazoea na sidhani kama kuna maisha mengine zaidi ya haya.” Marina akasema
“hapana Marina usiseme hivyo.Haya si maisha yako .Bado umri wako mdogo na una kila sababu ya kuishi maisha mazuri na yenye furaha.Unastahili maisha mazuri.” Innocent akasema
“hapana Innocent.Sihitaji maisha mazuri.Haya ndiyo maisha yangu.Sina baba,sina mama,sina ndugu yeyote sasa maisha mazuri niyatafute ya nini? Nimeridhika na maisha ninayoishi kwa sasa.”
“Marina hebu nisikilize kwa makini.Ni kweli nina nia ya dhati ya kukuondoa katika maisha haya unayoyaishi .”
“Innocent nimekwisha kwambia unapoteza muda wako bure wa kutaka kunisaidia.Sielewi unataka kunisaidia vipi kwa sababu hapa nilipo sina hata elimu ya kutosha,sina ujuzi wowote wa biashara iwapo utataka kunipatia mtaji wa biashara Innocent tafadhali usipoteze muda wako mwingi katika jambo hili.”
“Marina nimekuelewa vizuri sana.Lakini pamoja na sababu ulizozieleza bado nina lengo la kukusaidia na kukutoa katika maisha haya unayoyaishi sasa hivi.Kuhusu elimu nitakusaidia ili uweze kupata elimu hadi chuo kikuu na kuhusu…….”
Kabla hajaendelea Marina akaanza kucheka.
“hahahahahaaaaa !! leo umenifurahisa sana Innocent.Yaani mimi Marina nikasome?
“Ndiyo Marina hilo linawezekana kabisa.Marina unahitaji kukubali mabadiliko.bado u msichana mdogo na ambaye hustahili kuishi maisha haya unayoyaishi.”
“Innocent kama unataka kunisaidia ,labda unipe fedha za kutosha”
“Fedha si tatizo Marina.Ninaweza kukupa mamilioni ya fedha lakini hayatakusaidia kitu chochote.Ninachokitaka ni mabadiliko ya kifikra,kimaisha na kiroho pia.Unatakiwa uishi maisha yenye kumpendeza Mungu siku zote na ni yeye ndiye atakayekunyooshea mkono wake na kukumiminia baraka zake nyingi na utakuwa na maisha ya amani na furaha tele daima.”
“hahahaaaa ! Leo nimekutana na mchungaji..Hahahaa” marina akacheka kwa nguvu.
“Kumbe hata ninyi wachungaji huwa mnafuata makahaba..hahahaaa”
Innocent hakujibu kitu akaendelea kumtazama Marina aliyekuwa akicheka kicheko kikubwa.
TUKUTANE SEHEMU IJAYO
KWA SIMULIZI ZAIDI TEMBELEA HAPA MASIMULIZI
0 comments:
Post a Comment
Followers
MAHABA
SERENA
BEFORE I DIE
I DIED TO SAVE PRESIDENT
FAIDIKA NA MASIMULIZI
DEATH MESSENGER
CHOMBEZO ZA MASIMULIZI
MISS TANZANIA PART 2
Blog Archieves
April 2014
(57)
About Me
pettysean.blogspot.com
View my complete profile
Total Pageviews
BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU
Powered By
masimulizi
0 comments:
Post a Comment