MASIMULIZI
Friday, April 11, 2014
BEFORE I DIE SEHEMU YA 10
RIWAYA : BEFORE I DIE
SEHEMUI YA 10
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Kwa hiyo baada ya kuzunguka kote ukaona hapa ni kituo cha kulela watoto wasio na wazazi.Nakupa wiki moja huyu kahaba awe ameondoka humu ndani mwangu..” baba yake Inno akasema kwa ukali huku akiinuka na kuondoka pale sebuleni.Kwa unyonge Innocent akaondoka pale sebuleni na kuingia chumbani kwake.Kwa maneno makali aliyoambiwa na baba yake yakamfanya adondoshe chozi.Akasimama pembeni ya kabati la nguo akainama na kufikiri halafu akatoka na kurudi tena katika chumba cha marina.
“marina unajisikiaje kwa sasa?
“Kwa sasa naendelea vizuri.isipokuwa mwili ndio unawaka moto.nadhani ni kwa sababu ya yale madawa tunayotumia.hata hivyo nashukuru kwa sababu mimi ndiyo kwanza nimejifundisha kuyatumia kwa hiyo sikuwa bado mtumiaji mkubwa na ndio maana ninaimani nikiyavumilia mateso kwa muda mfupi nitashinda.”
“Sawa vumilia Marina ,kesho asubuhi nitaonana na daktari ili tuone namna tunavyoweza kukusaidia.Grace atakuletea chakula sasa hivi.Nakuomba ule halafu ulale.”
“nashukuru sana kaka Innocent”
ENDELEA……………….
Asubuhi kabla ya kwenda kazini Innocent akaenda kumjulia hali Marina na kumkuta anaendelea vizuri japokuwa bado maumivu ya mwili yalikuwa yakiendelea.Saa tano akiwa ofisini kwake mara simu ikapigwa toka nyumbani kwao.Alikuwa ni Grace
“Grace habari za huko nyumbani?
“Habari za hapa nyumbani si nzuri sana”
“Kuna kitu gani kimetokea? Innocent akauliza huku akiwa na wasi wasi
“kaka Inocent leo asubuhi ulipoondoka Marina aliamka kwa ajili ya kwenda kuoga.Baada ya kuoga nikamtengenezea uji akanywa.Wakati akinywa mama akatokea na ghafla Marina akatapika kitendo kilichomuudhi mno mama ambaye alianza kumtukana na kumfukuza mle ndani.Hivi tunavyoongea Marina hajulikani yuko wapi.Nimeona nikufahamishe ili utafute namna ya kumsaidia .”
Innocent akapumua kwa nguvu na kuegemea kiti chake.akazama ghafla katika mawazo mazito.
“Marina
amekwenda wapi? Yawezekana amerudi kule alikokuwa akiishi? Kwa nini mama amfukuze Marina nyumbani? Lakini sishangai kwa jambo kama hili kwa sababu toka jana familia nzima haikuonyesha kupendezwa na kitendo cha kumpeleka Marina pale nyumbani.Kwa mara ya kwanza hata baba alinitolea maneno makali mno.Ngoja kwanza nielekee nyumbani nijue nini kimetokea kule halafu nijue wapi pa kumtafutia Marina.Lazima nimpate” Innocent akawaza huku akiinuka na kuvaa koti lake,akatoka ofisini akaingia garini na kuelekea moja kwa moja nyumbani kwao.
“maisha ya Marina yanaongezeka ugumu kila uchao.Jana kakamatwa kwa wizi,leo kafukuzwa nyumbani,nini itakuwa hatima yake? Binti yule anahitaji msaada mkubwa na hakuna mtu yeyote anayeonyesha kumjali.Kwa kuwa nimekwishajitoa kumsaidia sina budi kufanya kila linalowezekana ili kumuondoa binti yule katika maisha haya anayoyaishi sasa hivi.Kitu kikubwa ninachotakiwa kufanya kwa sasa ni kumtafutia sehemu ya kuishi kwanza ndipo mambo mengine yafuate.Nilipenda sana aishi nyumbani kwetu kwa sababu pale angejiepusha na mambo mengi sana.Nikimpata leo hii nitarudi naye nyumbani na kujaribu kumshawishi tena mama ili akubali Marina aishi pale nyumbani wakati nikimtafutia sehemu nyingine ya kuishi” Aliwaza Innocent akiwa njiani kuelekea nyumbani.
