MASIMULIZI
Tuesday, April 1, 2014
" BEFORE I DIE " SEHEMU YA 1
Ni Edson Benard pekee ambaye hakuungana na familia yao jioni hii ya katika mapokezi ya mdogo wake Innocent anayerejea nyumbani baada ya kuhitimu shahada ya kwanza ya uchumi na fedha katika chuo kikuu cha Columbia jijini New york Marekani.
Mzee Vincent Benard akiwa ameongozana na mkewe Bi Gloria Benard pamoja na binti yao Sarah walijawa na nyuso za furaha
kwa kumpokea tena mtoto wao kipenzi Innocent ambaye ni mtoto wa tatu na wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto watatu ambao bwana na bi Vincent Bernard walijaliwa kuwapata.Mtoto wa kwanza kuzaliwa alikuwa ni Edson ambaye kwa sasa ni mfanya kazi katika shirika moja lisilokuwa la kiserikali linaloshughulika na masuala ya elimu ya ukimwi kwa umma.Wa pili ni Sarah ambaye ni mwandishi wa habari katika televisheni ya Taifa na wa mwisho ni Innocent ambaye leo hii anarejea nyumbani akitokea Marekani baada ya kuhitimu shahada yake ya kwanza ya uchumi na fedha katika chuo kikuu cha Columbia.Familia hii ni moja ya familia ambazo tunaweza kusema kuwa ni familia bora zenye kujiweza kiuchumi.Mzee Vincent alimiliki kiwanda cha kutengeneza magodoro na kiwanda cha kutengeneza maji ya kunywa. vile vile alikuwa na hisa za kutosha katika viwanda kadhaa kikiwemo kiwanda cha sigara na saruji.
Ni vigumu kuelezea furaha waliyoipata baada ya Innocent kutokeza katika sehemu ya kusubiria wageni.Walimkumbatia kwa furaha na kumkaribisha tena nyumbani.Innocent au Inno kama walivyozoea kumwita hakukaukiwa tabasamu kama ilivyo kawaida yake.Ilikuwa ni furaha ilioje kuwasili tena nyumbani baada ya miaka kadhaa ya kuwa mbali na nyumbani.
“Karibu tena nyumbani mwanangu” Mzee Vincent akasema
“Ahsante baba nimeshakaribia.Mbona kaka Edson simuoni hapa? Nilifikiri mtakuwa naye.” Inno akasema
“Edson amepata safari ya dharura kwenda mikoani katika shughuli zao,ila alipenda sana kuungana nasi kuja kukupokea.” mama yake akasema
Saraha akamsaidia Inno kusukuma mabegi yake hadi katika gari lao halafu wote wakaingia garini na kuondoka kuelekea nyumbani.
“Ama kweli Marekani kuzuri.Inno umebadilika.Umependeza sana mdogo wangu” Sarah akasema huku akicheka kwa furaha.Innocent kijana asiyekaukiwa tabasamu akajibu.
“Na wewe Sarah bado hujaacha utani wako tu.”
“Siongei utani.Ni kweli kabisa umependeza sana mdogo wangu.Inaonekana hali ya huko imekukubali.Halafu mimi nikafikiri utakuja na wifi mzungu”
Wote mle ndani ya gari wakaangua kicheko kikubwa kwa utani ule wa Sara.
“Huyo mzungu nitampeleka wapi? Unafikiri mzee Vincent atakubali mwanae aoe mzungu na kuacha wasichana warembo wenye maadili ya kiafrika? Thubutu! “ Inno akaendeleza utani na kumfanya mzee Vincent acheke kwa nguvu.
“Ndiyo maana nakupenda mwanangu.Hapo umenena.Sioni sababu ya kuacha mamilioni ya mabinti warembo wa kiafrika wenye sifa na maadili ya kiafrika na kwenda kuoa mtu wa mbali ambaye hayuko tayari kufuata mila na desturi zetu.Hebu muangalieni mama yenu jinsi alivyo mzuri,ule uzuri asilia wa kiafrika.Ana umbo la mwanamke wa kiafrika.Sura pana yenye weusi wa kung’aa,macho makubwa yenye kurembua,miguu ambayo nyie vijana mnaiita ya bia” Kicheko kikubwa kikaanguka ndani ya gari.
