MASIMULIZI
Saturday, April 26, 2014
SERENA SEHEMU YA 22
RIWAYA : SERENA
SEHEMU YA 22
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
Huku machozi yakimtoka Serena akamkumbatia Dr Jason kwa nguvu zaidi.
“Dr Jason I don’t know what I should say.I don’t know what to pay you.Hakuna kitu ninachoweza kukulipa kitakachozidi thamani ya hiki ulichokifanya..Dr J……..
“Shhhhhh…” Dr Jason akamkata kauli Serena ambaye alipatwa na furaha ya ajabu isiyo kifani.
“Don’t mention that.I promised you to make your father alive and I’ve kept my promise.” Akasema Dr Jason huku akitabasamu.
“Follow me” Akasema Dr Jason ,Serena akamfuata kuelekea katika chumba alimowekwa mzee Albano.Wakaufikia mlango wa chumba kile,wakasimama mlangoni .Toka katika kioo cha mlangoni hapo mzee Albano aliweza kuonekana akiwa amelazwa kitandani na pembeni yake alikuwepo Dr anna Maria.
“Ouh my father.Thanx God !!.” akasema Serena huku akilia.Akageuza kichwa akagonganisha macho na Dr Jason ambaye alikuwa na uso uliojaa tabasamu kubwa.Madaktari wenzake wageni wakatokea.
Akiwa na uso uliojaa tabasamu Dr Jason akawakumbatia madaktari wenzake waliomsaidia katika kufanikisha kazi ile ngumu.
ENDELEA……………………………………..
Saa kumi na mbili na robo za asubuhi gari la hospitali ya Patrick Charles memorial linalotumika katika kubeba wafanyakazi likawasili hospitali .Zakaria mwasigala ,Bi Bertha kitola pamoja na Maimuna rahim ni wauguzi wa muda mrefu ambao wamekuwa wakifanya kzi katika kitengo hiki cha upasuaji na asubuhi hii waliotakiwa kuanza maandalizi kwa ajili ya operesheni ya Mzee Albano iliyotarajiwa kufanyika usiku wa siku hiyo.
Baada ya kushuka garini wakaelekea moja kwa moja katika chumba alimolazwa mzee Albano.Dr Zakaria akakinyonga kitasa na mlango ukafunguka.Walitegemea kumkuta Dr Anna maria asubuhi hiyo lakini hakuwepo chumbani humo.Kitandani mgonjwa alikuwa amelala akiwa amefunikwa na shuka
“Kaenda wapi Dr Anna Maria? Akauliza Zakaria.
“Labda kaenda kule chini kunywa kahawa.Si unajua Anna maria na kahawa tena”Akajibu Maimuna akiwa katika mavazi yake tayari kwa kuanza shughuli za usafi.
“Ok tusipoteze muda tuchukue vifaa tukaanze usafi mara moja”Akaamuru Zakaria.
Akiwa bado katika chumba cha mzee Albano akiendelea na shughuli za usafi ,Bi Bertha akagundua kuwa mashine ya kumsaidia mgonjwa kupumua haikuwa ikifanya kazi.Akaisogelea ili kuhakiki,ni kweli ilikuwa imezimwa.Akawaita wenzake,wakaisogelea mashine ile na wote wakashangaa na ndipo walipogundua kwamba mashine nyingine zote zilizokuwa zimeunganishwa kwa mzee Albano ili kuisaidia mifumo mbali mbali ya mwili kufany akazi nazo zilikuwa hazifanyi kazi.Wasi wasi ukawaingia wakadhani labda mzee Albano atakuwa amefariki.Kitandani kulikuwa na mgonjwa ambaye alikuwa amefunikwa shuka mwili wote. Zakaria akakaribia kitanda akalifunua shuka.Karibu aanguke kwa mstuko alioupata.Mtu aliyelazwa kitandani pale hakuwa mzee albano.Alkuwa ni mtu mwingine kabisa.Haraka haraka akainua simu na kupiga mapokezi kuulizia kama kuna mabadiliko yoyote yalifanyika usiku kuhusu mzee Albano akajibiwa kuwa hakukuwa na taarifa zozote za mabadiliko.Shughuli zote zilitakiwa ziendelee kama zilivyopangwa. Kijasho kikaanza kumtoka .Akapiga tena simu mapokezi kuulizia kama Dr Anna maria alikwisha toka akaambiwa bado hajatoka.Kitabu cha makabidhiano kinaonyesha kwamba alikuwa bado hajakabidhi mgonjwa. Zakaria akazidi kuchoka.Akaomba tena Dr Anna Maria atafutwe katika simu yake ya mkononi lakini majibu yakaja kuwa alikuwa hapatikani simuni.Huku moyo ukimwenda mbio zakaria akachukua simu yake na kumpigia Dr Henry.
