MASIMULIZI
Wednesday, April 16, 2014
BEFORE I DIE SEHEMU YA 14
RIWAYA : BEFORE I DIE
SEHEMU YA 14
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
Huku akitabasamu Innocent akapanda juu ya kile kitanda cha magurudumu halafu muuguzi akaanza kukisukuma na kutoka ndani ya kile chumba.Moja kwa moja akapelekwa hadi katika mlango wa chumba cha upasuaji.Mlango ukafunguliwa na akaingizwa ndani.Katika chumba cha kwanza ambacho hakikuwa na vitu vingi akatokea daktari mmoja ambaye akamtazama na kumwambia.
“Innocent upasuaji tunaoenda kuufanya ni mkubwa na kabla hatujakuingiza katika chumba cha upasuaji ,una mtu yeyote ambaye ungependa kuwasiliana naye?
Inno akafikiri kwa sekunde kadhaa na kusema
“Nashukuru daktari lakini watu wangu wa muhimu tayari nimekwisha wasiliana nao.Mnaweza kuendelea na taratibu za upasuaji Innocent akasema na kisha daktari akaruhusu aingizwe katika chumba cha upasuaji.
ENDELEA…………………………..
Mara tu baada ya kumaliza kuongea na Innocent Latoya akajikuta amekaa juu ya meza.Alihisi baridi ya ghafla.
“Innocent ni kijana wa ajabu sana.Yaani kwa ajili ya kuokoa uhai wa Marina ameamua kujitolea figo yake mwenyewe? Sijawahi kukutana na kijana mwenye roho ya huruma kama yake.” Latoya akawaza huku akiifungua pochi yake kubwa na ghafla akatulia na kuanza kuwaza tena.
“Mbona nimeanza kuogopa ghafla namna hii? Nahisi mwili wote kunitetemeka.Namuonea huruma Innocent.Amejitolea kitu kikubwa sana kwa ajili ya kuokoa maisha ya msichana ambaye hana undugu naye wowote .Katika operesheni lolote linaweza kutokea.No ! Nothing bad is going to happen to him.He’s going to be ok .I must be there now.Ngoja niwahi hospitali ili nipate kuongea na Innocent walau maneno machache kabla hajaingizwa katika chumba cha upasuaji”
Latoya akawaza huku akiifunga pochi yake kubwa na kumpigia simu msaidizi wake kumtaarifu kwamba amepata dharura kwa hiyo hatakuwepo kwa siku hiyo.Kwa haraka Latoya akatoka na kumchukua Sabrina kisha wakaingia garini na kuelekea moja kwa moja hospitali
“Dada latoya una uhakika Innocent atakuwa mzima hata baada ya operesheni? Atakuwa katika hali yake ya kawaida baada ya kutolewa figo moja? Sabrina akauliza huu ameikunja mikono yake na kuiweka pamoja kifuani
“Sabrina usiwe na wasi wasi.Innocent atakuwa mzima.Operesheni kubwa kama hizi huwa zinafanywa na madaktari wataalamu sana kwa hiyo usiwe na wasi wasi wowote.Ninawaamini madaktari wa hospitali ile.Vile vile Innocent atakuwa katika hali yake ya kawaida hata baada ya operesheni kwa sababu mtu unaweza ukaishi ukiwa na figo moja bila matatizo.” Latoya akajibu
“Naogopa sana dada Latoya.Nina wasi wasi sana.Sitaki Innocent apate matatizo yoyote kwa sababu ni ndugu yangu pekee ninayemtambua kwa sasa.Ni yeye pekee ambaye alisimama na kunipigania hadi leo hii ninafanya kazi katika taasisi yako.” Sabrina akasema na kwa mbali machozi yakaanza kumchuruzika.Latoya akamtazama na kusema
“ Usilie Sabrina.Tunatakiwa tusimame imara kwa ajili ya Innocent.We have to be strong for him so stop crying”
Sabrina akatoa kitambaa na kujifuta kisha akachukua simu yake na kumpigia Grace.
“hallo Grace uko wapi sasa hivi?
“niko nyumbani najiandaa kwa ajili ya kuelekea chuoni” Grace akajibu
“Grace kuna tatizo limetokea”
“tatizo gani hilo” Grace akauliza kwa wasi wasi
“Ni kuhusu Innocent.”
“Innocent !! kafanya nini tena?