“lakini baba hizi ni zama za utandawazi.Haijalishi ni mtu wa namna gani unahitaji kumuoa au kuolewa naye .Kitu cha msingi muwe mnapendana kwa dhati” Sarah akasema
“Sikatai mwanangu.Hayo unayosema ni ya kweli.Lakini pamoja na hayo ni lazima tuendelee kulinda mila na desturi zetu sisi kama waafrika.Iwapo utapata bwana wa kizungu ni wazi hautauthamini utamaduni wako tena.Malezi,makuzi ya wenzetu ni tofauti na sisi.Hebu angalia kwa sasa sijui wanashinikiza dunia nzima ihalalishe hivi vitendo vichafu visivyompendeza Mungu ambavyo ni kinyume na maadili yetu ya kiafrika.Siwakatazi na wala siwaingilii katika masuala yenu ya mahusiano lakini nisingependa mwanangu yeyote aoe au kuolewa na mtu wa mataifa ya kigeni na hasa huko Ulaya na marekani.Nitafurahi sana kama wanangu wote wataoa na kuolewa humu humu ndani ya nchi yao.”
Maongezi yalikuwa matamu na hatimaye wakajikuta wamewasili nyumbani.Giza tayari likwishatanda.Mabegi ya Innocent yakashushwa na kupelekwa ndani halafu kwa furaha kubwa Inno akakaribishwa ndani.
“Karibu nyumbani mwanangu” akasema mama yake.
“Nimeshakaribia mama.Hivi yule mbwa wangu Pura bado yupo? Inno akauliza
“Mbwa wako bado yuko tena anazidi kunawiri siku hizi.”
“Mama siwezi kuingia ndani hadi kwanza nikamsalimu Pura.Nimemnunulia sabuni nzuri ya kuogea.”
“ahahahahaaaa..mambo ya wazungu hayo yaani hadi mbwa unamnunulia sabuni ya kuogea! “ mama yake akasema huku akicheka.
“mama nampenda sana mbwa wangu ndiyo maana nikaona ni bora naye nimletee zawadi”
Innocent akaelekea katika banda la kufugia mbwa anakokaa mbwa wake ampendaye sana Pura.Japokuwa ilipita miaka takribani sita lakini mara moja Pura alimfahamu Inno akamchangamkia na kumrukia kwa furaha.Baada ya kuhakikisha mbwa wake yuko salama na mwenye afya njema akaufunga mlango na kurudi ndani.
“Shikamoo kaka” Innocent akasalimiwa na dada mmoja mwembamba mrefu wastani aliyejifunga kitambaa kichwani aliyekuwa amesimama hapo sebuleni akiwa na sinia la kubebea vinywaji alivyokuwa amewapelekea Bwana na Bi Benard.
“Maharaba dada yangu,habari za hapa? Innocent akajibu huku akitabasamu na kumuangalia yule dada ambaye hakumuacha pale nyumbani wakati anaondoka kuelekea Marekani kwa masomo.
“Habari za hapa nzuri,pole na safari”
“Nimeshapoa” Innocent akajibu huku akiunyoosha mkono ili asalimiane na yule dada.
“wewe Grace hebu haraka nenda kamuandalie Innocent maji ya kuoga halafu mwambie na Grace muanze kuandaa meza haraka .” Ilikuwa ni sauti ya amri ya mama yake Inno
Binti yule akaondoka haraka baada ya kupokea amri ile.Innocent akamgeukia mama yake na kumtazama kwa mshangao.
“Innocent , wakati unaondoka hapa nyumbani kwenda masomoni hukuacha msichana wa kazi hapa ndani lakini kwa sasa kuna wasichana wawili tunaishi nao.Mmoja ni huyu Grace ambaye ametoka hapa sasa hivi ambaye ni binti tuliyemchukua atusaidie kazi za hapa nyumbani kama unavyojua baada ya Sarah kuanza kazi katika televisheni ya Taifa mama yako alizidiwa sana na kazi.Mwingine anaitwa Sabrina, yeye alikuwa ni mtoto wa Michael yule mfanyakazi wetu wa shambani ambaye nilikutaarifu katika simu kuwa alifariki dunia.Kwa kuwa niliishi naye vizuri sana yule bwana nikaona ni bora nimchukue binti yake wa pekee niishi naye hapa kwa sababu alihitaji uangalizi maalum kwani ni mlemavu wa ngozi yaani albino”Mzee Vincent akamfahamisha mwanae Inno.
