MASIMULIZI
Saturday, April 26, 2014
BEFORE I DIE SEHEMU YA 22
RIWAYA : BEFORE I DIE
SEHEMU YA 22
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“baba Eddy mimi katu sintaweza kupiga magoti na kumuomba msamaha mtoto wa kumzaa mwenyewe.Innocent aliondoka nyumbani mwenyewe kwa kiburi kabisa na hata kifo cha huyo kahaba wake ni pigo toka kwa Mungu.Ka…” mama yake Inno akasema kwa ukali lakini kabla hajaendelea mbele zaidi Sarah aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma akaingilia kati
“mama si vizuri kutamka maneno hayo.Baba yuko sahihi kwamba tumefanya makosa.Hata wale wasichana wengine Grace na Sabrina tumekuwa tukiwatendea visivyo.Mimi naungana na baba kwamba kuna kila sababu ya kubadilika na kuwa familia yenye upendo mkubwa.Angalia matajiri waliojazana katika msiba ule.Wote waliokuja pale hakuna hata mmoja ambaye anamfahamu Marina.Wote walikuja pale kwa sababu ya roho ya upendo aliyonayo Latoya.Ni binti mdogo mwenye utajiri wa kutisha lakini ana roho nzuri mno na ndiyo sababu akakubali kuubeba msiba wa mtu masikini kama Marina.Kama angekuwa na roho ya kibinafsi na kujivuna kwa utajiri alionao ,wasingejitokeza watu kama wale msibani.” Saraha akamweleza mama yake ambaye alikuwa amenuna ameangalia pembeni.Hakutaka kuongea kitu chochote tena.
ENDELEA………………………………….
Bado picha ya Marina imekuwa inamjia kichwani.Alikumbuka jinsi Marina alivyokuwa akitabasamu na vishimo kuonekana katika mashavu yake.Alikumbuka kicheko chake na sauti yake iliyokuwa inakwaruza kwaruza anapoongea.
“Alikuwa na uzuri wa kipekee ambao mtu unaweza ukautambua kama ukipata bahati ya kukaa naye kwa karibu” akawaza Innocent.
Picha ambayo kila alipokuwa akiikumbuka ilikuwa ikimtoa machozi ni ile ambayo Marina alikwa ametulia tuli katika jeneza .
“Ukurasa wa Marina ninaufunga rasmi.Nitamuombea kila siku ili aweze kupumzika kwa amani huko aliko.Nini kitakachofuata baada ya hapa? Moyo wangu unaniambia kuna kitu ninatakiwa kufanya lakini sielewi ni kitu gani hicho ninachotakiwa kukifanya.Ninajihisi kama nina kazi kubwa ya kufanya baada ya kumpoteza Marina.Ni kazi gani hiyo? Na nini yatakuwa maisha yangu baada ya hapa? “ Innocent akainuka na kukaa Mara sura ya Latoya ikamjia kichwani akatabaasmu
“Binti mzuri,mwenye sura ya kupendeza na kuvutia.Ana uzuri wa ajabu sana.Ana sura kama ya malaika.Uzuri wake unanifanya mara nyingine nihisi labda si binadamu wa kawaida.Ni binti mdogo lakini mwenye mambo makubwa mno.Latoya ni nani?? Kwa nini kila mtu anampa heshima kubwa namna ile.Nimeshuhudia kwa macho yangu jinsi matajiri wakubwa wa nchi hii ninaowafahamu na hata wale nisio wafahamu wakitoa heshima kubwa kwa binti huyu. Anafanya biashara gani kiasi cha kumfanya awe na utajiri mkubwa na kuheshimika namna hii? Vipi kuhusu masuala ya kimahusiano? Yawezekana akawa ameolewa? Kama kaolewa ni kwa nini basi huyo mume wake sijamuona msibani na wala hakugusia jambo lolote kuhusu suala hilo ? Pale msibani alinitambulisha wazazi wake ambao wanaonekana wana umri mkubwa wakati Latoya bado binti mdogo.je inawezekana walimpata Latoya wakita tayari ni wazee? Latoya ana ndugu wengine? Mbona sikuwaona msibani?” Innocent akahisi kuumwa kichwa kwa mawazo yale mengi kuhusiana na Latoya
“Halafu kitu kingine kinachonifanya niwe na udadisi mkubwa kuhusiana na binti huyu ni kwamba kwa nini katika ghorofa hii ya juu anaishi yeye pekee? Wafanyakazi wake wote wanaishi katika ghorofa za chini na toka nimefika hapa sijaona mfanyakazi yeyote akipanda huku ghorofa ya juu.Kulikoni? Swali jingine ninalojiuliza ni kwamba nimeonana naye kwa siku moja tu imetokea nini mpaka akawa karibu na mimi namna hii? Mbona ameniamini kwa kiasi kikubwa kama hiki? Kwa jinsi anavyonijali kila mtu anaamini kwamba mimi ni rafiki yake wa siku nyingi.Kuna kila ulazima wa kuanza kumfahamu Latoya ni nani kwani hata mimi nimeanza kuvutiwa naye,si kwa utajiri alionao lakini nahisi kuna kitu kinaanza kujengeka ndani ya moyo wangu kuhusu Latoya.Kila mara picha ya sura yake ikinijia ninasisimkwa mwili” Akawaza Innocent.