“Zakaria kuna nini mbona simu asubuhi namna hii? Akauliza Henry baada ya kupokea simu.
“Dr Heny kuna matatizo yametokea.Mzee Albano haonekani humu chumbani mwake.Nipo hapa katika chumba hiki alimokuwa amelazwa lakini kuna mgonjwa mwingine kabisa.Mapokezi wameniambia hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika.Dr Anna Maria naye hayupo hapa na wala hapatikani katika simu yake.Nimepiga simu katika wodi zote ,hakuna wodi hata moja ambayo mzee Albano amepelekwa…….”
“Unasemaje ???????????” akauliza Dr Henry kwa mstuko kubwa.
“Dr Henry, mzee Albano haonekani hapa hospitalini.”
“Haiwezekani…..what happened? Where is he ? Nakuja hapo sasa hivi” Akajibu Dr Henry kwa sauti iliyokuwa ikitetemeka.
Huku kijasho kikimtoka usoni akaamka haraka haraka akiwa bado na nguo za kulalia.Chini ya kitanda akaviona viatu vya wazi ,akavaa akaenda mezani na kuanza kutafuta funguo za gari.Mke wake alimuona namna alivyostuka akaogopa hata kumuuliza kulikoni
“Mama Kelvin nionyeshe funguo za gari langu haraka sana”
Akasema kwa hasira Dr Henry akimuuliza mkewe.Mkewe alikuwa amepigwa na butwaa kutokana na mabadiliko ya ghafla ya mumewe mara tu alipopokea simu ile kwa sababu usiku kucha walikuwa wakijadili kuanzisha miradi mikubwa mikubwa huku Dr Henry akidai kuna pesa nyingi anategemea kuzipata siku si nyingi..
“Baba Kelvin kuna nini kimetokea? Mbona hivyo? Akauliza mke wake.
“Nakwambia nataka funguo za gari langu haraka sana.” akafoka na mara akaziona funguo zilizokuwa zimeanguka chini ya meza akatoka mbio mle chumbani.Akaingia katika gari lake na kuondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea hospitali.Mkewe bado alikuwa akimshangaa.
“Haiwezekani hata kidogo.Mzee Albano hawezi kupotea hivi hivi.Kama ni kweli lazima kuna mchezo mchafu umefanyika hapa.Lazima mpango wetu utakuwa umestukiwa.Ooh Mungu wangu nitafanya nini kama mpango wetu utakuwa umejulikana?Nitauweka wapi uso wangu mimi? Mungu nisaidie jambo hili lisiwe kweli” Akawaza Dr Henry huku akihema kwa nguvu.