“Innocent ameamua kutoa figo yake moja kwa ajili ya kuokoa uhai wa Marina.Hivi tunavyoongea wanajiandaa kumuingiza katika chumba cha upasuaji.Mimi na dada Latoya tunaelekea huko kwa hiyo kama una nafasi nakuomba nawe ufike hospitali mara moja.Nadhani unafahamu ni namna gani Innocent alivyo mtu muhimu kwetu.”
Huku sauti yake ikionyesha mstuko wa dhahiri Grace akajibu.
“nakuja sasa hivi huko hospitali”
“Huyo Grace ni ndugu yako?” Latoya akamuuliza Sabrina baada ya kumaliza kuongea na Grace simuni.
“Grace ni msichana ambaye kwa pamoja tuko mahala tulipo kwa jitihada za Innocent.Sote tunaishi nyumbani kwao na ni Innocent aliyetusaidia mpaka tukafika hapa tulipo” Sabrina akasema na kumfanya Latoya azidi kuwa na mawazo mengi.
“Hivi huyu Innocent ni kijana mwenye moyo wa namna gani? Kwa mujibu wa maelezo aliyonipa Sabrina ni kwamba anamuheshimu Innocent kupita hata baba yake mzazi.Anasema mambo aliyomfanyia Innocent haoni hata ni neno gani alitumie kumshukuru.Si hawa wasichana wawili tu , anasema kwamba Innocent amekuwa akiwasaidia wau wengi pia.Innocent anaanza kunigusa sana.Sielewi ni kwa nini nimeguswa ghafla hivi wakati nimeonana naye kwa siku moja tu.Ninahitaji kumfahamu kijana huyu kwa undani wake.Kwa mbali ninaanza kuwa na mawazo kwamba labda
ile ndoto yangu imeanza kutimia.May be Innocent is the one “ akawaza
Latoya akastuliwa na simu yake iliyokuwa ikiita.Akaichukua akaangalia mpigaji akaamua kuizima kabisa.
“Sihitaji kuwasiliana na mtu yeyote muda kama huu.Akili yangu inawaza kitu kimoja tu Innocent atoke ndani ya chumba cha upasuaji mzima” Latoya akaongea huku sura yake ikionyesha alikuwa na mawazo mengi.Akageuka na kumtazama Sabrina
“Sabrina huyo Marina ulifanikiwa kumuona?
“Ndiyo nilimuona.Ni mimi ndiye nilikuwa nikimuhudumua Innocet alipomleta pale nyumbani.” Sabrina akajibu
“Unaweza ukamuelezeaje Marina? Latoya akauliza tena
“Ni msichana mdogo lakini aliyepitia shida nyingi kutokana na aina ya maisha anayoyaishi.Ukikaa na kuongea naye ni msichana jasiri sana lakini anaonekana kukata tamaa na kuridhika na maisha anayoyaishi sasa”
“Is she pretty” Latoya akauliza na kumfanya Sabrina atabasamu
“kwa kweli napenda nikiri kwamba Marina ni binti mzuri ingawa kutokana na maisha yake ule uzuri wake wa asili umeanza kujificha lakini ni binti mzuri.Kwa nini umeuliza hivyo?”
“Nimeuliza hivyo ili kufahamu ni kitu gani kimepelekea hadi Innocent akubali kufanya alivyofanya.Kumtolea figo mu ambaye humfahamu na huna mahusnao naye yoyote si suala rahisi sana lakini Innocent ameweza kufanya hivyo”
“dada Latoya kaka Innocent ndivyo alivyo.Katika maisha yake hapendi kuona mtu akiteseka.Yuko tayari kwa lolote ili kumsaidia mtu yeyote mwenye uhitaji”
Latoya na Sabrina wakawasili hospitali na moja kwa moja wakaulizia mapokezi kama tayari Innocent ameingizwa katika chumba cha upasuaji wakajibiwa kwamba bado alikuwa akiandaliwa.Kwa kasi ya ajabu wakaelekea katika chumba cha upasuaji.Wakafika katika mlango wa kuingilia chumba cha upasuaji na kugonga kisha ukafunguliwa na muuguzi aliyekuwa amevaa mavazi ya kijani.
