MASIMULIZI
Tuesday, April 15, 2014
BEFORE I DIE SEHEMU YA 13
RIWAYA : BEFORE I DIE
SEHEMU YA 13
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Hii ndiyo ofisi yetu kaka Innocent karibu sana.” Sabrina akasema huku akimtambulisha Inno kwa wafanyakazi waliokuwa pale ofisini.Innocent hakuificha furaha yake.Kwa muda huu mfupi aliowasili hapa kila mmoja alionekana kuufurahia ucheshi na uchangamfu wa Innocent. Baada ya maongezi na utani wa hapa na pale kama kawaida yake ,Sabrina akamchukua Inno na kumpeleka katika ofisi ya Latoya.
“Dada huyu ndiye Innocent,amekuja kukuona kwa ajili ya lile suala nililokueleza” Sabrina akamtambulisha Innocent kwa
Latoya.Kwa sekunde kadhaa walibaki wanatazamana halafu Latoya akasema
“Karibu sana Innocent,nafurahi kukufahamu” Latoya akasema huku akisimama na kumpa mkono
“Hata mimi nafurahi sana kukufahamu “ Innocent akajibu huku akihisi kama vile macho yake yalikuwa yakimdanganya kwa msichana aliyekuwa mbele yake.
ENDELEA…………………
Alikuwa akitazamana na msichana mwenye umbo dogo,mweupe na mwenye nywele ndefu nzuri na nyeusi.Msichana huyu alikuwa na macho mazuri ya kupendeza yaliyokuwa yamefunikwa na miwani mizuri iliyozidi kumfanya awe mrembo zaidi.Siku ya leo alikuwa amevaa koti refu la rangi nyeusi lililofika hadi mapajani na chini alivaa suruali nyeusi iliyomkaa vyema na kisha akamalizia na viatu virefu vyeusi.Koti lile lililoonekana la gharama kubwa lilikuwa limeachwa wazi hadi sehemu za chini ya kifua na kuifanya fulana nyeusi aliyokuwa ameivaa ndani kuonekana ikiwa imekifunika kifua cheupe na cha kupendeza kilichokuwa kinang’aa kwa cheni nzuri ya dhahabu.
“Nilitegemea Latoya angekuwa ni mama mtu mzima ,lakini kumbe ni binti mdogo tu kama huyu.She looks so pretty.Au ndiye huyu Latoya Bilionea ambaye niwahi kumsikia kwamba ana utajiri mkubwa lakini bado ni binti mdogo?” Akawaza Innocent
“Innocent karibu sana.Mimi naitwa Latoya na ndiye mmiliki wa taasisi hii yenye kuwasaidia wanawake wasiokuwa na uwezo kupata tiba za maradhi mbali mbali yanayowasumbua.Sabrina alinieleza kwamba una mgonjwa anayehitaji msaada wa figo?” Latoya akasema kwa sauti yake laini.
“Ni kweli Latoya .Nina mgonjwa wangu anaitwa Marina yuko hospitali kwa sasa na anahitaji kubadilishiwa figo.” Inno akasema
“Pole sana Innocent.Sasa umefikia wapi kuhusu kupata figo nyingine?? Latoya akauliza
“Mpaka sasa hivi bado sijafanikiwa kupata figo.Nilikuwa naelekea kuonana na mmoja wa rafiki zangu ambaye ni daktari ili nione kama anaweza kunisadia,lakini Sabrina akanipigia simu na kuniambia kwamba ameongea na wewe na umemwambia kwamba nije kuonana nawe.Kwa hiyo mpaka sasa hivi bado hiyo figo haijapatikana”
Latoya akatoa miwani yake akamtazama Innocent na kusema
“Baada ya Sabrina kunieleza niliguswa sana na nikamwambia akutaarifu uje hapa ili tuweze kushauriana nini tufanye kwa sababu kwa bahati mbaya ni kwamba hakuna mahala tunakoweza kununua figo.Inatakiwa apatikane mtu ambaye atakuwa tayari kujitolea figo hiyo kwa ajili ya Marina.Umeshajaribu kuongea na watu mbali mbali kama marafiki,ndugu na jamaa kuhusu mmoja wao kujitolea figo?