Hali ya sintofahamu ilikuwa imetanda
Patrick Charles memorial hospital.Tayari habari za kutoonekana kwa mzee Albano zilikwisha sambaa katika kila kona na watu walikuwa wamesimama katika vikundi vikundi wakijadili jambo hili la kustusha.Ilikuwa vigumu kuamini kuwa katika ulinzi ule mkali uliokuwapo hapo hospitalini mzee Albano angeweza kupotea.Taarifa za kutoonekana kwa mzee Albano tyari zilikwisha fika katika jeshi la polisi na hivyo kuongeza ulinzi huku upekuzi ukiendelea kila chumba.Hakuna gari lililoruhusiwa kuingia wala kutoka hospitalini hapo.Ni magari machache tu ya vikosi vya usalama ndiyo yaliruhusiwa kuingia ndani.Baadhi ya wafanyakazi waliokuwa zamu ya usiku hospitalini hapo walikuwa wakihojiwa na makachero wa polisi ili kufahamu namna tukio lile lilivyotokea.
Gari ya Dr henry ikiwa katika mwendo mkali ikafunga breki za ghafla na kusimama baada ya kuamriwa kufanya hivyo na askari waliokuwa katika kizuizi mita kadhaa kabla ya kulifikia geti la hospitalini hapo.Akashusha kioo na kuwatazama wale askari akiwa na uso wenye wasi wasi mwingi.
“Mimi ndiye daktari mkuu hapa.Nimepata taarifa hizi sasa hivi na ndio maana niko katika haraka namna hii” akajitambulisha
Askari wakamruhusu kupita. Geti likafunguliwa akaingia ndani.Baada ya kushuka garini huku akikimbia, akaelekea moja kwa moja katika chumba alimolazwa mzee Albano.Kitu alichoambiwa kilikuwa cha kweli.Mzee Albano hakuwemo mle chumbani.Nguvu zikamuisha,akahisi miguu ikimtetemeka akaanguka na kupoteza fahamu.
*
*
*
*
Mkuu wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam alikuwa katika kikao cha faragha na timu yake ndogo aliyoiunda ili kufuatilia suala la mzee Albano.Kikosi hiki cha watu sita kiliongozwa na kamishna wa upelelezi kanda maalum Joseph afwilile.Chumba kilikuwa kimya kabisa kila mmoja akisubiri maelekezo toka kwa mkuu wa polisi kanda maalum Barnabas
byagabo
mmoja kati ya makamanda wakakamavu na wakuogopwa.
“kama wote mlivyosikia juu ya tukio lililotokea.” Akafungua kikao kamanda Barnaba.
“Ni tukio lenye utata mkubwa na kwa ufupi tu ni kwamba baada ya mzee huyu kurudishwa toka India kwa maelezo kwamba hataweza kupona,serikali iliamuru apelekwe Patrick Charles memorial hospital ambako angepatiwa matibabu hadi hapo atakapofariki.Lakini Akiwa pale hospitalini kuna daktari bingwa wa ubongo na uti wa mgongo anaitwa Dr Jason akafanya uchunguzi wake na kugundua kuwa kuna uwezekano wa kumfanyia upasuaji mzee Albano na akapona.Familia yake ikaelezwa nao wakakubali baba yao afanyiwe upasuaji huo.Baada tu ya uamuzi ule,wa kumfanyia operesheni mzee Albano likatokea jaribio la kutaka kumuua.Kuna mtu ambaye kwa mujibu wa uchunguzi wetu inaonyesha ni daktari wa pale pale ,alichoma sindano ya sumu katika moja ya chupa za maji aliyokuwa ametundikiwa mzee Albano.kwa bahati nzuri madaktari waliwahi kuiondoa sumu ile mwilini na mzee Albano akawa salama.Usiku huo huo daktari huyo aliyejulikana kama dokta Selemani akakutwa amefariki katika ajali ya gari.Wataalamu wetu bado wanaifanyia uchunguzi wa kina ajali ile ili kuona kama ni ajali iliyopangwa au la.Baada ya kukamilisha uchunguzi wao watatatupa taarifa.Baada ya jaribio lile la kumuua mzee Albano tulilazimika
tuweke ulinzi mkali hapo hospitalini na kuzuia watu wasio wa muhimu kuingia kwenye chumba alimokuwa amelazwa mzee Albano.Waliokuwa wakiruhusiwa ni familia yake na madaktari wachache.” Kamanda Barnabas akanyamaza akawaangalia wajumbe wa kikao kile kwa macho makali halafu akaendelea.