Baada ya kuwasili nyumbani moja kwa moja akaelekea katika chumba alimokuwa amelala Marina,lakini hakuwepo mle chumbani.Alisimama na kuushika ukuta huku ameinamisha kichwa akifikiri,mara mlango unafunguliwa na Grace akaingia.Innocent akainua kichwa akamtazama halafu akasema
“Grace hebu nieleze ni kitu gani kimetokea mpaka Marina akaondoka?
“Kaka Innocent kilichotokea ni kwamba baada ya Marina kuamka alitengenezewa uji akanywa na mara tu baada ya kunywa alitapika sana mbele ya mama,kitendo kilichomuudhi na kuamua kumfukuza .”
“Alipoondoka hakuwaeleza alikuwa akieleka wapi? Innocent akauliza
“hapana kaka Innocent ,hakutuambia mahala alikokuwa akielekea.” Grace akajibu
“mama amekwenda wapi? Inno akauliza
“Alisema anakwenda kutengeneza nywele na atarejea muda si mrefu”.
Innocent akafikiri kwa sekunde kadhaa halafu akaingia katika gari lake akaondoka .
“Ni lazima marina apatikane leo.Amekwisha onyesha kila dalili za kutaka kubadilika.Nikimuacha atarudia maisha yake ya awali kwa sababu hana msaada wowote ule.Hana mtu yeyote wa kumsaidia zaidi yangu.Ngoja nikamuangalie kule anakoishi na wasichana wenzake.Litakuwa jambo la busara kama nikimtaarifu na mzee Mustapha kitu kilichotokea” Innocent akawaza huku akipunguza mwendo wa gari na kulisimamisha pembeni halafu akachukua simu yake na kumpigia mzee Mustapha
“Hallo mzee Mustapha shikamoo mzee wangu” Innocent akasema baada ya mzee Mustapha kupokea simu.
“Marahaba Innocent habari za toka jana?
“habari nzuri mzee ila kuna tatizo limetokea “
“Tatizo gani Innocent? Mzee Mustapha akauliza
“marina ametoweka nyumbani asubuhi ya leo na sijui yuko wapi.Kwa hivi sasa niko njiani nakuja ili tukamuangalie kule katika chumba chao”Inno akasema
“Nadhani atakuwa amerudi kule mahala wanakoishi.Maisha yale alikwisha yazoea hivyo itamchukua muda mrefu kuyazoea mazingira mapya.Nina imani atakuwa amerudi kule kwenye makazi yao” Mzee Mustapha akasema
“Ok mzee Mustapha nitafika hapo muda si mrefu ili tukamuangalie huko” Akasema Inno na kukata simu
Ilimchukua saa moja na dakika kadhaa kuwasili nyumbani kwa mzee Mustapha.Alitumia muda mrefu kutokana na foleni ndefu za magari katika jiji hili la Dar
“karibu sana Innocent” mzee Mustaha akamkaribisha Inno baada ya kuwasili pale kwake.
“ahsante sana mzee “ akasema Inno huku akishuka na kufunga milango ya gari halafu kwa pamoja wakaanza kuelekea katika makazi ya wasichana wale wanaofanya biashara ya kuuza miili ambako Marina naye huishi huko.