“Ouh ! nafurahi kusikia hivyo baba.Unajua ni vizuri kuwa na familia kubwa .Familia inapokuwa na mchanganyiko mkubwa wa watu basi inakuwa na furaha zaidi.” Innocent akasema
Mrs Benard alikuwa amefura kwa hasira wakati mumewe akimfahamisha Innocent kuhusu wasichana wawili wanaoishi nao mle ndani.
“Nakwambia baba Eddy waondoe hawa wasichana humu mwangu,sitaki mwanangu akaribiane nao kabisa.Usipowatoa mimi nitawaondoa kwa nguvu” Akasema kwa hasira
“kwani mama kuna tatizo gani kuishi nao katika jumba hili kubwa? Innocent akauliza
“Baba yako ametuletea balaa humu ndani.Kaenda kamleta yule albino humu ndani.Hajui kama watu wale wana mikosi.halafu huyu mwingine ni muathirika wa ukimwi .Huoni kama nyumba yetu imeingiliwa? Mwanangu naomba ukae mbali nao kabisa hawa wasichana.”
Innocent akabaki mdomo wazi akishangaa
“mama ! kumbe hilo ndilo tatizo ? Mimi nilidhani labda ni tatizo kubwa lakini kama ni hilo tu basi hakuna tatizo lolote katika kuishi nao.Mzee Michael alikuwa ni kama ndugu yetu aliyekuwa akitulimia na kutulindia shamba letu kwa hiyo kukaa na binti yake hapa tena ambaye anahitaji uangalizi maalum ni jambo la busara sana.Tunahitaji kumuenzi yule mzee.Tunahitaji kumtunza mtoto wake bila ubaguzi wowote.Japokuwa ametoka katika familia ya kimasikini tofauti na sisi lakini hakuna sababu yoyote ya kumtenga.na hata huyu Grace ambaye unadai ameathirika na ugonjwa wa ukimwi,hatuna budi kumtunza na kumlea.Kuathirika na ugonjwa huu si sababu ya kunyanyapaliwa au kutengwa.Mama naomba tuwaonyeshe upendo wajisikie kama ni sehemu ya familia hii”
Innocent akasema na mara Grace akaingia mle sebuleni
“kaka maji ya kuoga tayari.”
“Ahsante Grace” Innocent akajibu huku akitabasamu na kumfanya mama yake anune.
“Nenda kaoge mwanangu tuje tujumuike pamoja kwa chakula cha usiku tufurahie kurejea kwako” mzee Vincent akasema
Innocent akaelekea chumbani kwake akabadili nguo na kwenda kuoga .Kisha oga akarudi tena sebuleni kujumuika na familia yake kwa chakula cha usiku.
“Mwanangu nimekuandalia sherehe kubwa ya kukukaribisha nyumbani jumamosi ijayo..”mzee Vincent akasema
“Nashukuru sana baba.Lakini sioni kama kuna umuhimu wa kufanya sherehe yoyote kwa ajili ya kurudi nyumbani na kutumia fedha nyingi wakati kuna maelfu ya watu wanazihitaji fedha hizo kwa ajili ya elimu ya watoto wao,wengine matibabu n.k.”
Huku akitabasamu Mzee Vincent akajibu
“mwanangu nalifahamu hilo.nafahamu una moyo wa kusaidia wengine toka ukiwa mdogo.lakini kuna kitu ninataka kukifanya siku hiyo ya jumamosi na ndiyo maana nikaamua kuandaa sherehe hiyo .”
“hakuna shida baba,nilikuwa najaribu tu kukumbusha kwamba tunapotumia fedha kwa mambo yasiyo ya lazima tukumbuke kuna watu masikini wanasumbuka usiku na mchana kutafuta fedha kama hizo kwa ajili ya mahitaji yao muhimu.Halafu mbona akina Grace siwaoni hapa?
Sarah na mama yake wakatazamana halafu Sarah akajibu
“Wana chakula chao jikoni”
“Ina maana wao hawajumuiki nasi hapa mezani? Innocent akauliza
“wao wanakula jikoni” mama yake akajibu
“No ! That’s not fair.Waiteni wajumuike nasi hapa,nao ni
sehemu ya familia.” Innocent akasisitiza
“Waende wapi? Wao chakula chao kiko jikoni.Kwani kuna tatizo gani?
Mama yake akasema kwa sauti yenye ukali kidogo ndani yake.
Innocent hakujibu kitu akachukua chakula katika sahani yake akainuka na kuelekea jikoni.