“Dada tunaomba utusaidie.Kuna kaka mmoja anatarajia kufanyiwa upasuaji wa figo mchana huu sisi ni ndugu zake na tumekuja ili walau kuongea naye kabla hajaingizwa katika chumba cha upasuaji” Latoya akasema huku moyo ukimwenda mbio
“samahani dada zangu.mmechelewa kidogo sana kama dakika mbili zilizopita Innocent ameingizwa katika chumba cha upasuaji ambako si rahisi kwa mtu asiye daktari kuingia.Itawabidi mkae hapa msubiri hadi opresheni itakapokwisha” Muuguzi yule akawataarifu akina Latoya ambao walionyesha kuishiwa nguvu na majibu yale.Taratibu wakajivuta na kukaa katika sofa kubwa jeusi lililokuwa hapo nje ya chumba cha upasuaji.
Kila mmoja alionekana kuwa na mawazo mengi .Latoya alikuwa ameinama huku amekiegemeza kichwa katika mikono yake.Dakika kama kumi hivi toka wamewasili pale hospitali mara wakatokea Grace na mama yake Innocent
“Grace Innocent yuko wapi? Akauliza mama yake Innocent huku akihema
“Mama tayari amekwisha ingizwa katika chumba cha upasuaji na si rahisi kuonana naye kwa sasa.Tumeambiwa tusubiri hapa hapa nje hadi operesheni itakapomalizika baada ya masaa matatu.”
Mama yake Wayne akainua mikono yake na kukishika kichwa .
“Jamani hivi huyu Wayne amepatwa na nini hadi anaamua kufanya mambo ya hatari kama haya? “ Akalalama mama yake Wayne.Latoya ambaye muda wote alikuwa amekaa kimya akamtazama kwa macho makali.Muda huo huo baba yake Wayne akatokea.
“Hebu niambieni nini kinaendelea hapa? Akahoji mzee Benard baba yake Innocent huku jasho likimtiririka.
“Innocent tayari ameingizwa katika chumba cha upasuaji.” Mke wake akasema huku kwa mbali akitokwa na machozi.Jibu lile likamfanya mzee Benard kukaa kimya na kujitenga pembeni akiwa na mawazo mengi.Wakati kila mmoja akiwa kimya akiwaza lake mara kwa kasi akapitishwa msichana mmoja na kuingizwa katika chumba kile cha upasuaji.Alikuwa ni Marina.Sabrina akamsogelea Latoya na kumnong’oneza.
“Huyo msichana aliyepitishwa hapa ndiye Marina.” Latoya hakujibu kitu zaidi ya kutikisa kichwa chake.Akiwa ameinamisha kichwa akiwaza akastuliwa na sauti iliyomuita.Akainua kichwa na kutazama mtu aliyemuita akakutanisha macho na Dr.Rajiv Patel mkurugenzi wa hospitali hii aliyekuwa akimuangalia kwa mshangao.Hakuamini macho yake kwa kumuona Latoya maeneo yale.
“Dr Rajiv “ Latoya akasema na kuinuka wakapeana mikono.Daktari Yule alikuwa akimuangalia Latoya kana kwamba ameona malaika.Hakuyaamini macho yake
“Latoya mbona uko hapa? Kuna tatizo gani? Una mgonjwa humu ndani? akauliza Dr Rajiv huku mikono ikimtetemeka.
“Ndiyo Rajiv,kuna rafiki yangu anafanyiwa upasuaji sasa hivi”
“Ni huyu kijana anayefanyanyiwa upasuaji wa figo?
“Ndiye huyo huyo”
“Latoya kwa nini hukunitaarifu kama una mgonjwa hapa hospitali? Ulipaswa kunitaarifu ili nijue kama yule ni mgonjwa wako.Karibu basi ukapumzike kule sehemu ya V.I.P. wakati ukisubiri operesheni imalizike.Operesheni hii itachukua si chini ya saa tatu” Dr Rajiv akasema
“Nashukuru sana Dr Rajiv lakini naona ni bora kama nikikaa hapa ili kusubiri operesheni hiyo imalizike.” Latoya akasema
“Naelewa Latoya lakini mtu kama wewe hutakiwi kukaa sehemu kama hii.Tuna sehemu maalum kwa ajili ya kupumzika watu kama ninyi.Sehemu nzuri na yenye usalama wa kutosha. ” Dr Rajiv akasisitiza na kumfanya Latoya atabasamu.