“Nimekumbuka zile namba alizoniambia nimpigie kama nina shida naye nyakati za usiku.Ngoja nimpigie nimwambie kitu chochote kile hata usiku mwema inatosha.Ili kumfahamu vizuri ninatakiwa kuanza kujenga mazoea ya karibu sana naye” akawaza Inno huku akiandika namba alizopewa na Latoya na kupiga.simu ikaita lakini haikupokelewa.Akapiga tena lakini haikupokelewa.
“Inawezekana amelala usingizi mzito sana.Amechoka mno .Ngoja na mimi nilale” akawaza Innocent na kisha akalala
*
*
*
*
Curtis Stevens mtu ambaye kwa miaka kumi na mitano amekuwa balozi wa Tanzania katika nchi za Uholanzi ,Denmark
Ufilipino na Marekani bado alikuwa
amekaa katika sofa sebuleni kwake na pembeni yake kulikuwa na kikombe cha kahawa.Toka amerejea kutoka katika mazishi ya Marina Mr Curtis amekuwa ni mtu mwenye mawazo mengi .
“Curtis ,unawaza nini? Akauliza mke wake .
“Nina mawazo mengi sana kuhusiana na huyu binti yetu Latoya”
“Nimekwisha kuambia Curtis mambo ya Latoya ni mambo magumu sana na sisi kuendelea kumfuatilia ni kupoteza muda wetu bure.Kila siku nimekuwa nikikueleza kuhusiana na suala hili kwamba muda ukifika Latoya mwenyewe atatueleza kuhusiana na maisha yake yenye utata mkubwa” mama yake Latioya akasema
“nakubaliana nawe mke wangu lakini kuna jambo nimejifunza pale msibani.”
“Jambo gani hilo?
“Ni kuhusu uhusiano uliopo baina ya Latoya na yule kijana Innocent.Umeuonaje urafiki wao?
“Kwa mara ya kwanza katika maisha ya Latoya nimeshuhudia akiwa na urafiki wa karibu na kijana wa kiume.Sijawahi kumuona au hata kusikia akiwa na urafiki wa karibu na kijana yeyote kama alionao kwa Yule kijana Innocent.” akasema mzee Curtis..
“Hata mimi nimehisi kama kuna kitu kinaendelea baina yao japokuwa hakiko wazi lakini kama mzazi na mtu ninayemfahamu Latoya vizuri nimekiona kitu hicho.Kwa upande mmoja nimefurahi kwa sababu tunaweza tukamtumia kijana yule katika kuutafuta undani wa Latoya.Kama wazazi hatuwezi kamwe kumuona binti yetu akiwa na utajiri mkubwa kama ule bila kufahamu ni wapi alikoutoa na hataki kusema ameupata wapi utajiri wa namna hii akiwa binti mdogo.Mambo mengi sana yanasemwa kuhusiana na binti yetu.Kama tulivyo sisi wazazi wake ,hakuna anayefahamu
chanzo cha utajiri wake na aina ya maisha anayoyaishi na ndiyo maana kila mmoja anatamka lake.Wengine wanasema kwamba ni mshirika wa imani hii ya freemason ambayo inasemekana watu wanaojiunga na imani hii huwa wanapata utajiri mkubwa sana.Wengine wanadai kwamba pesa yake inatokana na imani za kishirikina ili mradi kila mmoja anatamka maneno yake.Lakini ukweli ninaoufahamu ni kwamba Latoya nimemlea katika misingi imara ya kidini na sina hakika kama anaweza akashiriki katika hayo mambo wanayosema anashiriki.Lakini lisemwalo lipo kwa sababu vijana hawa wa siku hizi wamekuwa na tamaa kubwa ya utajiri wa haraka haraka.Kinachonifanya hata mimi niwe na wasi wasi na Latoya na niamini baadhi ya maneno wanayoyasema watu ni jinsi utajiri wake ulivyokuja ghafla na bila kumueleza mtu yeyote ameupata wapi utajiri ule mkubwa “ akasema Mr Curtis akanyanyua kikombe chake cha kahawa akanywa kidogo na kusema