“jamani .mbona hamji kujumuika nasi kule mezani?” Innocent akawauliza grace na Grace waliokuwa wamekaa wakipata chakula jikoni.
“Sisi chakula chetu huwa kinabaki huku jikoni.Haturuhusiwi kukaa mezani na mama” Grace akajibu.
Innocent akatabasamu kama kawaida yake akamsogelea Sabrina na kumpa mkono.
“Naitwa Innocent.Sidhani kama unanikumbuka kwa sababu mara ya mwisho kukuona ulikuwa mdogo nadhani ulikuwa darasa la nne au la tano.Pole sana kwa msiba wa mzee .Mzee Michael nilikuwa namchukulia kama baba yangu na nilikuwa naelewana naye sana.” Innocent akasema na kumfanya Sabrina atokwe na machozi huku akimshangaa .Toka amekuja katika nyumba ile hakuna hata siku moja ambayo ameweza kuongea na mtu wa familia hii zaidi ya mzee Vincent kwa upole na heshima ya ajabu namna hii.Siku zote imekuwa ni kugombezwa na kufokewa.
“nyamaza kulia Sabrina.Ni kazi ya Mungu ambayo sisi wanadamu hatuna budi kuikubali.” Innocent akambembeleza.Sabrina hakuwa akilia kwa sababu ya kukumbushwa kifo
cha baba yake bali kwa jinsi Innocent alivyomsalimia na kuongea naye kwa upole na ucheshi huku macho na sauti yake vikionyesha upendo wa hali ya juu.
Sabrina akafuta machozi na kumtazama Inno usoni.
“Ahsante sana kaka Innocent.Pole na safari”
“Nimekwisha poa.Nashukuru Mungu baada ya miaka sita sasa nimerudi nyumbani.Nadhani tutaendelea kuwa wote hapa kwa sababu sifikirii tena kwenda kusoma nje ya nchi labda hapo baadae sana.”
“kaka Innocent kuna kitu umekuja kuchukua huku jikoni?
Grace akauliza baada ya kuona Inno hakuwa na dalili za kuondoka mle jikoni.
“hapana Grace nimekuja huku tule wote. mimi sijazoea kukaa mezani na kula bila maongezi .Kule mezani tunakula kimya kimya na hata mkiongea ni kuhusu maisha binafsi.Mimi nataka kula kwa uhuru halafu nahisi chakula cha huku ni kitamu kuliko hata cha kule mezani” Innocent akasema na kuwafanya Grace na grace waangue kicheko kinachosikika hadi sebuleni na kumfanya Mrs Benard kutoka haraka na kuja
kuangalia.Alipoingia jikoni akakuta Innocent amekaa na akina Grace wakiongea na kucheka kwa furaha.Mara tu alipoingia maongezi na vicheko vikakoma.Mrs benard akaukunja uso na kusonya kwa hasira halafu akaondoka.
“Msijali sana,mama yangu ndivyo alivyo.Jitahidini kumzoea na kumvumilia” Innocent akasema na kuwafanya grace na Grace kutabasamu.
“I have to change things here.Ni lazima niwasaidie wasichana hawa masikini ili wawe na maisha mazuri na yenye furaha kama tulivyo sisi.Najua wana wakati mgumu sana kuishi na mama yangu.Ninamfahamu mama yangu vizuri.Hana roho nzuri.Nitafanya kila niwezalo kuwasaidia.
Baada ya kula chakula wakaendelea na maongezi yaliyotawaliwa na utani na vicheko.Laiti kama ungewakuta wakiongea ungedhani labda ni watu waliokaa pamoja zaidi ya miaka kumi kumbe ni leo tu wameonana.Wakati wakiendelea na maongezi yao jikoni ghafla Sarah akaingia.
“ Grace mnacheka huku wakati kule tumemaliza kula chakula.Hebu nenda kaondoe vyombo haraka .Na wewe Sabrina kwa nini usianze kuosha vyombo .Inuka mara moja uanze kazi.” Sarah akasema kwa ukali.
“Sawa dada Sarah” Grace akasema na kuondoka haraka kuelekea sebuleni kukusanya vyombo walivyolia chakula.
Baada ya Grace na Sabrina kuondoka mle jikoni Sarah akamuangalia Innocent kwa macho makali .