“Jana mchana limetokea tena tukio jingine.Mtoto wa kwanza wa mzee Albano aitwaye Serena gari lake lilishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana na kusababisha kifo cha mtu mmoja.Mtu huyo,kijana mwenye umri wa miaka 23 ambaye amejulikana kuwa ni mkaazi wa Kiwalani ,aitwaye Salum Ahmed alikuwa ni mfanyakazi wa Papaya group na aliambiwa na bosi wake aipeleke ile gari Rosela restaurant ambako binti huyo wa mzee Albano alikuwa akipata chakula akiwa na Dr Jason.Kwa mujibu wa mashuhuda gari lile lilipofika katika geti la kuingilia hapo hotelini ikatokea pikipiki iliyobeba watu wawili na kijana aliyekuwa amepanda nyuma akaanza kuimiminia risasi gari ile ya Serena na kusababisha kifo cha yule kijana aliyekuwa katika ile gari .Asubuhi ya siku ya leo tumepokea taarifa toka hospitalini hapo kuwa mzee Albano haonekani hospitalini.Ametoweka katika mazingira yenye utata sana kwani mzee huyu hana fahamu na kama ametoweka basi lazima kuna mtu au watu waliotoa hapo hospitali.Tumeongeza askari ili kuimarisha ulinzi katika eneo zima la hospitali Mpaka sasa hivi tunavyoongea bado upekuzi unaendelea lakini hakuna dalili zozote za kumpata mzee Albano.Hii inatufanya tuamini kwamba mzee yule ametoroshwa na watu wenye nia mbaya ambao wamekuwa wakijaribu kumuua bila mafanikio.Kutokana na mlolongo huu wa matukio ambayo yote yanahusiana na mzee Albano pamoja
na familia yake moja kwa moja tumeona kuna kila ulazima wa kuunda kikosi kazi kidogo ambacho kitalishughulikia suala hili kwa haraka sana na mwisho wa siku kuhakikisha mzee Albano anapatikana na kuwabaini watu hawa waliofanya kitendo hiki kiovu na kuhatarisha uhai wa mzee huyu .Tunachotakiwa kukifanya kwanza ni kujua mahali alipo mzee Albano na kumuokoa kabla ya watekaji hawa hawajakeleza mpango wao ambao ninaimani wana lengo la kumuua kwa sababu toka mwanzo walikwisha onesha dalili mbaya.Pili ni kupata ukweli wa nini sababu ya wao kumteka mzee Albano.Nini sababu ya kutaka kumuua.Tatu nini sababu ya kutaka kumuua binti wa mzee Albano na hapo hapo
mchunguze kama shambulio lile la gari la Serena lina uhusiano wa moja kwa moja na mzee Albano.Nne wote waliohusika katika mpango wote huu watiwe nguvuni haraka iwezekanavyo”
Kamanda Barnabas akatoa maelekezo kwa kikosi kazi hiki alichokiteua halafu akawaamuru waanze kazi mara moja na wahakikishe wanampata mzee Albano akiwa hai ndani ya kipindi kifupi
TUKUTANE SEHEMU IJAYO………
0 comments:
Post a Comment
Followers
MAHABA
SERENA
BEFORE I DIE
I DIED TO SAVE PRESIDENT
FAIDIKA NA MASIMULIZI
DEATH MESSENGER
CHOMBEZO ZA MASIMULIZI
MISS TANZANIA PART 2
Blog Archieves
April 2014
(57)
About Me
pettysean.blogspot.com
View my complete profile
Total Pageviews
BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU
Powered By
masimulizi
0 comments:
Post a Comment