“Nakumbuka baada ya kumaliza muda wangu kama balozi wa Tanzania nchini Marekani tulimuacha Latoya akiendelea na masomo yake huko huko Marekani.Baada ya mwaka mmoja kupita ndipo alipotueleza kwamba ana mpango wa kufungua biashara hapa Tanzania ingawa hakusema pesa za kuanzisha biashara hiyo amezitoa wapi.Kama utani alianzisha kiwanda cha kutengeneza nguo na baadae biashara zake zikaanza kuongezeka na kuongezeka na ghafla tukasikia kwamba binti yetu amekuwa ni bilionea.Jambo hili si la kufumbia macho mama Latoya tunatakiwa tufahamu ni wapi binti yetu alikoupata utajiri huu mkubwa sana.Ukiachana na maswali hayo kwamba ni wapi alikotoa utajiri huu Latoya amekuwa ni mtu mgumu sana kuweza kuyaweka wazi maisha yake.Maisha yake yametawaliwa na usiri mkubwa sana.Jumba lake kubwa lina watumishi ambao hakuna hata mmoja ambaye amewahi kukiona chumba cha Latoya.Hakuna mfanyakazi anayeruhusiwa kufika katika ghorofa ya juu ambako ndiko anakolala Latoya.Unadhani ni kwa nini amefanya hivi ? Ni wazi kuna kitu anakificha.Kuna siri kubwa anyoificha na ambayo ni lazima tuifahamu.Nafikiri muda umewadia kwa sisi kuupata ukweli kupitia kwa huyu kijana Innocent ambaye anaonekana kuwa karibu sana na Latoya.Inaonekana ni marafiki wakubwa.” Mzee Curtis akamwambia mkewe ambaye alikuwa amekaa kimya akimsikiliza kwa makini
“Curtis nakubaliana nawe kwa yote uliyoyasema.Ni kweli kwamba Latoya ni binti ambaye tumempata kwa shida baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kujaliwa mtoto.Ni mtoto ambaye tulimpata kama muujiza vile kutokana na umri wetu kuwa umekwenda sana kwa maana hiyo tuna kila sababu ya kumchunga kama mboni ya jicho letu japokuwa amekwisha kuwa binti mkubwa sasa.Kusema ukweli utajiri wake unatia mashaka sana .Umekuwa ni utajiri wa ghafla mno kwa binti mdogo kama yeye.Katika umri wake huu mdogo tayari amekuwa billionea kweli nijambo la kushangaza mno.Kinachowashangaza watu ni kwamba sisi wazazi wake tunaishi maisha ya kawaida na wala hatuna utajiri wowote.Suala hili linawafanya watu wajiulize maswali mengi sana kuhusiana na wapi Latoya ameupata utajiri huu mkubwa.Kuna mtu aliwahi kuniambia kwamba alisikia tetesi kwamba eti Latoya anaishi na kiumbe wa ajabu sana chumbani kwake ambaye ndiye anayempatia utajiri huo na ndiyo sababu amekuwa hataki mtu yeyote aingie chumbani kwake.Kila mtu anaongea la kwake.Kuna ulazima wa kuutafuta ukweli kuhusiana na binti yetu.” Akasema mama Latoya
“Kuanzia kesho nitaanza kutafuta namna ya kuweza kuonana na yule kijana Innocent ili niweze kumuomba atusaidie kuupata ukweli halisi kuhusiana na Latoya.Twende tukalale mke wangu .Mambo ya Latoya ni magumu sana .” akasema mzee Curtis huku akiinuka pale sofani na kuongozana na mkewe kwenda kulala.
TUKUTANE TENA SEHEMU IJAYO…………
0 comments:
Post a Comment
Followers
MAHABA
SERENA
BEFORE I DIE
I DIED TO SAVE PRESIDENT
FAIDIKA NA MASIMULIZI
DEATH MESSENGER
CHOMBEZO ZA MASIMULIZI
MISS TANZANIA PART 2
Blog Archieves
April 2014
(57)
About Me
pettysean.blogspot.com
View my complete profile
Total Pageviews
BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU
Powered By
masimulizi
0 comments:
Post a Comment