Thursday, April 17, 2014

TEN CHAPTERS SEHEMU YA 15




RIWAYA : TEN CHAPTERS
SEHEMU YA 15

Kabla ya kufanya jambo ambalo nimedhamiria kulifanya nataka kwanza niandike kitabu cha historia ya maisha yangu ambacho kitakuwa na sura kumi kulingana na maisha yangu niliyoyapitia ambayo ninaweza kuyagawanya katika vipindi kumi na sura ya kumi ni hii ya maisha yangu ya Arusha kitabu ambacho nitakiita Ten  chapters.Katika kitabu hiki nitaeleza ukweli wote bila kuficha,mimi ni nani ,nimepitia mambo gani hadi hapa nilipofika.Kuna mambo mengi ambayo watu hawayafahamu kuhusu mimi.Nataka kupitia kitabu hicho wayafahamu.Wadogo zangu nao pia kuna mambo mengi sana ambayo hawayajui kuhusiana na mimi na sina ujasiri wa kuwaeleza kwa mdomo.Watasoma kupitia kitabu hiki na wakati wakisoma kitabu hiki sintakuwa katika upeo wa macho yao  kwani baada tu ya kumaliza kuiandika kitabu change nitapotea kama kimbunga.Najua wataumizwa sana lakini sina namna nyingine ya kufanya.Hii ndiyo njia pekee ya kuweza kuyamaliza maisha haya ya mateso na maumivu.” Alipowaza kuhusu hilo mara sura ya Genes ikamjia kichwani