“Mzee Mustapha suala la Marina linaoneka kuwa gumu sana” Innocent akasema.Mzee Mustapha akamtazama halafu akasema
‘kama nilivyokwambia Innocent,Marina amekwisha yazoea maisha haya anayoyaishi kwa hiyo itamchukua muda kidogo kuubadili mfumo wa maisha yake na kuanza maisha mapya.Naomba usikate tamaa Innocent kwa sababu wewe ndiye mtu pekee ambaye uliyebaki wa kuweza kumsaidia.Kitu cha muhimu ninachokiona mimi ni kwamba ili kumsaida binti huyu
ni lazima kwanza aondoke mahala hapa.Ni lazima aachane na magenge haya ya makahaba Kama akiendelea kukaa hapa tutakuwa tunatwanga maji katika kinu kwa sababu hataweza kuacha tabia zake.Akiwa hapa bado ataendelea kuvuta bangi,kutumia unga na biashara ya ngono.Ili tufanikiwe inatubidi tumuondoe hapa haraka” Mzee Mustapha akasema .Innocent hakusema kitu alikuwa akitembea huku ameinama chini akifikiri.
“Mzee Mustapha anayoyasema ni ya kweli kabisa.Kuna kila ulazima wa kumtoa Marina hapa.lakini ataishi wapi? Nilitegemea nyumbani kwetu kungekuwa ni sehemu nzuri na salama lakini nako mama anawasha moto hataki kumuona .Ngoja nikajaribu tena kwa mara nyingine kumshawishi mama akubali Marina akae pale nyumbani japo kwa siku kadhaa wakati nikiangalia uwezekano wa kumtafutia makazi ya kudumu.” Innocent akawaza wakati wakikata kona kuingia katika nyumba wanayoishi wasichana wanaofanya biashara ya ukahaba ambako anaishi pia Marina.Mzee Mustapaha ndiye aliyekuwa ametangulia mbele.Toka afanyiwe udhalilishaji na wasichana wakaao katika chumba hiki Innocent amekuwa muoga mno na kama si suala la Marina aliapa kutokurudi tena eneo hili.Mzee Mustapha akagonga mlango na ukafunguliwa na msichana mmoja mwenye macho mekundu aliyeonekana kana kwamba alikuwa ametoka kulala.
“Habari yako binti” mzee Msuatapha aksema
“Nzuri mzee Mustapha shikamoo” akasalimu binti yule
“Marahaba.namuulizia Marina .Yupo humu ndani?
“marina yupo.” Akasema yule binti huku akimuita Marina
Akiwa na sura iliyosawajika Marina akajitokeza pale mlangoni.Akatabasamu baada ya kuwaona mzee Mustapha na Innocent.
“karibuni ndani” akasema huku akijilazimisha kutabasamu
“ahsante Marina.Tulijua tutakukuta huku.Innocent amepigiwa simu akiwa kazini kwamba umetoroka nyumbani kwao.kwa nini umefanya hivyo Marina?.Mzee Mustapha akauliza
“Kweli Marina nimepigiwa simu na Grace akanitaarifu kwamba kulikuwa na kutokuelewana na mama kwa hiyo ukaamua kuondoka.Nimeamua kuacha kazi na kuja kukutafuta.” Innocent naye akaongezea.
Michirizi ya machozi ilionekana katika macho ya Marina na kwa kutumia viganja vya mikono yake akayafuta.
“Innocent najua wewe ni mtu mwema sana na una nia ya dhati ya kunisaidia.Si kwamba nilifanya makusudi kuondoka pale nyumbani lakini mama yako hakupenda nikae pale.Kuanzia asubuhi nimekuwa nikisikia akiongea maneno mengi sana ya kunikashifu.Nilivumilia kwa sababu nimekwisha zoea kashfa.Kilichonifanya niondoke ni baada ya kutapika uji niliopewa na Grace na mama yako akanitukana mno.Sikuona sababu ya mimi kutukanwa namna ile nikaamua kuondoka.” Marina akasema huku machozi yakiendelea kuchuruzika mashavuni mwake.