“Latoya ,labda kwa kukupa picha halisi ya msichana huyu ni kwamba Marina ni binti mdogo ambaye nilimkuta akifanya biashara ya ukahaba katika moja ya kumbi
za burudani.Nilipomuona nilijikuta nikiguswa sana ,kwanza kwa umri wake na pili kwa ile biashara aliyokuwa akiifanya.Nilifanya jitihada za kuonana naye nikijifanya ni mteja ninayehitaji huduma ya ngono .Tulipokuwa hotelini nilimweleza kuhusu lengo langu la kutaka kumsaidia ili aweze kuondokana na maisha yale yasioendana na umri wake.Alinieleza historia yake.Ni mtoto asiyekuwa na wazazi wala ndugu yeyote hapa mjini.Ndugu yake pekee anayemfahamu alikuwa ni mama yake ambaye alifariki miaka kadhaa iliyopita hivyo kumfanya Marina kujiingiza katika biashara hii ya kuuza mwili ili aweze kuyaendesha maisha yake.Nilifika hadi mahala alikokuwa akiishi na wenzake.kwa kweli wanaishi maisha mabaya sana.Mwanzoni
Marina alikuwa mgumu kukubali kubadilisha aina ya maisha anayoyaishi.Alikwisha kata tamaa na maisha yake.Siku ya pili tangu nimemfahamu nilipigiwa simu na mjumbe wa eneo analoishi Marina kwamba Marina pamoja na wenzake wawili wamekamatwa kwa wizi wa simu ,nilikwenda kumtoa polisi na kulipa vifaa vyote ambavyo yeye na wenzake walikuwa wakituhumiwa kuviiba.Matatizo yalianza baada ya kutoka polisi kwani alianza kuumwa sana ikanibidi kumpeleka hospitali akapata matibabu halafu nikampeleka nyumbani kwetu.Kule nyumbani kwetu mambo hayakuwa mazuri sana ,wazazi hawakupendezwa na kitendo cha mimi kumpeleka Marina akaishi pale.Siku iliyofuata nikiwa kazini nilipigiwa simu kwamba Marina ameondoka nyumbani.Nikaenda tena kumtafuta na kumkuta kule alikokuwa akiishi na wasichana wenzake.Nilimchukua na kumpeleka tena hospitali kwani hakuwa akijisikia vizuri.Baada ya uchunguzi ikagundulika kwamba ana matatizo ya figo kwa hiyo inabidi abadilishiwe figo nyingine.Jana jioni nilirudi naye tena nyumbani lakini ukatokea mtafaruku baina yangu na mama ambaye hakuwa akitaka Marina akae pale nyumbani.Niliumia sana kwa kitendo kile na hivyo ikanilazimu kuondoka nyumbani na kwenda kuchukua chumba katika hoteli.Usiku wa manane hali ya Marina ilibadilika ikanibidi nimkimbize hospitali ambako bado amelazwa hadi sasa.Kwa maana hiyo Marina ni mtu asiye na ndugu wala mtu wa karibu ambaye anaweza akamshughulikia au kuyajali matatizo yake.kwa sasa mtu pekee ambaye anaweza kumuita ndugu ni mimi . Marina anahitaji msaada mkubwa na wa haraka.Kama kuna lolote unaloweza kufanya ili kuaokoa maisha yake tafadhali naomba unisaidie” Innocent akasema.
Maneno yale ya Innocent yalionyesha kumchoma moyo Latoya ambaye alishindwa kujizuia na kutoa chozi.