            Saa kumi za jioni gari ndogo aina ya BMW rangi nyeusi iliyokuwa katika mwendo wa taratibu inawasha taa ya kushoto kuashiria kwamba ilikuwa ikiingia Beach paradise hotel moja kati ya hoteli kubwa na ya kisasa sana jijini Dar es salaam.Taratibu gari ile nyeusi ikaelekea hadi katika sehemu ya maegesho ambako alikuwepo mtu maalum aliyeyaongoza magari ili yaweze kuegeshwa katika utaratibu mzuri.Dakika kama mbili hivi toka gari lile liegeshwe mlango wa upande wa dereva ukafunguliwa na msichana mmoja mrembo kupindukia akashuka taratibu.Msichana huyu ambaye alikuwa amevaa kaptura fupi nyeupe na fulana ndogo iliyofunika matiti yake machanga na kuiacha sehemu yote ya tumbo lake ikiwa wazi akafungua mlango wa nyuma na kutoa kompyuta ndogo ya mkononi na chupa mbili,moja ikiwa ni ya maji ya kunywa na nyingine ilikuwa ni chupa ya mvinyo.Kwa muonekano wake ulivyo pamoja na umbo lake haikuwa rahisi kukubali kwamba msichana yule mrembo alikuwa akitumia mvinyo ule aliokuwa ameushika.Taratibu akatoa mkoba na kuiweka ile kompyuta yake na kisha akauvaa mkoba begani halafu akachukua pakiti la sigara,akatoa moja akaiwasha na kupiga mikupuo kadhaa halafu akatoa moshi mwingi akaupuliza hewani.Akalifunga gari lake kwa ufunguo kisha akabeba chupa zake mbili na kwa mwendo wa madaha akaanza kutembea kuelekea katika sehemu ya ufukwe.Hoteli hii ilisifika kwa kuwa na ufukwe tulivu na msafi.Watu wengi walipenda sana kuja kupumzika katika ufukwe wa hoteli hii maarufu.Watu wengi waliokuwepo katika hoteli hii wakipumzika jioni hii walimtolea macho ya mshangao binti huyu aliyekuwa akitembea taratibu kuelekea ufukweni lakini yeye hakujali mtu aliendelea kutembea kwa madaha huku akivuta sigara yake na katika mkono wake wa kushoto alikuwa ameshika chupa zake mbili moja ya maji ya kunywa na nyingine ya mvinyo.
   “ Kila nikiiangalia dunia sitamani tena hata kuishi ndani yake .Lakini kwa muda huu mfupi nilioishi hapa duniani sijayafurahia maisha hata kidogo.Ninawachukia binadamu sana.Mungu atanisamehe kwa kuwa na chuki kubwa namna hii kwa binadamu aliowaumba kwa mkono wake.Katika umri wangu huu mdogo nimejifunza mambo mengi sana na ambayo nitayaandika na kuyaweka kama kumbu kumbu na siku moja watu watayasoma na kuutambua ubaya wa binadamu.Nina imani kila mtu atakayesoma simulizi yangu atakubaliana nami kwamba dunia ya sasa imebadilika sana na binadamu ambao Mungu aliwaumba ili waishi maisha ya kumuambudu na kumtukuza yeye pekee kwa sasa wamemuweka pembeni na kumgeukia ibilisi ambaye anawadanganya kwa kuwapa furaha ya dunia na maisha matamu na kusahau kwamba Mungu huyo huyo wanayemuweka pembeni leo hii na kumpigia magoti ibilisi ndiye aliyemuumba ibilisi .Nataka niwaeleze watu kila nukta ya maisha niliyoyapitia.Nataka watu wapime wao wenyewe ni jinsi gani binadamu walivyo wanyama lakini papo hapo nataka niwape fundisho kwamba siku zote Mungu atabaki muumba na siku zote hakuna kiumbe mwingine kama yeye na humpa kila mwanadamu kile akiombacho kwa wakati ambao anaona yeye unafaa.Ninataka niwafundishe pia binadamu kwamba siku zote upatapo shida hutakiwi kukata tamaa.Matatizo ni sehemu ya maisha yetu na kupitia matatizo tunajifunza mambo mengi sana yaliyoko katika dunia hii ambayo bila ya matatizo hayo kamwe huwezi kuyafahamu.Kupitia matatizo tunafahamu upande wa pili wa mwanadamu ukoje.Mwanadamu ambaye kila siku uso wake umepambwa kwa tabasamu pana sana na akikuchekea hadi meno yote yanaonekana lakini ukiufahamu upande wake wa pili hutatamani tena hata kumuona mwanadamu huyo." akawaza yule msichana mrembo kisha akaichukua tena chupa yake ya mvinyo akanywa ,akaitazama bahari akatabasamu.
  " Hii ni sehemu ya kwanza ambayo nitaanza kuiandika simulizi yangu kwa sababu ndipo mahala kila kitu kilianzia.Nitatembelea sehemu zote ambazo nilikuwa nikizipenda,sehemu ambazo nilikuwa nikipata furaha,sehemu ambazo zilinifanya niipende dunia hii,sehemu nilizocheza na watoto wenzangu wakati huo na sehemu ambazo nilizoea kwenda na wazazi wangu ,nataka nikaziangalie kwa mara ya mwisho sehemu hizi zote kwa sababu sintapata tena nafasi ya kuziona au kupata furaha niliyokuwa nikiipata nyakati hizo.Nitaishukuru kila sehemu kwa kuwa iliwahi kuwa sehemu ya furaha yangu kwa wakati huo kabla sijawafahamu binadamu makatili.Kwa leo nitasema kwa heri kwa sehemu hii muhimu sana ambayo nilianzia safari yangu ya matatizo.Ninafurahi kupaona tena mahala hapa ambako miaka kadhaa uko nyuma palikuwa ni sehemu ya furaha yangu.Nilizoea kuja hapa na kuyaona na kufurahia mawimbi ya bahari yalivyokuwa yakiupiga mwamba huu na kisha maji yake kuruka na kutawanyika.Nilipenda kukaa na kurukiwa na maji ya bahari .Nilihisi furaha ya ajabu sana kipindi hicho lakini kwa sasa siwezi tena kuipata furaha hiyo.Siwezi tena kukaa na kuyafurahia tena mawimbi ya bahari yanavyoupiga ukuta wa mwamba huu.Sina tena sababu ya kufurahi .Nifurahi kwa sababu gani hasa? kwa nini nifurahie kuishi katika dunia iliyojaa wanadamu makatili wasio kuwa hata na chembe ya huruma? Sioni sababu ya kuwa na furaha katika dunia hii.Kitu kimoja tu ambacho kinanipa furaha kwa sasa ni kila nikiwaona wadogo zangu wapendwa ambao ndio ndugu zangu pekee ninaowafahamu wamekuwa watu wakubwa na wanaendelea vizuri na maisha yao.Nafurahi kwa sababu  hata baada ya matatizo yote haya kutokea lakini hata siku moja sijawahi kukubali taabu ya aina yoyote ile iwapate.Wamesoma na hadi sasa wamepata kazi na kila mmoja anajitegemea Ninasikia furaha sana nikiwaona wadogo zangu wakitimiza ndoto zao maishani.Kwa hilo ninaweza nikasimama na kujivuna mbele ya ulimwengu kwamba mimi ni mwanamke wa shoka.Nimesimama imara kuhakikisha kwamba ndugu zangu wanakuwa  na maisha bora.Nimewaongoza katika njia njema hadi hapa walipofika japokuwa mimi sikupitia njia iliyo njema hata kidogo.Muda wangu umefika sasa wa mimi kupumua na kumshukuru Mungu na kuwaacha ndugu zangu waendelee na maisha yao wao wenyewe na mimi nitafutika katika upeo wa macho yao na hawataniona tena .Najua watalia sana lakini watabaki na kumbu kumbu kubwa kwamba nilisimama kidete kuhakikisha kwamba wanapata elimu safi na malezi bora yenye maadili na wao watafanya vivyo hivyo kwa familia zao.Watahakikisha kwamba siku zote wanasimama imara katika kuzilinda familia zao hata kutokee dhoruba kali namna gani." akawaza msichana yule akachukua tena chupa yake ya mvinyo akanywa halafu akatoa sigara akaiwasha na kuendelea kuvuta huku akipuliza moshi mwingi hewani.

0 comments:

Post a Comment

Followers

 

BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU

Powered By masimulizi