“Marina ,mama yangu ni mtu ambaye inahitaji moyo kuishi naye.Ninamfahamu vizuri mama yangu.Nafahamu kwamba hakupendezwa na suala la wewe kuwepo pale nyumbani lakini nilikwisha ongea naye pamoja na baba kwamba uwepo wako pale ni kwa muda mfupi wakati nikikuandalia sehemu nzuri ya kuishi.Wakati mchakato wakupata mahala utakapoweza kuishi kwa uhuru ukiendelea niliona ni vyema kama utakaa pale nyumbani ambako kuna huduma zote.Kwa hiyo Marina nimekuja kukuchukua tena ili ukaishi nyumbani kwetu wakati nakutafutia sehemu nzuri utakapoweza kuishi.” Innocent akasema huku akimsogelea marina aliyekuwa ameinama chini akitokwa na machozi
“Innocent siwezi tena kurudi kule kwenu.Mama yako anaweza hata kuniua kwa namna anavyonichukia.Mimi nitaendelea kuishi hapa hapa.japokuwa ni maisha ya shida lakini ninaishi kwa furaha na amani.” Marina akasema
“tafadhali marina ,nakuomba umsikilize Innocent anavyokwambia.Amini kile anachokueleza.Hapa unaposema unakaa kwa amani muda si mrefu serikali ya mtaa tutawahamisha wote,sasa utakwenda wapi? Nakuomba binti yangu kubali kufuatana na Innocent.Yeye ndiye anayejua nini amekiandaa kwa ajili yako” Mzee Mustapha akasema.Kauli ile inamfanya Marina kulegeza msimamo wake na akakubali kuondoka na Innocent.
“Oya brother mbona unamchukua mdogo wetu kienyeji enyeji ? ,tuachie basi hata msimbazi mmoja tupone asubuhi hii.”Alisema mwanamke mmoja mwenye sauti ya kukwaruza aliyekuwa amesimama mlangoni wakati Innocent na mzee Mustapha wakiondoka na Marina.Innocent akageuka akatabasamu ,akatoa pochi na kuchomoa noti moja ya shilingi elfu kumi akampa yule dada.
“brother wewe mzungu.Ila yule mzee mwanga tu.Kila siku anatuwangia kutaka kutuhamisha.Mwambie tutamfanyia kitu mbaya sisi,tumeshachoka na maisha haya” dada yule akalalama akimnyooshea kidole
mzee Mustapha..
Innocent akaagana na mzee Mustapha halafu yeye na Marina wakaingia garini na kuondoka.
“marina naomba usiwe na wasi wasi na nyumbani kwetu.Pale ni sehemu salama na utakaa kwa muda tu wakati nikikutafutia sehemu nzuri ya kuishi” Innocent akasema
“Mimi sina tatizo Innocent..Mimi kamanda.Mimi naishi mazingira yoyote yale.Tatizo ni mama yako hataki kuniona nyumbani kwenu.” Marina aliongea huku akifumba macho kana kwamba anasikia maumivu makali.Innocent akamtazama halafu akauliza
“Unasikia maumivu makali?
“Nasikia maumivu makali hasa sehemu hizi” akasema huku akigusa sehemu alizokuwa akisikia maumivu.
“Toka lini umeanza kusikia maumivu hayo? Inno akauliza
“Muda mrefu sasa.Huu ni mwezi kama wa nane sasa.Maumivu haya huwa yanakuja na kupotea lakini kwa siku za hivi karibuni yamekuwa makali zaidi”
“Umeshawahi kwenda hospitali kupima na kuangalia nini kinakusumbua?
“ hapana sijakwenda.Nikisikia maumivu huwa natumia dawa maumivu yanapotea..”