“Pole sana Innocent kwa matatizo uliyonayo.Ni watu wachache sana wenye moyo wa huruma kama wa kwako.Mimi niliposikia kuhusu mgonjwa wako nikajua labda ni ndugu yako wa karibu au dada yako,lakini kumbe ni mtu ambaye hata humfahamu.Pole sana Inno.Siwezi kuelezea ni jinsi gani nilivyoguswa kwa tatizo hili hadi nimejikuta nikitoa machozi.Innocent taasisi yangu inajihusisha na kutatua matatizo mbali mbali ya wanawake wasiokuwa na msaada.Ninafahamiana na madaktari wengi na hospitali nyingi kubwa ndani na nje ya nchi.Ninachotaka kukifanya ni kufanya mawasiliano nao ili nione namna gani wanaweza wakanisaidia…” Akasema Latoya lakini kabla hajaendelea simu ya Innocent ikaita,akasogea pembeni na kuipokea.Baada ya maongezi yaliyochukua kama dakika mbili hivi sura ya Innocent ikabadilika ghafla.Akajishika kiuno.
“Innocent mbona umebadilika hivyo? Latoya akauliza
“Hospitali wamenipigia simu kwamba hali ya Marina imebadilika na kuwa mbaya zaidi.Latoya ngoja nikimbie nikamuangalie anaendeleaje.I cant let her die…..”
“sawa Innocent ,mimi ninaendelea kuwasiliana na watu mbali mbali ili nione watatusaidia vipi.Wahi hospitali mara moja na lolote nitakalolipata nitakutaarifu mara moja.Usife moyo Innocent tuko pamoja katika suala hili.Chukua hizi namba zangu za simu kwa mawasiliano.Nipigie simu kunifahamisha kuhusu hali ya mgonjwa” Latoya akasema na kwa haraka Innocent akatoka mle ofisini kwake.
Dakika arobaini zilimfikisha Innocent hospitali na moja kwa moja akafululiza hadi katika ofisi ya daktari mkuu ambako alifahamishwa kwamba hali ya Marina ilibadilika ghafla na tayari amehamishiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi akisubiri kubadilishiwa figo ili kuokoa uhai wake.
Innocent akainua kichwa chake akatazama juu akafikiri kwa muda kisha akashusha pumzi ndefu,na kusema
“Daktari hatuwezi kumpoteza Marina kwa ukosefu wa figo.Nitajitolea figo yangu ili Marina apone” Daktari yule akainua kichwa na kumtazama Innocent asiamini kile alichokisikia.Ikambidi amuulize tena kama alimaanisha alichokiongea.Innocent akasisistiza kwamba figo yake moja itolewe na awekewe Marina ili waweze kuokoa uhai wake.Daktari akatoka mle ofisini na kwenda kuwataarifu madaktari wenzake juu ya uamuzi ule wa Inno na kuanza maandalizi ya kuifanya operesheni ile mara moja.Innocent alikuwa amekaa katika sofa la mle ofisini kwa daktari mkuu akiomba Mungu kimoyo moyo na baada ya nusu saa daktari akarejea na kumtaka waongozane.Kabla hajatoka mle ofisini Innocent akakumbuka kitu.Akaitoa simu yake mfukoni na kubonyeza namba za simu za Latoya akampigia.