“Vipi kuna tatizo? Mbona unaniangalia hivyo? Innocent akauliza
“Yes lipo tatizo.Hebu acha uzungu uzungu wako uliotoka nao Marekani.Hawa wasichana huwa hawachangamani na sisi hata siku moja.Tena usijaribu kuwaozea”
Huku akicheka kichini chini Innocent akasema
“Sister mnavyofanya si vizuri.Hawa ni binadamu na isitoshe wana matatizo.Tunatakiwa tuishi nao kwa upendo mkubwa.Ikiwa tutaanza kuwanyanyapaa haitapendeza” Mara Grace akaingia mle jikoni akiwa na sinia la vyombo.Innocent akamshika mkono dada yake wakatoka.
******************************
Mlio wa saa ya ukutani ndio ulimstua toka katika usingizi mzito.Akafunua shuka na kuangalia saa.Ilikuwa ni saa mbili za asubuhi.
“Leo nimelala usingizi ambao sijaulala kwa miaka kadhaa.Kweli nyumbani ni nyumbani.” Akawaza Innocent huku akijinyoosha nyoosha pale kitandani.
“Ngoja niendelee kulala kidogo mpaka saa tatu ndio niamke. No ! I have to wash Pura” haraka haraka akainuka akavaa na kutoka nje.Kabla hajafunga mlango akasikia kelele za kufoka.Mama yake alikuwa akifoka maeneo ya jikoni.Taratibu akapiga hatua na kuelekea huko.
“Nimekwambia mwaka huu ni lazima utaondoka tu.Sitaki uiambukize familia yangu maradhi yako.Na kama baba Edson hataki kukuondoa humu ndani nitahama na kumuachia nyumba.Siwezi kuishi na mwathirika wa ukimwi ndani mwangu” mama yake Innocent alikuwa akimfokea Grace.Maneno yale yakamchoma sana Inno na hasa pale alipomuona Grace ameinama chini akilia na pembeni yake kukiwa na sahani ya udongo iliyovunjika.Huruma ikamwingia .
“Tena naomba usinililie hapa.Inuka sasa hivi ukaendelee na kazi.Na sahani yangu uliyoivunja utailipa” Mrs Benard akaendelea kufoka kwa nguvu.
“mama its enough” Innocent akaingilia kati.Mama yake akasimama na kumuangalia kwa macho makali.
“Mama kwa nini unawafanya hivi ? this isn’t right.Hawa ni wenzetu na ni lazima tuwapende na kuwaona ni sehemu ya familia yetu.” Innocent akasema huku akiinama na kuushika mkono wa Grace akamwinua
“Inuka Grace.” Akamshika mkono na kumpeleka chumbani kwake.
“Hebu pumzika kwanza humu chumbani kwako hadi baadae.halafu usilie sana utaumwa na kichwa.Mama yangu ndivyo alivyo.Unatakiwa uwe mvumilivu sana kuishi naye”
“kaka Innocent mimi nimevumilia lakini sasa naona nimeshindwa.Mama kila siku ananitukana kupita maelezo.Au kwa vile sina wazazi? Grace akasema kwa uchungu huku akilia.
“hapana usiseme hivyo Grace.Namfahamu mama yangu ni mkorofi sana.Nitaongea na baba ili tuone tutafanya nini kuwasaidia wewe na Sabrina”
“Kaka Innocent kwa mateso ninayoyapata katika hii nyumba ni bora niende nikateseke mtaani.Ninachoomba niombee nauli kwa baba ili niondoke hapa na kwenda kokote kule nikaishi.”
Grace akaendelea kulalamika huku uso wake umejaa machozi.Aliongea toka moyoni.Ni wazi alikuwa ameumia mno na maneno aliyoambiwa na Mrs benard.
“hapana usiseme hivyo Grace.Hautaenda sehemu yoyote ile,wewe utaishi katika nyumba hii miaka yote.Jihesabu ni mmoja kati ya wana familia hii.Naomba futa kabisa mawazo ya kuondoka katika nyumba hii.Kama walikuwa wakiwanyanyasa na kuwadharau ni wakati sipo.lakini kwa sasa hakuna mtu atakayethubutu kufanya hivyo tena nikiwa hapa nyumbani.Pumzika Grace tutaongea baadae”
Innocent akatoka mle chumbani kwa Grace na mara akakutana na mama yake akiwa amefura hasira.
“Naona sasa wamepata mwokozi wao” akasema Mrs Benard kwa dhihaka.
“Mama naomba niwe wazi.Mnavyowatendea hawa wasichana si vizuri.”