“Umechoma sindano leo? Inno akauliza akimaanisha sindano ya dawa za kulevya
“Sijafikia bado kuchoma sindano.Dawa nimeanza kutumia hivi karibuni.Ninachotumia sana ni bangi na pombe.Unga ni mara chache sana.” Marina akasema
“ Ok.usijali Marina .Kwa sasa ninaelekea ofisini kwangu kuna kikao natakiwa kukiendesha.Nitakukabidhi kwa mtu akupeleke hospitali kwa ajili ya vipimo halafu jioni tutakwenda wote nyumbani”
Walifika ofisini ,Innocent akamkabidhi Marina kwa daktari wa kampuni ili ampeleke hospitali kucheki afya na yeye akaendelea na kazi zake.
*
*
*
*
Saa kumi za jioni Dokta Peter Mbarali akarejea na Marina.Moja kwa moja akaelekea katika ofisi ya meneja wake Innocent.
“Bosi nimempeleka Marina hospitali ,wamemfanyia uchunguzi na Marina amegundulika kuwa na matatizo ya figo.Kwa mujibu wa madaktari figo zake zote zinashindwa kufanya kazi sawasawa na madaktari wana wasi wasi kwamba kuna nafasi kubwa ya muda si mrefu figo hizo kushindwa kabisa kufanya kazi.Madaktari wameshauri uonane nao haraka iwezekanavyo ili kwa pamoja muangalie jinsi ya kuweza kumsaidia Marina.” Dr Peter akasema huku akimkabidhi Innocent bahasha lililokuwa na vyeti mbali mbali toka hospitali.Innocent akaviangalia vyeti vile akavuta pumzi ndefu.
“marina unajisikiaje kwa sasa? Inno akamuuliza marina aliyekuwa amekaa katika sofa la pembeni
“ najisikia afadhali si kama asubuhi.Nimepewa dawa zinanisaida sana”
Innocent akamuangalia marina usoni kwa dakika takribani mbili
halafu akasema
“Dr Peter naomba umpumzishe Marina kule ofisini kwako,bado nina kazi muhimu nazimalizia.Hawa madaktari nitakwenda kuonana nao kesho” Dr Peter akamchukua Marina na kwenda kumpumzisha katika chumba cha kupumzishia wagonjwa kwa dharura pale kiwandani.
“My God why her? “ Innocent akasema taratibu baada ya Marina na Dr Peter kutoka mle ofisini mwake.
“kwa nini mzigo wa mambo yote haya umuelemee yeye peke yake? Lakini Leo nimegundua kitu ambacho sikuwa nimekigundua hapo awali.Marina ana uzuri wa asili uliojificha .Mtoto yule ni mzuri.Kuna kitu nimekiona katika macho yake ambacho kimenisisimua mwili wangu wote.Sielewi kama niko sahihi kwa hisia zangu lakini nahisi hisia zangu ziko sahihi.There is a connection between us.Kuna nguvu inayonivuta kuwa karibu na Marina.” Innocent akawaza halafu akainuka na kusimama
huku mikono yake imeshikilia kiti
“No ! No No Innocent you are wrong.Marina isn’t the one”” Innocent akasema kwa sauti ndogo huku akizunguka zunguka mle ofisini.Akaenda na kusimama dirishani.
“ A woman of my deams must be simple,educated,full of love,…and…..” Innocent akawaza akahisi kama kichwa kikimuuma.
“marina is a simple girl,asiyekuwa na elimu but I can see something in her eyez..I can see passion..I can see love..Kama akibadilika anaweza akanifaa.” Mawazo ya innocent yakakatizwa na simu ya mezani iliyolia mle ofisini.
TUKUTANE TENA SEHEMU IJAYO….
KWA SIMULIZI ZAIDI TEMBELEA HAPA MASIMULIZI
0 comments:
Post a Comment
Followers
MAHABA
SERENA
BEFORE I DIE
I DIED TO SAVE PRESIDENT
FAIDIKA NA MASIMULIZI
DEATH MESSENGER
CHOMBEZO ZA MASIMULIZI
MISS TANZANIA PART 2
Blog Archieves
April 2014
(57)
About Me
pettysean.blogspot.com
View my complete profile
Total Pageviews
BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU
Powered By
masimulizi
0 comments:
Post a Comment