“Latoya naomba usiendelee tena kutafuta ile figo.Hali ya Marina inaendelea kuwa mbaya kwa hiyo hatutakuwa na muda mwingi wa kusubiri figo hiyo ipatikane.Nimeamua kujitolea mimi mwenyewe figo yangu ili kuokoa uhai wa Marina.Nashukuru sana kwa msaada wako na samahani kwa usumbufu niliokusababishia”
Latoya akavuta pumzi ndefu na kusema
“Innocent nashukuru kama umeamua wewe mwenyewe kujitolea figo kwa ajili ya Marina.Naomba ufute kabisa wazo kwamba umenisumbua.Hukunisumbua kitu chochote na niliamua kujitolea kwa moyo wangu wote kusaidiana nawe katika tatizo hili.Innocent nakosa maneno ya kusema kwa sababu sijawahi kukutana na kijana mwenye roho ya huruma kama ya kwako.Kutokana na umuhimu wa suala hili
naahirisha shughuli zangu zote na ninakuja huko hospitali kuungana nawe.Innocent tuko pamoja katika hili.” Latoya akaongea kwa sauti ya upole yenye kuonyesha uchungu ndani yake
“Nashukuru sana Latoya kwa kunipa moyo.Tafadhali naomba umtaarifu na Sabrina ili afahamu kinachoendelea Kwa sasa.yeye na Grace ndio watu pekee ambao naweza kusema kwamba ni familia yangu iliyobaki baada ya familia yangu kunitenga.Latoya I need to go now.See you later” Innocent akakata simu na kuizima kabisa kisha akaongozana na madkatari wawili waliokuwa wakimsubiri amalize kuongea na simu akapelekwa moja kwa moja hadi katika chumba maalum akatoa mavazi yake na kuvishwa mavazi mengine ya hospitali kisha akaingizwa katika chumba kimoja chenye mitambo mingi akalazwa juu ya kitanda.Mashine moja iliyokuwa juu ikaanza kushuka taratibu huku wale madaktari wakiangalia katika luninga zilizokuwemo mle ndani.mashine ile ikashuka hadi karibu kabisa na tumbo na kisha ikawaka taa.Dakika kumi baadae mwanga ule ukazima na mashine ile ikarudi tena juu.madkatari wakajadiliana na wakaendelea kuchunguza mambo mengine kama vile damu n.k.
“Innocent tumeliangalia figo lako na kuona linafaa kuwekwa kwa Marina kwa hiyo kama bado haujabadili mawazo tunaanza kufanya maandalizi ya operesheni hii ya figo.”
“Thank you God.Nilikuwa na wasi wasi sana kama figo yangu ingeonekana haifai kuwekewa Marina.Daktari nimedhamiria kuokoa maisha ya Marina kwa hiyo tusipoteze wakati,mimi niko tayari kwa operesheni hiyo.” Innocent akasema
Madkatari wale wakaondoka katika chumba kile na kumuacha Innocent pale kitandani.Baada ya dakika kumi na tano akaingia muuguzi wa kike na kumuomba Innocent apande juu ya kitanda cha magurudumu kwa ajili ya kupelekwa katika chumba cha upasuaji.Huku akitabasamu Innocent akapanda juu ya kile kitanda cha magurudumu halafu muuguzi akaanza kukisukuma na kutoka ndani ya kile chumba.Moja kwa moja akapelekwa hadi katika mlango wa chumba cha upasuaji.Mlango ukafunguliwa na akaingizwa ndani.Katika chumba cha kwanza ambacho hakikuwa na vitu vingi akatokea daktari mmoja ambaye akamtazama na kumwambia.
“Innocent upasuaji tunaoenda kuufanya ni mkubwa na kabla hatujakuingiza katika chumba cha upasuaji ,una mtu yeyote ambaye ungependa kuwasiliana naye?
Inno akafikiri kwa sekunde kadhaa na kusema
“Nashukuru daktari lakini watu wangu wa muhimu tayari nimekwisha wasiliana nao.Mnaweza kuendelea na taratibu za upasuaji Innocent akasema na kisha daktari akaruhusu aingizwe katika chumba cha upasuaji.
TUKUTANE TENA SEHEMU IJAYO……..
KWA SIMULIZI ZAIDI TEMBELEA HAPA MASIMULIZI
0 comments:
Post a Comment
Followers
MAHABA
SERENA
BEFORE I DIE
I DIED TO SAVE PRESIDENT
FAIDIKA NA MASIMULIZI
DEATH MESSENGER
CHOMBEZO ZA MASIMULIZI
MISS TANZANIA PART 2
Blog Archieves
April 2014
(57)
About Me
pettysean.blogspot.com
View my complete profile
Total Pageviews
728,271
BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU
Powered By
masimulizi
0 comments:
Post a Comment