“Dr Rajiv ningependa sana kuelekea huko lakini naona ingekuwa vyema kama nikikaa hapa hadi operesheni itakapokamilika.Ahsante sana Dr Rajiv kwa ukarimu wako.” Akasema Latoya
“ Latoya wewe ni mtu muhimu sana kwetu unastahili huduma za kipekee kabisa.Nasikitika sana kwa kutofahamu kama ulikuwa hapa muda mrefu.Kama haujisikii kwenda kukaa kule V.I P basi ngoja niwatume wahudumu walete meza hapa waweke pale pembeni ili uendelee kupumzika wakati operesheni ikiendelea.”
“ Ahsante sana Dr Rajiv.Naomba usisumbuke mimi hapa pananitosha sana “.akasema Latoya .
Dr Rajiv alionekana kutoridhishwa kabisa na kitendo cha Latoya kukaa pale nje ya chumba cha upasuaji.Kwa shingo upande akaagana na Latoya kwa ahadi ya kuonana naye baada ya muda mfupi kwani alitakiwa kuhudhuria kikao muhimu sana.Alipopiga hatua mbili akageuka na kuuliza .
“ Walinzi wako wako wapi? Akauliza Dr Rajiv .Huku akitabasamu Latoya akajibu
“ Leo nimeamua kutembea mwenyewe bila ulinzi wowote”
Kitendo cha Latoya kunyenyekewa namna ile na mkurugenzi wa hospitali ile kiliwashangaza sana wazazi wa Innocent.Kila mmoja alikuwa akijiuliza huyu msichana ni nani? Swali hilo likawafanya wamwite Grace na kumuuliza kama anamfahamu Latoya.
“Yule anaitwa Latoya ndiye aliyempa kazi Sabrina.Ana taasisi yake ya kuwasaidia wanawake na watu wenye matatizo mbali mbali nadhani ni rafiki wa Innocent ndiyo maana yuko hapa sasa hivi”
“Kumbe Innocent ana marafiki wazuri kama huyu sasa kwa nini apoteze muda na hatimaye ahatarishe maisha yake kwa ajili ya wasichana machangudoa wasiokuwa na msaada wowote kwake? Mzee Benard akauliza huku ameikunja sura.
“Huyu niliyekuwa naongea naye ndiye mkurugenzi wa hospitali hii anaitwa Dr Rajiv Patel.” Latoya akamwambia Sabrina baada ya Dr Rajiv kuondoka.
“Inaonekana anakufahamu sana” Sabrina akasema
“Tunafahamiana sana kwa sababu huwa ananisaidia
pindi ninapokuwa na wagonjwa wa kuwapeleka nje ya nchi.Ni rafiki yangu sana” Latoya akasema kisha kimya kidogo kikapita halafu akauliza
“Sabrina umeishi na Innocent kwa muda sasa,unaweza ukanieleza kwa undani ni mtu mwenye tabia zipi?
“dada Latoya nashindwa hata nikuelezee vipi kuhusu Innocent kwa sababu maelezo yake ni mengi sana.Naomba tukitoka hapa unikumbushe nitakueleza mambo mengi kuhusiana naye.Naogopa kuongea hapa mbele ya wazazi wake.Mama yake hatupendi sana mimi na Grace na ni yeye ndiye aliyesababisha Innocent aamue kuondoka pale nyumbani” Sabrina akasema kwa sauti ndogo.Ni wazi alikuwa akiwaogopa wazazi wa Innocent.
Dakika arobaini zilikatika wakiwa bado wako pale nje ya chumba cha upasuaji .Kila mmoja akiwa kimya akiwaza lake,mara milango ikafunguliwa na wauguzi wakatoka wakikisukuma kitanda kilichokuwa kimefunikwa shuka.Wote walikuwa na nyuso za huzuni.Nyuma yao alikuwepo daktari mmoja ambaye alikuwa na mavazi yake ya kijani akawafuata akina Grace ambao walikuwa wamesimama kwa wasi wasi baada ya kuona kitanda kile kikitolewa mle ndani.
TUKUTANE TENA SEHEMU IJAYO……………..
KWA SIMULIZI ZAIDI TEMBELEA HAPA MASIMULIZI
0 comments:
Post a Comment
Followers
MAHABA
SERENA
BEFORE I DIE
I DIED TO SAVE PRESIDENT
FAIDIKA NA MASIMULIZI
DEATH MESSENGER
CHOMBEZO ZA MASIMULIZI
MISS TANZANIA PART 2
Blog Archieves
April 2014
(57)
About Me
pettysean.blogspot.com
View my complete profile
Total Pageviews
726,808
BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU
Powered By
masimulizi
0 comments:
Post a Comment