Mama yake hakujibu kitu akaondoka zake.Innocent akelekea katika banda anamolala mbwa wake Pura akamtoa na kumuogesha halafu akarudi ndani akaoga akapata chai na kuamua kwenda kupumzika bustanini..Akiwa pale bustanini mara Grace akatokea.
“Ouh Grace karibu”
“kaka Innocent samahani kwa kukusumbua.Nimekuja kukuuliza kama una nguo za kufua nikakufulie.”
Huku akitabasamu ,Inno akajibu.
“Grace nashukuru lakini nitazifua mwenyewe.Tafadhali pata muda wa kupumzika”
“Usijali kaka Innocent.Kama zipo nipe nikufulie kwani mama alisema tuchukue nguo zako tufue pia”
“Ina maana hata Sarah huwa mnafua nguo zake? Inno akauliza
“Ndiyo.Hata nguo za dada Sarah pia huwa tunafua.”
Innocent akakaa kimya halafu akasema.
“Grace nenda tu kapumzike.Nina nguo chache lakini nitazifua kesho mimi mwenyewe”
Grace akaondoka na kumwacha Innocent peke yake bustanini.
“Wasichana hawa wanatumikishwa namna hii kiasi kwamba hawana hata muda wa kupumzika na bado wanaendelea kunyanyaswa na kubaguliwa.I must stop this”
**********************************
Ni siku ya nne tangu Innocent arudi toka Marekani .Siku hii ya Jumamosi baba yake alikuwa amemuahidi kumfanyia sherehe ya kumkaribisha tena nyumbani.Ni sherehe iliyoandaliwa kwa siri japokuwa yeye Innocent alidokezwa kuwa itakuwa ni sherehe ndogo tu yenye kujumuisha watu wachache.
Saa kumi na mbili za jioni akiwa ndani ya suti nzuri nyeusi akaongozana na baba na mama yake pamoja na dada yake Sarah wakaingia garini na kuondoka kuelekea mahala inakofanyikia sherehe.
Lamona palace ni ukumbi mkubwa
na wa kisasa kwa ajili ya semina hafla na sherehe mbali mbali.Ni katika ukumbi huu sherehe ya kumkaribisha nyumbani Innocent inafanyikia.Tayari wageni waalikwa wamekwisha wasili na waliokuwa wakisubiriwa ni Mr benard na familia yake.Mara tu walipoingia ukumbini ukumbi wote ukalipuka kwa makofi na vigere gere.Innocent akapatwa na mshangao mkubwa.Hakutegemea kama sherehe ya kukaribishwa kwake nyumbani ingekuwa kubwa namna ile.alitegemea sherehe ndogo yenye watu wachache lakini kwa umati alioukuta mle ukumbini akasimama
na kushika mdomo wake kwa mshangao.Alihisi kuishiwa nguvu .Huku akitabasamu Mr Benard akamshika mkono na kumuongoza kuelekea meza kuu iliyoandaliwa maalum kwa ajili yao.
Sherehe ikafunguliwa na watu wakaanza kuburudika kwa vinywaji na ndipo Mr benard alipopewa nafasi ya kuongea.
“Ndugu zangu,wageni waalikwa,mabibi na mabwana.Nakosa neno kubwa la kuwashukuru kwa kuacha shughuli zenu leo hii na kuja kuungana na familia yangu katika sherehe hii ya kumkaribisha nyumbani kijana wetu Innocent aliyekuwa akisoma nchini Marekani.Ujio wenu jioni hii ya leo unaonesha ni jinsi gani mlivyotuthamini sisi kama familia.Tunasema Ahsanteni sana.Sina mambo mengi sana ya kusema kwani mengi yamekwisha semwa ila ningependa nitumie nafasi hii kutangaza jambo moja kwenu wote.”
Ukumbi wote ukakaa kimya kabisa kumsikiliza mzee huyu.
“Si kitu cha kuficha kuwa kwa sasa mimi na mke wangu umri umesogea sana na kwa maana hiyo tunahitaji muda mwingi zaidi wa kupumzika baada ya kazi ngumu tuliyokwisha ifanya kwa miaka mingi.Nimekuwa na majukumu ya kusimamia miradi na kampuni zote zilizoko chini ya familia yangu.Napenda nikiri kuwa hii ni kazi ngumu na bila usaidizi wa karibu basi hakuna ufanisi utakaopatikana.Ninachotaka kukisema hapa ni kwamba kutokana na kuzidiwa mno na majukumu na hivyo kukosa hata muda wa kupumzika,nimeonelea niyagawe majukumu ili walau nipate wasaa wa kupumua.Napenda sasa nitamke kuwa kampuni ya kutengeneza maji ya kunywa ya Benardo ambayo kwa siku za hivi karibuni ufanisi wake umeshuka sana kwa sasa itakuwa chini ya usimamizi wa kijana wangu Innocent benard.”
Ukumbi wote ukalipuka kwa kelele za kushangilia.
Hizi zilikuwa ni habari njema mno kwa wafanyakazi wote wa kampuni hii.Kampuni hii ilikuwa ikiyumba baada ya kukosa usimamizi thabiti.Kupata meneja mpya tena kijana msomi kama Innocent ilikuwa ni faraja kubwa sana kwa wafanyakazi waliokuwa wana wasiwasi na ajira zao iwapo ingetokea kampuni ile kufungwa.
Innocent akapatwa na mstuko mkubwa.Hakuwa ametegemea kama angeweza kupewa kampuni kubwa kama ile aisimamie.Alipomaliza masomo yake nchini Marekani angeweza kubaki na kufanya kazi huko lakini alitambua umuhimu wa kurudi nyumbani na kusimamia miradi ya familia.Aliinama na kushika kichwa kwa mshangao.Kwa jinsi watu walivyoshangilia walizidi kumchanganya akili kwani japokuwa hawamjui lakini walionekana kuwa na imani na matumaini makubwa kwake ndiyo maana walifurahi na kushangilia
Baada ya Mr benard kumaliza kuongea akamkaribisha Innocent aweze kuwasalimu wageni na kuongea machache.Ukumbi wote ukawa kimya kumsikiliza .Huku akitabasamu akaanza kwa kusema
“Ndugu wageni waalikwa mabibi na mabwana ,nakosa neno la kuweza kuelezea furaha yangu kwa makaribisho haya makubwa.Sikutegemea kama ningeweza kupata makaribisho makubwa kama haya.Kitu kimoja ninachoweza kukisema toka moyoni mwangu ni Ahsanteni sana kwa kuja katika sherehe hii.Kuna msemo usemao nyumbani ni nyumbani na mkataa kwako mtumwa.Ni kwa kuzingatia misemo hii ndiyo maana nikachagua kurudi na kuishi nyumbani Tanzania badala ya kuishi
na kufanya kazi katika nchi za kigeni.Nimerudi nyumbani kusaidiana na watanzania wenzangu katika kuijenga nchi yetu,kuinua uchumi wetu.Nitatumia ujuzi na maarifa yote niliyoyapata katika kuhakikisha tunapiga hatua kimaendeleo. Japokuwa hapa si mahala pake kulisema hili lakini kwa wale ndugu zangu wa kampuni nitakayokuja kuisimamia,naomba niseme kuwa muwe na amani na ninaahidi kushirikiana nanyi kwa moyo mmoja kwa manufaa ya kampuni yetu,jamii na nchi yetu kwa ujumla.Mabibi na mabwana sina cha kuongezea zaidi ya kuwashukuru sana kwa kuja kwenu .Naomba tuendelee na sherehe hizi kwa amani na utulivu.Ahsanteni sana”
Makofi na vigele gele vikasikika katika kila kona ya ukumbi.Watu waimshangilia Innocent kwa maneno machache aliyoyatoa.Sherehe zikaendelea hadi usiku mwingi halafu watu wakatawanyika na kurudi majumbani
kwao.
MPENZI MSOMAJI ENDELEA TUKUTANE TENA KESHO KWA MUENDELEZO WA SIMULIZI HII
KWA SIMULIZI ZAIDI USIACHE KUTEMBELEA HAPA
0 comments:
Post a Comment
Followers
MAHABA
SERENA
BEFORE I DIE
I DIED TO SAVE PRESIDENT
FAIDIKA NA MASIMULIZI
DEATH MESSENGER
CHOMBEZO ZA MASIMULIZI
MISS TANZANIA PART 2
Blog Archieves
April 2014
(57)
About Me
pettysean.blogspot.com
View my complete profile
Total Pageviews
BONYEZA "LIKE" NA UJIUNGE NASI MOJA KWA MOJA KWA SIMULIZI MPYA KILA SIKU
Powered By
masimulizi
0 comments:
Post a Comment